Katibu Mkuu wa Chadema Dr Wilbrod
Slaa
---
CHAMA CHA DEMOKRASIA NA
MAENDELEO
UTANGULIZI
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) ilikaa kikao cha dharura ili kupokea, kujadili na kuamua juu ya
utetezi wa mashtaka ya ukiukaji wa Katiba, Kanuni na Mwongozo wa Chama
yaliyokuwa yanawakabili aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Zitto Zuberi Kabwe,
aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu Dr. Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa
Chama Mkoa wa Arusha Samson Mwigamba.
Kikao hicho cha dharura kilifanyika Dar es Salaam kati
ya tarehe 3-4 Januari, 2014. Kabla ya kuanza kwa kikao, Kamati Kuu ilipokea
taarifa kwamba Zitto Zuberi Kabwe amefungua mashtaka dhidi ya CHADEMA katika
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam. Aidha, Kamati Kuu ilijulishwa
kwamba Mahakama Kuu imetoa amri ya zuio la muda ya kuizuia Kamati Kuu au chombo
kingine cha Chama kutokukaa, kujadili na kuamua suala la uanachama wa Zitto
Zuberi Kabwe. Kutokana na amri hiyo ya Mahakama Kuu, Kamati Kuu haikujadili na
kuamua juu ya mashtaka dhidi yake.
MASHTAKA
Watuhumiwa wote watatu walishtakiwa jumla ya mashtaka
11 yanayohusu ukiukaji wa vifungu mbali mbali vya Katiba ya Chama, Kanuni za
Uendeshaji Kazi za Chama, Kanuni za Kusimamia Shughuli, Mwenendo na Maadili ya
Wabunge wa Chama na Mwongozo wa Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi za Uongozi
Kwenye Chama, Mabaraza na Serikali. Mashtaka yote yalitokana na watuhumiwa
kuandaa kile kinachoitwa Mkakati wa Mabadiliko, 2013 kama
ifuatavyo:
1.
Kukashifu Viongozi Wakuu wa Chama, yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa Mh.
Freeman A. Mbowe, na Katibu Mkuu Dr. Wilbrod P. Slaa;
2.
Kutokuwa wakweli na wawazi kwa kushirikiana na vikundi vya majungu kwa
kuanzisha na kuratibu mtandao wa siri ulioitwa ‘Mtandao wa Ushindi’ nje ya
utaratibu wa Chama ili kumwezesha Zitto Zuberi Kabwe kutwaa nafasi ya Mwenyekiti
wa Chama Taifa;
3.
Kutoa tuhuma za uongo dhidi ya viongozi wa Chama na bila kupitia vikao
halali vya Chama;
4.
Kujihusisha na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini na ukanda vyenye
makusudi ya kubaguana ndani ya Chama na miongoni mwa
jamii;
5.
Kujihusisha na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro
ndani ya uongozi wa Chama na wanachama wake;
6.
Kuandaa na kutekeleza mpango wa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama
Taifa bila kutangaza kusudio la kufanya hivyo kwa mujibu wa Mwongozo wa
Chama;
7.
Kutengeneza makundi na mitandao haramu ya kuwania uongozi ndani ya Chama
kinyume cha Mwongozo wa Chama;
8.
Kuwachafua viongozi na wanachama wenye nia au kusudio la kugombea nafasi
ya Mwenyekiti wa Chama kinyume cha Mwongozo wa Chama;
9.
Kujihusisha na upinzani dhidi ya Chama na makundi ya majungu ya
kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa uchaguzi wa
Chama;
10.
Kukashifu Chama na viongozi wa Chama nje ya Bunge kinyume cha Kanuni za
Maadili ya Wabunge; na
11.
Kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama kinyume cha Kanuni za Maadili ya
Wabunge.
UTETEZI WA WATUHUMIWA
Watuhumiwa wote walijitetea kwa maandishi. Zaidi ya
utetezi huo wa maandishi, Dr. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba waliitikia wito
wa Kamati Kuu wa kujitetea kwa mdomo mbele yake.
