MAAMUZI
YA KAMATI KUU YA CHADEMA KUWAVUA UANACHAMA DKT. KITILA NA MWIGAMBA
MAAZIMIO
YA KIKAO CHA DHARURA CHA KAMATI KUU YA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO
(CHADEMA) KUHUSU HATUA ZA KINIDHAMU DHIDI YA WANACHAMA ZITTO ZUBERI KABWE, DR.
KITILA MKUMBO NA SAMSON MWIGAMBA
UTANGULIZI
Kamati
Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ilikaa kikao cha dharura ili
kupokea, kujadili na kuamua juu ya utetezi wa mashtaka ya ukiukaji wa Katiba,
Kanuni na Mwongozo wa Chama yaliyokuwa yanawakabili aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu
Zitto Zuberi Kabwe, aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu Dr. Kitila Mkumbo na
aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Mkoa wa Arusha Samson Mwigamba. Kikao hicho cha
dharura kilifanyika Dar es Salaam kati ya tarehe 3-4 Januari, 2014. Kabla ya
kuanza kwa kikao, Kamati Kuu ilipokea taarifa kwamba Zitto Zuberi Kabwe
amefungua mashtaka dhidi ya CHADEMA katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar
es Salaam. Aidha, Kamati Kuu ilijulishwa kwamba Mahakama Kuu imetoa amri ya zuio
la muda ya kuizuia Kamati Kuu au chombo kingine cha Chama kutokukaa, kujadili na
kuamua suala la uanachama wa Zitto Zuberi Kabwe. Kutokana na amri hiyo ya
Mahakama Kuu, Kamati Kuu haikujadili na kuamua juu ya mashtaka dhidi
yake.
MASHTAKA
Watuhumiwa wote watatu walishtakiwa jumla ya mashtaka 11 yanayohusu
ukiukaji wa vifungu mbali mbali vya Katiba ya Chama, Kanuni za Uendeshaji Kazi
za Chama, Kanuni za Kusimamia Shughuli, Mwenendo na Maadili ya Wabunge wa Chama
na Mwongozo wa Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi za Uongozi Kwenye Chama,
Mabaraza na Serikali. Mashtaka yote yalitokana na watuhumiwa kuandaa kile
kinachoitwa Mkakati wa Mabadiliko, 2013 kama ifuatavyo:
1. Kukashifu Viongozi Wakuu wa Chama, yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa
Mh. Freeman A. Mbowe, na Katibu Mkuu Dr. Wilbrod P.
Slaa;
2. Kutokuwa
wakweli na wawazi kwa kushirikiana na vikundi vya majungu kwa kuanzisha na
kuratibu mtandao wa siri ulioitwa ‘Mtandao wa Ushindi’ nje ya utaratibu wa Chama
ili kumwezesha Zitto Zuberi Kabwe kutwaa nafasi ya Mwenyekiti wa Chama
Taifa;
3. Kutoa
tuhuma za uongo dhidi ya viongozi wa Chama na bila kupitia vikao halali vya
Chama;
4. Kujihusisha na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini na ukanda
vyenye makusudi ya kubaguana ndani ya Chama na miongoni mwa
jamii;
5. Kujihusisha na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro
ndani ya uongozi wa Chama na wanachama wake;
6. Kuandaa
na kutekeleza mpango wa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa bila
kutangaza kusudio la kufanya hivyo kwa mujibu wa Mwongozo wa
Chama;
7. Kutengeneza makundi na mitandao haramu ya kuwania uongozi ndani ya
Chama kinyume cha Mwongozo wa Chama;
8. Kuwachafua viongozi na wanachama wenye nia au kusudio la kugombea
nafasi ya Mwenyekiti wa Chama kinyume cha Mwongozo wa
Chama;
9. Kujihusisha na upinzani dhidi ya Chama na makundi ya majungu ya
kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa uchaguzi wa
Chama;
10. Kukashifu Chama na viongozi wa Chama nje ya Bunge kinyume cha Kanuni
za Maadili ya Wabunge; na
11. Kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama kinyume cha Kanuni za Maadili ya
Wabunge.
UTETEZI
WA WATUHUMIWA.
