SERIKALI YAJENGA UWEZO WA WALIMU KUTUMIA TEKNOLOJIA DARASANI




Na Mwandishi Wetu
OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) imeanza kuwajengea uwezo walimu wa shule za sekondari za Serikali katika Jiji la Arusha na Halmashauri ya Arusha kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika ufundishaji, ujifunzaji na upimaji wa wanafunzi.

Mafunzo hayo ya siku nne yanayofanyika katika Hoteli ya Gold Crest jijini Arusha kuanzia Septemba mosi hadi nne, 2026, yanafanyika kwa ushirikiano kati ya OR-TAMISEMI, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE).

Mafunzo hayo yanaendeshwa kupitia Mradi wa ICT Transforming Education in Africa – Awamu ya Tatu, unaoungwa mkono na Mfuko wa Korean Funds-in-Trust (KFIT), kwa lengo la kuwapatia walimu ujuzi wa vitendo wa kuunganisha TEHAMA katika ufundishaji, ujifunzaji na upimaji.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu kutoka OR-TAMISEMI, Melchiory Baltazary, alisema Serikali imejipanga kuendelea kuimarisha uwezo wa walimu kutumia TEHAMA kwa ufanisi ili kuboresha ubora wa elimu nchini.

Alisema ushirikiano kati ya Serikali, UNESCO na TIE umekuwa muhimu katika kuwapatia walimu ujuzi wa vitendo ambao wanaweza kuutumia moja kwa moja katika shughuli za ufundishaji na ujifunzaji.

Baltazary aliwataka walimu hao kutumia kikamilifu maarifa wanayoyapata na kuyasambaza kwa walimu wenzao ambao hawakupata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo.

Alisema mfumo wa mafunzo wa kueneza ujuzi (cascade training) utasaidia kuwafikia walimu wengi zaidi katika shule na halmashauri zao.

Pia aliwahimiza walimu kuendelea kutumia mifumo na rasilimali za kidijitali zinazotolewa na Serikali ili kuimarisha uwezo wao kitaaluma hata baada ya kumalizika kwa mafunzo ya ana kwa ana.

Kwa upande wake, Mkuu wa Sekta ya Elimu katika Ofisi ya UNESCO Dar es Salaam, Dkt. Faith Shayo, alisema uimarishaji wa ujuzi wa kidijitali kwa walimu ni muhimu ili kuhakikisha mfumo wa elimu unaendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.

Dkt. Shayo aliwataka walimu hao kushirikisha wenzao maarifa na ujuzi wanaoupata ili kuongeza idadi ya walimu wanaoweza kutumia TEHAMA katika elimu

Alisema walimu wana nafasi kubwa katika mabadiliko ya elimu kwa kuwa ndio wanaohakikisha teknolojia na ubunifu vinatafsirika kuwa mbinu bora za ufundishaji ndani ya madarasa.

“Tunatarajia mtashirikisha walimu wenzenu mnayojifunza hapa ili nao waweze kwenda sambamba na mabadiliko haya katika elimu,” alisema.

Aliongeza kuwa teknolojia inapaswa kutumika kuboresha ubora wa ufundishaji na ujifunzaji, kuongeza upatikanaji wa maarifa na kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi unaohitajika katika karne ya 21.

Naye Afisa Taaluma wa Mkoa wa Arusha, Oscar Kapinga, alisema matumizi sahihi ya teknolojia yanaweza kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji pamoja na kuongeza fursa kwa wanafunzi kupata maarifa na rasilimali mbalimbali za kielimu.

Aliwataka walimu kuhakikisha matumizi ya TEHAMA yanaelekezwa katika maeneo yanayochangia moja kwa moja kuboresha matokeo ya ujifunzaji.

Mafunzo hayo yanahusisha maeneo mbalimbali ya ujuzi wa kidijitali, ikiwamo matumizi ya zana na majukwaa ya kujifunzia kidijitali, matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na upimaji, Rasilimali Huria za Kielimu (OER), utafutaji wa taarifa mtandaoni na matumizi ya teknolojia katika utekelezaji wa mtaala.

Pia walimu wanafundishwa mbinu shirikishi za ufundishaji, usimamizi wa kumbukumbu na taarifa za shule, uandaaji wa rasilimali za kujifunzia kidijitali, utengenezaji wa maudhui ya kielimu kwa njia ya sauti na picha pamoja na matumizi ya Akili Bandia (AI) katika elimu.

Walimu hao wanatumia mfumo wa TIE wa Mafunzo Endelevu ya Maendeleo ya Kitaaluma kwa Walimu (TCPD LMS), unaounganishwa na mfumo wa Serikali wa MEWAKA, kupata vifaa vya mafunzo na kukamilisha moduli mbalimbali.

Akieleza utekelezaji wa mradi huo, Gabriela Lucas kutoka Sekta ya Elimu ya UNESCO, alisema mpango huo unaolenga kujenga uwezo wa walimu kutumia teknolojia kwa ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji unatumia pia mifumo iliyopo ya Serikali katika kuwawezesha walimu kuendelea kujifunza.

Alisema UNESCO inalenga kuhakikisha kila mwalimu anakuwa na uwezo wa kutumia TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji.

Kwa mujibu wa Lucas, mfumo wa ICT-CSTT una viwango mbalimbali vya umahiri vinavyowawezesha walimu kukuza ujuzi wao wa kidijitali hatua kwa hatua kulingana na kiwango walichonacho.

Alisema mfumo huo una jumla ya moduli 15, huku mafunzo ya Arusha yakilenga viwango vya Mwanzo na Kati vinavyohusisha moduli 10, pamoja na utangulizi wa moduli tano za kiwango cha Juu.

Alifafanua kuwa mradi huo unatumia mfumo wa mafunzo ya kueneza ujuzi ambapo walimu wanaopata mafunzo wanatarajiwa kuwafundisha wenzao katika shule zao.

Alisema mafunzo hayo yameanza Morogoro na sasa yanaendelea Arusha, huku mradi ukitekelezwa pia nchini Namibia na Uganda.

Naye mwezeshaji kutoka TIE, Watson Mtewele, alisema moduli zinazotumika katika mafunzo hayo zinapatikana kupitia mfumo wa maendeleo endelevu ya kitaaluma kwa walimu unaojulikana kama MEWAKA.

Alisema mfumo huo unawawezesha walimu kuendelea kujifunza na kuimarisha ujuzi wao wa kitaaluma hata baada ya kumaliza mafunzo ya ana kwa ana.

Jumla ya walimu 64 kutoka Jiji la Arusha na Halmashauri ya Arusha wanashiriki mafunzo hayo na wanatarajiwa kurejea shuleni kwao na kuwasaidia walimu wenzao kutumia zana na majukwaa ya kidijitali, kuandaa maudhui ya kielimu na kutumia teknolojia katika ufundishaji, ujifunzaji na upimaji.

Mpango huo unalenga kujenga mtandao mpana wa walimu wenye ujuzi wa kidijitali kupitia mfumo wa kushirikishana na kuhamishiana maarifa na ujuzi, hatua inayotarajiwa kuwafaidisha wanafunzi.

Mafunzo hayo pia yanaunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika elimu na kujenga nguvu kazi yenye ujuzi na maarifa yanayokidhi mahitaji ya karne ya 21.

Aidha, mpango huo unaendana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 inayosisitiza umuhimu wa kuwa na wananchi wenye maarifa, ujuzi na uwezo wa kutumia teknolojia katika kuchochea maendeleo ya taifa.

Mafunzo hayo yanaendelea katika Hoteli ya Gold Crest jijini Arusha na yanatarajiwa kuhitimishwa Septemba 4, 2026.

Post a Comment

أحدث أقدم