Hata hivyo, siku ya utetezi wao, ni Dr. Kitila Mkumbo
peke yake aliyejitokeza kwenye Kamati Kuu na kujitetea kwa mdomo. Katika utetezi
wake wa maandishi, licha ya kukiri kushiriki katika maandalizi ya kile
kinachoitwa Mkakati wa Mabadiliko 2013, Dr. Kitila Mkumbo – kama ilivyokuwa kwa
Samson Mwigamba – alikanusha na kukataa tuhuma zote za kukiuka Katiba ya Chama,
Kanuni zake na Mwongozo wa Chama.
Kwa maneno yake mwenyewe, Dr. Mkumbo alikanusha “kila
tuhuma mojamoja na kwa ujumla wake dhidi yake”, na kwamba mashtaka hayo sio ya
kweli na hakuvunja Katiba, Kanuni wala Mwongozo wa Chama.
Aidha, licha ya kukiri kwake katika kikao cha Kamati
Kuu ya Novemba mwaka jana kwamba walioshiriki kuandaa Mkakati huo ni pamoja na
mtu anayejulikana kama M2, mara hii Dr. Kitila Mkumbo aliiambia Kamati Kuu
kwamba “waraka husika ulikuwa ni wa siri na haukuwahi kusambazwa wala
kushirikisha … wanachama au viongozi wa CHADEMA isipokuwa mimi binafsi na Samson
Mwigamba….” Vile vile, ijapokuwa katika Kamati Kuu ya Novemba mwaka jana Dr.
Mkumbo alidai kutokumfahamu kabisa M2, mara hii aliiambia Kamati Kuu kwamba
anamfahamu fika M2 lakini hayuko tayari kumtaja mbele ya Kamati Kuu hadi
atakapowasiliana naye!
USHIRIKI WA ZITTO ZUBERI KABWE KATIKA MKAKATI WA
MABADILIKO
Itakumbukwa kwamba katika kikao cha Novemba 2013, Dr.
Kitila Mkumbo na Zitto Zuberi Kabwe walikataa kata kata kuhusika kwa Zitto
Zuberi Kabwe katika maandalizi ya Mkakati wa Mabadiliko.
Aidha, Zitto Zuberi Kabwe alidai mbele ya Kamati Kuu
kwamba alikuwa ameusikia Mkakati huo kwa mara ya kwanza kwenye Kamati Kuu, na
amerudia kauli hiyo mara nyingi na hadharani tangu avuliwe nafasi zake za
uongozi. Hata hivyo, wakati wa mahojiano na wajumbe wa Kamati Kuu, Dr. Kitila
Mkumbo alikiri kwamba yeye na waandishi wenzake wa Mkakati walimpa Zitto Zuberi
Kabwe briefing juu ya Mkakati na kwamba alikuwa anaufahamu.
Ukweli huu pia umethibitishwa na mawasiliano ya
baruapepe iliyotumwa na Zitto Zuberi Kabwe mwenyewe kwa mtu anayeitwa ‘CHADEMA
Mpya 2014’ tarehe 27 Oktoba, 2013, karibu mwezi mmoja kabla ya kikao cha Kamati
Kuu ya Novemba iliyowavua madaraka.
Zaidi ya hayo, baada ya kuonyeshwa waraka wa Chama juu
ya mabadiliko ya Katiba ya Chama uliotumwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa
Chama wakati huo Shaibu Akwilombe Julai 2006 unaothibitisha kwamba mabadiliko ya
Katiba yaliyoondoa ukomo wa uongozi yalifanywa kwa uwazi na kwa kushirikisha
ngazi zote za Chama, Dr. Kitila Mkumbo alikataa kata kata kujadili suala hilo
kwa madai kwamba tayari walishapeleka malalamiko yao kwa Msajili wa Vyama vya
Siasa.
Kuhusu tuhuma zao kwamba kuna ufisadi na ubadhirifu wa
fedha za Chama unaofanywa na Mwenyekiti wa Chama, Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa
Fedha Anthony Komu na kwamba taarifa za matumizi ya fedha ni siri ya viongozi
hao watatu, Dr. Mkumbo alionyeshwa taarifa mbali mbali za fedha zilizowasilishwa
mbele ya vikao vya Kamati Kuu a Chama ambavyo yeye mwenyewe na Zitto Zuberi
Kabwe walishiriki kama wajumbe wa Kamati Kuu. Aidha, Dr. Mkumbo alionyeshwa
taarifa za kibenki zinazoonyesha jinsi michango ya Mzee Jaffer Sabodo na
michango mingine ya watu binafsi zilivyopokelewa na kutumiwa na taarifa zake
kuwasilishwa kwenye vikao vya Kamati Kuu walivyohudhuria yeye na Zitto Zuberi
Kabwe.