Watuhumiwa wote walijitetea kwa maandishi. Zaidi ya utetezi huo wa
maandishi, Dr. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba waliitikia wito wa Kamati Kuu wa
kujitetea kwa mdomo mbele yake. Hata hivyo, siku ya utetezi wao, ni Dr. Kitila
Mkumbo peke yake aliyejitokeza kwenye Kamati Kuu na kujitetea kwa mdomo. Katika
utetezi wake wa maandishi, licha ya kukiri kushiriki katika maandalizi ya kile
kinachoitwa Mkakati wa Mabadiliko 2013, Dr. Kitila Mkumbo – kama ilivyokuwa kwa
Samson Mwigamba – alikanusha na kukataa tuhuma zote za kukiuka Katiba ya Chama,
Kanuni zake na Mwongozo wa Chama. Kwa maneno yake mwenyewe, Dr. Mkumbo
alikanusha “kila tuhuma mojamoja na kwa ujumla wake dhidi ya[ke]”, na kwamba
mashtaka hayo sio ya kweli na hakuvunja Katiba, Kanuni wala Mwongozo wa
Chama.
Aidha,
licha ya kukiri kwake katika kikao cha Kamati Kuu ya Novemba mwaka jana kwamba
walioshiriki kuandaa Mkakati huo ni pamoja na mtu anayejulikana kama M2, mara
hii Dr. Kitila Mkumbo aliiambia Kamati Kuu kwamba “waraka husika ulikuwa ni wa
siri na haukuwahi kusambazwa wala kushirikisha … wanachama au viongozi wa
CHADEMA isipokuwa mimi binafsi na Samson Mwigamba….” Vile vile, ijapokuwa katika
Kamati Kuu ya Novemba mwaka jana Dr. Mkumbo alidai kutokumfahamu kabisa M2, mara
hii aliiambia Kamati Kuu kwamba anamfahamu fika M2 lakini hayuko tayari kumtaja
mbele ya Kamati Kuu hadi atakapowasiliana naye!
USHIRIKI
WA ZITTO ZUBERI KABWE KATIKA MKAKATI WA MABADILIKO.
Itakumbukwa kwamba katika kikao cha Novemba 2013, Dr. Kitila Mkumbo
na Zitto Zuberi Kabwe walikataa kata kata kuhusika kwa Zitto Zuberi Kabwe katika
maandalizi ya Mkakati wa Mabadiliko. Aidha, Zitto Zuberi Kabwe alidai mbele ya
Kamati Kuu kwamba alikuwa ameusikia Mkakati huo kwa mara ya kwanza kwenye Kamati
Kuu, na amerudia kauli hiyo mara nyingi na hadharani tangu avuliwe nafasi zake
za uongozi. Hata hivyo, wakati wa mahojiano na wajumbe wa Kamati Kuu, Dr. Kitila
Mkumbo alikiri kwamba yeye na waandishi wenzake wa Mkakati walimpa Zitto Zuberi
Kabwe briefing juu ya Mkakati na kwamba alikuwa anaufahamu. Ukweli huu pia
umethibitishwa na mawasiliano ya baruapepe iliyotumwa na Zitto Zuberi Kabwe
mwenyewe kwa mtu anayeitwa ‘CHADEMA Mpya 2014’ tarehe 27 Oktoba, 2013, karibu
mwezi mmoja kabla ya kikao cha Kamati Kuu ya Novemba iliyowavua
madaraka.
Zaidi ya
hayo, baada ya kuonyeshwa waraka wa Chama juu ya mabadiliko ya Katiba ya Chama
uliotumwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama wakati huo Shaibu Akwilombe
Julai 2006 unaothibitisha kwamba mabadiliko ya Katiba yaliyoondoa ukomo wa
uongozi yalifanywa kwa uwazi na kwa kushirikisha ngazi zote za Chama, Dr. Kitila
Mkumbo alikataa kata kata kujadili suala hilo kwa madai kwamba tayari
walishapeleka malalamiko yao kwa
Msajili wa Vyama vya Siasa.
Kuhusu
tuhuma zao kwamba kuna ufisadi na ubadhirifu wa fedha za Chama unaofanywa na
Mwenyekiti wa Chama, Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Fedha Anthony Komu na kwamba
taarifa za matumizi ya fedha ni siri ya viongozi hao watatu, Dr. Mkumbo
alionyeshwa taarifa mbali mbali za fedha zilizowasilishwa mbele ya vikao vya
Kamati Kuu a Chama ambavyo yeye mwenyewe na Zitto Zuberi Kabwe walishiriki kama
wajumbe wa Kamati Kuu. Aidha, Dr. Mkumbo alionyeshwa taarifa za kibenki
zinazoonyesha jinsi michango ya Mzee Jaffer Sabodo na michango mingine ya watu
binafsi zilivyopokelewa na kutumiwa na taarifa zake kuwasilishwa kwenye vikao
vya Kamati Kuu walivyohudhuria yeye na Zitto Zuberi
Kabwe.
