October 2, 2014
SAMWEL SITTA AKASILIKA BAADA YA KUTUKANWA NA JOHN MNYIKA WA CHADEMA, AELEZA KUWA YEYE NI BABA YAKE.
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta.
MWENYEKITI wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta amelieleza Bunge hilo kuwa, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), aliamua kumtukana yeye na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge.
“Bwana mmoja Mnyika ameamua kututukana mimi na Chenge…ametuita maharamia mbele ya mkutano wa hadhara huko Mwanza.
“Mimi kwake ni baba yake na kama hawezi kuniheshimu, basi aniheshimu kama mtu mzee katika nchi hii…lakini namsamehe kwa kuwa ni kijana mdogo, huenda ndio anakomaa kisiasa lakini sisi Watanzania tunatumia lugha yetu kwa staha,” alisema Sitta.
Alifafanua kuwa Mnyika ametoka chuoni juzi juzi na siasa anazoziendesha ni za kivyuo vyuo, ambazo alisema kama ndio zitakuwa siasa za chama hicho, itachukua muda kushika madaraka. Hata hivyo, alipokuwa akisema ametoka chuo kikuu juzi juzi, wajumbe walipiga kelele wakisema: “Hajamaliza chuo! hajamaliza chuo!”.
Vitisho vingine, Ukawa Mbali na waraka huo na Mnyika kufanya jitihada ili Katiba Inayopendekezwa isipatikane, Sitta alisema baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba walitishwa ili wapige kura ya Hapana na wamekiri mbele ya Katibu wa Bunge.
“Kuna wajumbe wawili wamekwenda kwa Katibu na kuonesha ujumbe wa simu wa maneno wa vitisho, wakitakiwa kuondoka hapa Dodoma, wametishwa sana kiasi tumewaruhusu waondoke.
“Mjumbe mwingine alifungiwa ndani jana (juzi) ili asije kupiga kura…kumfungia mtu ndani ni jinai sasa watu wanatuchukia mpaka wanafungia watu ndani? Ilibidi tuwasiliane na vyombo vya ulinzi na usalama ili afunguliwe na alipiga kura,” alisema Sitta.
Mbali na hao, Sitta alitoa taarifa kuwa kuna mjumbe ambaye jina lake lilimtoka, ambaye kazi yake kubwa ilikuwa kushawishi wajumbe kutoka Zanzibar, na hasa wenye muelekeo wa kuunga mkono CUF, wapige kura ya ‘Hapana’.
Mmoja wa wajumbe ambaye alishawishiwa na mjumbe huyo na kushikilia kama ‘mfungwa’ kwa mujibu wa Sitta, ni Mwanaidi Othman Twahir, ambaye alipiga kura ya ‘Hapana’.
Hata hivyo, Sitta alisema Mwenyekiti wa chama chake cha NRA, alituma ujumbe kusema kuwa mjumbe huyo hana elimu kuhusu kinachoendelea, ndio maana alipiga kura ya ‘Hapana’ lakini yuko tayari kupiga kura upya.
Sitta alisema kutokana na rai hiyo ya Mwenyekiti wa NRA, aliruhusu kura hiyo irudiwe lakini baada ya kukamilika kwa kazi ya Kamati ya Mashauriano.
Pamoja na harakati za mjumbe huyo, Sitta alisema kuna baadhi ya wajumbe wawili waliotoka nje (kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi), baada ya kusoma Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa, waliifurahia na kuona ni uzalendo kupiga kura. Hata hivyo, hakuwataja.HABARILEO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment