Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mazungumzo na Rais Paul Kagame wa Rwanda wakati walipokutaba na kufanya mazungumzo ya faragha, katika Hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort, jijini Kampala, Uganda.
UHUSIANO tete baina ya Tanzania na Rwanda bado unaendelea kupita chini kwa chini, licha ya viongozi wakuu wa nchi hizo kukutana juzi mjini Kampala, Uganda na kufanya mazungumzo ambayo hayakufika mwisho.
Uhusiano huo ulizorota baada ya Rais Jakaya Kikwete kumshauri Rais Paul Kagame, kukutana na waasi wa kikundi cha FDLR kinachopigana mashariki mwa nchi ya Demokrasia ya Kongo (DRC).
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema marais hao walikutana juzi ambapo kila mmoja aliwasilisha dukuduku lake kwa mwenzake.
“Walikutana na walipotoka walionyesha nyuso za furaha, kwa kuwa kila mmoja aliwasilisha dukud
uku lake. Kila mmoja alieleza jinsi alivyopokea na kutafsiri kauli ya mwenzake.
“Kila mmoja alipata fursa ya kujadili ukweli na kile anachokijua, ikiwa lengo ni kutafuta suluhu na kurejesha uhusiano, amani na ushirikiano wa kimaendeleo kama ulivyokuwa.
“Mkutano ule umekata majungu yaliyokuwa yakiendelea, kwa sababu pale kila upande uliweza kueleza ukweli wa jambo na nini anachokijua, huku busara na elimu ya kueleweshana ikitumika zaidi.
“Sasa kilichokuwa kikielezwa kila upande kilikuwa kinaandikwa, sasa kinachofuata ni vikao na mikutano mingine ya kujadiliana kila upande.
“Hivi sasa ni mapema sana kueleza wazi kilichosemwa kila upande, lakini baada ya vikao kuanza tutajua nani alikosea au mmoja wapo alichukulia upande mwingine sivyo,” alisema.
Membe alisema kuwa katika kikao hicho, walijadili suala la kudaiwa Tanzania imewafukuza wakimbizi wa Rwanda na nchi nyingine ikiwamo Burundi, ambapo alisema taratibu zilifuatwa na waliokimbia ni wahamiaji haramu.
Tanzania kutengwa EAC
Akizungumzia sakata linaloendelea la Tanzania kutoalikwa katika vikao vya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Membe alisema nchi hizo hazina ubavu wa kuitenga Tanzania, kutokana na historia yake.
“Naomba nilieleze hili kwa kina, kwamba ifahamike kuwa dunia na Afrika kwa ujumla ipo na Tanzania, naomba Watanzania wasiwaze wala kuhangaika na ajenda za kutengwa kwetu.
“Kwanza Tanzania tuna uchumi mzuri, usalama, madini, chakula cha kutoka, bandari na hata raia wa nchi hizo wakipata matatizo wanakimbilia kwetu na misaada tunatoa kwao.
“Tanzania ndio iliyopewa kibali cha kumiliki anga ya nchi za Afrika Mashariki, hata wakifanya vipi watarudi Tanzania, ndio maana hatutaki kuburuzwa, nafikiri wanafanya jambo wasilolijua.
“Pamoja na mambo mengi yaliyojadiliwa, sisi Tanzania tumeomba baada ya vikao vyao wanavyofanya watupatie taarifa walichojadili na lengo lao kwa sababu bado ni wanachama, tunasema mpango wao hauwezi kuitingisha hata wasipotumia ardhi yetu,” alisema.
Mzozo Ziwa Nyasa
Kuhusu mgogoro kati ya Tanzania na Malawi kutofautiana juu ya mpaka katika Ziwa Nyasa, Membe alisema hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa chini ya marais wastaafu wa Afrika.
Alisema kuwa muda wowote Tanzania itaitwa kutoa maelezo yao, ambapo itawakilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Membe alisema baada ya nchi zote kutoa maelezo yao na vielelezo, pande zote mbili zitaunda jopo la mawakili na kwenda kushirikiana na jopo linaloshughulikia mgogoro huo kutoa uamuzi.
Waasi wa M23
Akizungumzia suala la mgogoro wa vikundi vya waasi nchini Kongo, alisema kuwa viongozi wa nchi wanachama walijadiliana kwa kina suala la kuzorota amani hasa katika miji ya Goma na Kivu.
Membe alisema wakuu wa nchi za Maziwa Makuu, wamemwagiza na kumpa siku 17 Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kusuluhisha mgogoro huo kwa kuwakutanisha viongozi wa M23 na Rais wa DRC Kongo, Joseph Kabila.
“Siku hizo zimegawanywa, siku tatu ni kuwakutanisha viongozi na siku zilizobaki ni kufanya majadiliano ya amani kutafuta suluhisho.
“Pia wakati shughuli hiyo ikiendelea, imeamuliwa nchi za Maziwa Makuu kwa kushirikiana na UN watakuwa karibu na vikundi vingine vya waasi, kuhakikisha vinaweka silaha chini.
“Na mwisho wamependekeza uchunguzi ufanyike juu ya mabomu yaliyorushwa hivi karibuni na kuua raia na wanajeshi wa UN akiwamo wa askari mmoja wa Tanzania na kujeruhi watano,” alisema.
Ruto, Kenyatta ICC
Membe alisema kuwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na makamu wake, William Ruto wanakabiliwa na kesi ya jinai ya mauaji ya raia zaidi ya 1,000 katika uchunguzi mkuu wa 1997.
“Viongozi hao wanakabiliwa na kesi kule ICC na wanatakiwa kwenda kusikiliza kesi yao kuanzia Septemba 10 hadi mwisho wa mwezi huu, sasa kazi iliyopo nchi itabaki na kiongozi gani na kwa mujibu wa katiba yao lazima Rais akitoka makamu awepo.
“Sasa hili limeleta mvutano hadi kukata rufaa ili kesi iweze kusikilizwa nchini Kenya au mawakili wa viongozi hao waende kusimamia kesi hiyo huko ICC hadi siku ya hukumu, lakini imeshindikana.
“Suala hili bado ni gumu na tunaendelea kuangalia jinsi nchi za Afrika tunavyoweza kuisaidia Kenya, pia tumegundua hii mahakama ya ICC ina ajenga na viongozi wa Afrika kwa sababu inawakandamiza sana,” alisema. MTANZANIA.
No comments:
Post a Comment