Zaidi ya
hayo, Dr. Mkumbo alionyeshwa nyaraka za manunuzi ya vifaa vya Chama kama vile
vile pikipiki, kadi, bendera, n.k, na jinsi ambavyo uamuzi wa manunuzi hayo
yalifanywa na Kamati Kuu ambayo wao wenyewe ni wajumbe na walihudhuria vikao
husika. Vile vile, Dr. Mkumbo alionyeshwa ushahidi wa maandishi kwamba
Mwenyekiti wa Chama hakuhusika kwa namna yoyote ile katika manunuzi hayo na
hakuna karatasi yoyote inayoonyesha saini ya Mwenyekiti katika manunuzi ya vifaa
hivyo. Aidha, Dr. Mkumbo hakuweza kuthibitisha kwa namna yoyote kwamba CHADEMA
ina mkataba wowote na watu binafsi wanaouza vifaa vya uenezi vya Chama kwa vile
Kamati Kuu ya Chama katika vikao ambavyo vilihudhuriwa na Dr. Mkumbo na Zitto
Zuberi Kabwe ilikwisharuhusu wafanya biashara binafsi kuagiza vifaa hivyo na
kuviuza kwa wanachama wanaotaka kuvinunua. Kwenye yote haya, Dr. Kitila Mkumbo
hakuwa na lolote la maana la kuiambia Kamati Kuu.
MAAMUZI
YA KAMATI KUU.
Baada ya
kusikiliza utetezi wa Dr. Kitila Mkumbo na baada ya kumhoji kwa kirefu, Kamati
Kuu imeridhika bila mashaka yoyote kwamba Mkakati wa Mabadiliko 2013 haukuwa na
lengo la kumwezesha Zitto Zuberi Kabwe kutwaa nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa
Chama peke yake. Mkakati huo ulikuwa na malengo makubwa zaidi ya kukibomoa Chama
kwa kukichafua kwa wananchi na kuwachafua viongozi wake wa juu kwa kutumia
tuhuma za uongo za ufisadi. Hii ni kwa sababu, kwa maoni ya Kamati Kuu, Chama
cha siasa ambacho viongozi wake wa juu wanatuhumiwa kwa ufisadi hakiwezi
kuaminiwa na wananchi kama tumaini lao la ukombozi.
Kamati
Kuu imeridhika kwa ushahidi wa nyaraka mbali mbali zilizoandaliwa na Zitto
Zuberi Kabwe mwenyewe ama na mawakala wake wakitumia vitambulisho bandia katika
mitandao ya mawasiliano ya kijamii kwamba mkakati wa kukibomoa Chama umeandaliwa
na kutekelezwa kwa muda mrefu. Mkakati huo ulihusisha pia hujuma dhidi ya Chama
kwa kuwaengua wagombea wake katika chaguzi mbali mbali kama ilivyotokea katika
majimbo ya Mpanda Mashariki, Musoma Vijijini na Singida Mjini ambapo Zitto
Zuberi Kabwe alishiriki moja kwa moja.
Kwa
sababu zote hizo, Kamati Kuu imeazimia ifuatavyo:
1. Kwamba
kuanzia tarehe ya uamuzi wake, Dr. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba wafukuzwe
uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA);
na
2. Kwamba,
kwa vile Zitto Zuberi Kabwe amekishtaki Chama kinyume na matakwa ya Katiba ya
Chama na Kanuni zake, na kwa vile Mahakama Kuu imeamuru vikao vyote vya Chama
visijadili wala kuamua suala lolote linalohusu uanachama wa Zitto Zuberi Kabwe,
viongozi wa ngazi zote za Chama, wanachama, washabiki na wapenzi wa CHADEMA
popote walipo katika nchi yetu na nje ya Tanzania wasishiriki wala kusaidia kwa
namna yoyote mikutano yoyote ya nje au ya ndani au shughuli nyingine yoyote ya
kisiasa itakayofanywa na Zitto Zuberi Kabwe na mawakala wake kwa jina la
CHADEMA.
--------------------------------
Dr.
Wilbrod P. Slaa
KATIBU
MKUU
No comments:
Post a Comment