Pages

May 25, 2014

WATANZANIA WASHAURIWA KUFUGA NA KULA NYAMA YA PANYA AINA YA NDEZI.





Watanzania wameshauriwa kufuga na kula nyama ya panya aina ya ndezi kwa kuwa nyama hiyo haina mafuta mengi na pia ina virutubisho muhimu.Ndezi ni aina ya panya jamii ya nungunungu na pimbi, wakiwa wa aina mbili, ambapo wadogo huwa na uzito wa kati ya kilo nne hadi sita na wakubwa hufikia hadi kilo tisa. Wanyama hao hupendelea kuishi kwenye maeneo yanayolimwa mashamba ya miwa, ulezi na mpunga.

Mhadhiri Mwandamizi wa SUA, Idara ya Uzalishaji, Mirende Matiko alisema kuwa ingawa wanyama hao wanafugwa kwa wingi katika nchi za Afrika Magharibi, hapa nchini ufugaji wake unakabiliwa na changamoto nyingi.“Wakulima wetu hapa tunawapa wafuge, siku chache baadaye ukienda utaambiwa walikufa, lakini ukiwauliza majirani wanakuwambia ‘jamaa aliwachinja’, ni sawa na kumpa mkulima mbegu halafu anakula,” alisema Matiko.

Akizungumzia namna nyama hiyo inavyoliwa, Matiko alisema: “ Nyama yake ina viinilishe vingi, yanatupwa manyoya na miguu yake tu, vitu vingine vyote vinaliwa. Tena utumbo ndiyo mtamu sana, si unajua wanakula nyasi tu.” Pia Alisema wanyama hao wana faida nyingi kiuchumi ikiwamo kuongeza pato la kaya, kuchangia uwindaji endelevu, kutunza bioanuwai pia nyama yao ni gharama nafuu, ikilinganishwa na nyingine.

Mtu akitaka kufuga wanyama hao anatakiwa kuwa na banda madhubuti lenye ubora, chakula na maji safi yawepo bandani muda wote na upandishaji ufanyike katika muda mwafaka.  Wafugaji wakiwataka kuwakamata wanyama hao kwa umakini wanatakiwa kutumia chandarua, kuepuka kusababisha majeraha. (mwananchi, may 25)

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...