NMB, IFC Waandika Historia ya Uwekezaji,Hatifungani ya Sh262.5 Bilioni Yaingia LSE


Tanzania imepiga hatua nyingine kimataifa baada ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) kuorodhesha hatifungani yake ya kwanza ya kimataifa kwa Shilingi ya Tanzania katika Soko la Hisa la London (LSE). 

Hatifungani hiyo, yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 100 (Shilingi bilioni 262.5), itaipatia Benki ya NMB ikiwa ni fedha za muda mrefu kwa ajili ya kupanua mikopo kwa biashara ndogo na za kati, huku asilimia 20 - sawa na Shilingi bilioni 52.5 - ikitengwa mahsusi kwa wafanyabiashara wanawake.

Akizungumza baada ya kupiga kengele ya uzinduzi, Mkurugenzi Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema fedha hizo zitaongeza uwezo wa benki kutoa mikopo ya muda mrefu, jambo litakalochochea ukuaji wa sekta binafsi na ajira. Naye Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, alisema hatua hiyo inaonesha imani ya kimataifa kwa uchumi wa Tanzania na inaunga mkono Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Fedha hizi, zinazotolewa kwa Shilingi badala ya fedha za kigeni, zinawawezesha wafanyabiashara kupata mtaji bila hatari ya mabadiliko ya thamani ya fedha. Hii ni mara ya pili NMB kufaidika na soko la London - mwaka 2023 benki ilikusanya zaidi ya Shilingi bilioni 400 kupitia hatifungani ya kijamii. 


Post a Comment

Previous Post Next Post