Zaidi ya hayo, Dr. Mkumbo alionyeshwa nyaraka za
manunuzi ya vifaa vya Chama kama vile vile pikipiki, kadi, bendera, n.k, na
jinsi ambavyo uamuzi wa manunuzi hayo yalifanywa na Kamati Kuu ambayo wao
wenyewe ni wajumbe na walihudhuria vikao husika. Vile vile, Dr. Mkumbo
alionyeshwa ushahidi wa maandishi kwamba Mwenyekiti wa Chama hakuhusika kwa
namna yoyote ile katika manunuzi hayo na hakuna karatasi yoyote inayoonyesha
saini ya Mwenyekiti katika manunuzi ya vifaa hivyo.
Aidha, Dr. Mkumbo hakuweza kuthibitisha kwa namna
yoyote kwamba CHADEMA ina mkataba wowote na watu binafsi wanaouza vifaa vya
uenezi vya Chama kwa vile Kamati Kuu ya Chama katika vikao ambavyo vilihudhuriwa
na Dr. Mkumbo na Zitto Zuberi Kabwe ilikwisharuhusu wafanya biashara binafsi
kuagiza vifaa hivyo na kuviuza kwa wanachama wanaotaka kuvinunua. Kwenye yote
haya, Dr. Kitila Mkumbo hakuwa na lolote la maana la kuiambia Kamati
Kuu.
MAAMUZI YA KAMATI KUU
Baada ya kusikiliza utetezi wa Dr. Kitila Mkumbo na
baada ya kumhoji kwa kirefu, Kamati Kuu imeridhika bila mashaka yoyote kwamba
Mkakati wa Mabadiliko 2013 haukuwa na lengo la kumwezesha Zitto Zuberi Kabwe
kutwaa nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama peke yake. Mkakati huo ulikuwa na
malengo makubwa zaidi ya kukibomoa Chama kwa kukichafua kwa wananchi na
kuwachafua viongozi wake wa juu kwa kutumia tuhuma za uongo za ufisadi. Hii ni
kwa sababu, kwa maoni ya Kamati Kuu, Chama cha siasa ambacho viongozi wake wa
juu wanatuhumiwa kwa ufisadi hakiwezi kuaminiwa na wananchi kama tumaini lao la
ukombozi.
Kamati Kuu imeridhika kwa ushahidi wa nyaraka mbali
mbali zilizoandaliwa na Zitto Zuberi Kabwe mwenyewe ama na mawakala wake
wakitumia vitambulisho bandia katika mitandao ya mawasiliano ya kijamii kwamba
mkakati wa kukibomoa Chama umeandaliwa na kutekelezwa kwa muda
mrefu.
Mkakati huo ulihusisha pia hujuma dhidi ya Chama kwa
kuwaengua wagombea wake katika chaguzi mbali mbali kama ilivyotokea katika
majimbo ya Mpanda Mashariki, Musoma Vijijini na Singida Mjini ambapo Zitto
Zuberi Kabwe alishiriki moja kwa moja.
Kwa sababu zote hizo, Kamati Kuu imeazimia
ifuatavyo:
1.
Kwamba kuanzia tarehe ya uamuzi wake, Dr. Kitila Mkumbo na Samson
Mwigamba wafukuzwe uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA);
na
2.
Kwamba, kwa vile Zitto Zuberi Kabwe amekishtaki Chama kinyume na matakwa
ya Katiba ya Chama na Kanuni zake, na kwa vile Mahakama Kuu imeamuru vikao vyote
vya Chama visijadili wala kuamua suala lolote linalohusu uanachama wa Zitto
Zuberi Kabwe, viongozi wa ngazi zote za Chama, wanachama, washabiki na wapenzi
wa CHADEMA popote walipo katika nchi yetu na nje ya Tanzania wasishiriki wala
kusaidia kwa namna yoyote mikutano yoyote ya nje au ya ndani au shughuli
nyingine yoyote ya kisiasa itakayofanywa na Zitto Zuberi Kabwe na mawakala wake
kwa jina la CHADEMA.
——————————–
Dr. Wilbrod P.
Slaa
KATIBU MKUU
No comments:
Post a Comment