Pages

October 7, 2014

Lowassa: Viongozi acheni kuuza utajiri(ardhi) na kununua umasikini(fedha)

Waziri mkuu wa zamani na mbunge wa Monduli Mh Edward Lowassa akihutubia semina ya ardhi wilayani Monduli jana katika hoteli ya Emanyata ambapo alisema kuuza ardhi ni sawa na kuuza utajiri na kununua umasikini.Wilaya ya Monduli ni moja kati ya wilaya zenye matatizo makubwa ya ardhi.

Lowassa aliwaonya viongozi wa vijiji, ccm na wakuu wa kimila kuacha tabia ya kuuza ardhi hususan za wajane.
Waziri Mkuu wa zamani na mbunge wa Monduli Mh Edward Lowassa amewanyooshea vidole viongozi wa kimila(malaigwanani),viongozi wa vijiji na wale wa ccm wilayani humo, kuwa wanalaumiwa kwa kushiriki katika uuzaji ardhi kinyume na sheria.
Akifungua semina ya siku mbili juu ya ardhi kwenye ukumbi wa hoteli ya Emanyata mjini Monduli,Mh Lowassa amesema shutuma hizo zimekuwa nyingi kwa kuuza utajiri(ardhi) na kununua umasikini.
"Walikuja pale nyumbani kwangu wale watu wa maombezi(walokole), moja ya mambo waliyoyalalamikia ni uzwaji wa ardhi.wakaniambia hivi Mh mbunge hamuoni viongozi, vijiji an ccm pamoja na malaigwanan wanavyopokea rushwa na kuuza ardhi? Wanavyowadhulumu wajane?" Alisema Lowassa na kuongeza akaona kuna umuhimu wa kulijadili kwa kina suala,hilo.
Kutokana na hali hiyo Lowassa amewatahadharisha viongozi wa vijiji kuhakikisha waiondoa kero hiyo, kabla ya uchaguzi ujayo wa serikali za mitaa vinginevyo tatizo hilo litawagharimu.
Aidha Mh Lowassa ambaye yeye pamoja na mbunge wa Viti maalum Namelok Sokoine ndiyo waliyoiandaa semina hiyo, amempongeza mbunge wa zamani wa Monduli hayati Edward Moringe Sokoine, kwa kufanikisha makubaliano kati ya wilaya na jeshi kuhusiana na matumizi ya ardhi.
"Marehemu Sokoine alifanya jambo kubwa sana kwa kufikia makubaliano yale na faida yake kwetu sisi wana Monduli ni kubwa kimejengwa Hapa Chuo kikubwa cha kijeshi(TMA), na tulikubaliana tusilipwe fidia na jeshi ili tuwe na haki kwa mifugo yetu kuingia eneo lile,lakini kuna watu wameipeleka halmashauri mahakamani kupinga" alisema na kuonya kuwa" tutapambana kuhakikisha tunashinda! tumekuwa na mahusiano mazuri na jeshi na tunataka mahusiano hayo yaendelee".
Naye mbunge wa viti maalum Nameloki Sokoine alisema kuwa madhumuni ya kuandaa semina hiyo ni kutoa dira itakayofafanua nini kifanyike kuondoa tatizo hilo la uuzaji holela wa ardhi.
Amesema mifugo na binaadamu wamekuwa wakiongezeka lakini ardhi ni ile ile kwa hivyo bila ya kuwepo kwa dira na mipango thabiti hali itakuwa mbaya.
Aidha alitoa changamoto kwa mbunge wa Monduli Mh Lowassa kusaidia kupatikana kwa wawekezaji wa viwanda vya maziwa, ngozi na nyama wilayani Monduli.
"Ningependa kumuomba Mh mbunge najua hili analiweza atusaidie watu wa Monduli tupate wawekezaji wa viwanda vya ngozi, maziwa na nyama,tukiwa na viwanda hivi itasaidia wafugaji kuachana na ufugaji wa kimila wa ng'ombe wengi na badala yake kuwa na ng'ombe wachache wa kisasa wenye tija" alisema Namelok na kushangiliwa.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...