Jiji
la Abuja, ambao ndilo makao makuu ya nchi ya Nigeria, lipo katikati ya
nchi hiyo kubwa na tajiri yenye utajiri mkubwa wa mafuta na gesi.
Mji huu ulijengwa miaka ya 1980, na ukatangazwa rasmi kuwa makao makuu
ya nchi December 12, 1991, kuchukua nafasi ya jiji la Lagos, ambalo
linabakia kuwa ni jiji lenye wakazi wengi kuliko sehemu yoyote katika
Nigeria.
Kama
ilivyo ada, Abuja limekua siku hadi siku huku likishuhudia ongezeko
kubwa la watu kiasi cha serikali kulazimika kuanza kujenga miji ya
pembeni (satellite cities) katika maeneo ya Karu, Suleja, Gwagwalanda,
Lugbe, kuje na sehemu zingine ndogondogo ambako mji huo unaelekea.
Inakadiriwa
mji wa Abuja una wakaazi takriban milioni tatu, hivyo kuwa mji wa nne
wa Nigeria wenye wakaazi wengi, wa kwanza ukiwa Lagos (milioni 21), Kano
na Ibadan. Inasemekana mwaka 2006 Lagos ilikuwa na watu milioni 17.5,
kwa mujibu wa sense iliyofanyika mwaka huo. Kwa sasa, ongezeko la watu
likiwa asilimia 3.2 kwa mwaka, jiji hilo sasa lina wakaazi milioni 21.
Kwa Tanzania, jiji la Dar es salaam lina wakaazi 4,364,541 kwa mujibu wa matokeo ya sense ya watu na makaazi ya mwaka 2012.
Jiji la Dar liliacha kuwa na hadhi ya makao makuu ya nchi mwaka 1974, na mji wa Dodoma kuchukua nafasi hiyo.
Historia
ya mji wa Abuja inaanza miaka ya 1970 wakati wa migogoro ya kidini na
kikabila ilipokuwa kileleni. Ndipo mikakati ikawekwa kuwa na makao makuu
ya nchi katikati ya nchi ambapo patakuwa huru na rafiki kwa kila upande
unaopingana.
Sababu
ingine ya kuhamishia makao makuu hapo Abuja ambako awali palikuwa na
kijiji kidogo na misitu, ni msongamano kutokana na wingi wa watu katika
jiji la Lagos.
Mpango uliotumika ni kama ule wa Brazil ambao walichagua kujenga makao makuu yake Brasilia, kutoka Rio de Janeiro.
Jiografia ya Abuja inajengeka kuanzia mwamba mkubwa uitwao Aso Rock, wenye ukubwa wa mita 400.
Mji huu pia una sifa za kuwa mji uliopangika kwa ubora wa hali ya juu , tajiri na ghali sana kuishi barani Afrika.