Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo linaanza kikao chake cha
Bajeti, ambapo muda wa kuchangia na kuwasilisha bajeti za wizara
mbalimbali, umepunguzwa.
Katika
mkutano wake na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Shughuli za
Bunge, John Joel, alisema muda wa kuchangia Bajeti hiyo, umepunguzwa
kutoka dakika 10 hadi saba na muda wa uwasilishaji wa bajeti za wizara
mbalimbali, pia umepunguzwa.
Alisema
kutokana na mabadiliko hayo, sasa kila wizara itapewa siku moja ya
kuwasilisha bajeti yake na kujadiliwa. “Tumepima muda tukaona unatosha,“
alisema.
Kwa
mujibu wa Joel, Bunge litaanza kujadili hotuba ya bajeti ya Ofisi ya
Waziri Mkuu leo jioni kuanzia saa kumi baada ya kumalizika kipindi cha
maswali na majibu na kikao cha kupeana ratiba.
Joel
alisema Bunge hilo pia limeongeza siku za kufanya kazi na litakaa
mpaka siku za Jumamosi, lengo likiwa ni kuokoa muda uliopotea.
“Vikao
vitaanza saa tatu asubuhi hadi saa nane mchana na kutakuwa na mapumziko,
ambapo vitaanza tena saa 10 hadi saa mbili usiku na kwa siku za Ijumaa,
vikao vitaanza saa tatu hadi saa saba na Jumamosi vitaanza saa tatu
mpaka saa saba,” alisema.
Alisema
wabunge wawili wapya, Ridhiwani Kikwete wa Jimbo la Chalinze Mkoa wa
Pwani na Godfrey Mgimwa wa Jimbo la Kalenga Mkoa wa Iringa wataapishwa
leo, kabla ya kuanza kwa mkutano wa kawaida.
Huko
Kalenga, Mgimwa aliwashinda wagombea wenzake, Grace Tendega wa Chadema
na Richard Minja wa Chausta, kwa kupata kura 22,943 dhidi ya kura 5,800
za Chadema huku Chausta ikiambulia 143.
Ridhiwani
alishinda uchaguzi wa Jimbo la Chalinze kwa kupata kura 20,812,
akifuatiwa kwa mbali na mgombea wa Chadema, Mathayo Torongey aliyepata
kura 2,628, mgombea wa CUF, Fabian Skauti aliyepata kura 473 na mgombea
wa AFP, Munir Husein aliyeambulia kura 78.
Uchaguzi
mdogo wa Kalenga ulifanyika hivi karibuni baada ya kifo cha aliyekuwa
Mbunge wake, Dk William Mgimwa na Uchaguzi wa Chalinze, ulifanyika
baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge, Said Bwanamdogo.
No comments:
Post a Comment