Lusaka, Julai 8, 2026
AFISA Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Airtel Africa, Sunil Taldar, ametangaza dhamira ya kuunganisha shule 5,000 na mtandao wa intaneti ifikapo mwaka 2027 katika nchi 14 barani Afrika ambapo kampuni hiyo inatoa huduma. Hatua hii inatekelezwa kupitia taasisi yake ya hisani, Airtel Africa Foundation, kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).
Hadi sasa, mradi huo wa ushirikiano wenye thamani ya dola milioni 57 uliozinduliwa mwaka 2021, umefanikiwa kuunganisha shule 3,296 na kutoa fursa ya mtandao kwa zaidi ya wanafunzi milioni 2 na walimu takribani 40,000. Maeneo 64 ya kujifunzia kwa njia za mtaondao yameondolewa malipo (zero-rated), na kuwawezesha watumiaji zaidi ya milioni 11 kupata maudhui ya elimu bila gharama yoyote.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika Shule ya Wasichana ya Mtakatifu Monika (St. Monica) mjini Lusaka, ambayo ni moja ya shule 300 zilizokwishaunganishwa na intaneti nchini Zambia, Afisa Mtendaji Mkuu huyo wa Airtel Africa alieleza kuwa mpango huo una mchango mkubwa katika kuboresha ubora wa elimu kwa kupanua fursa ya kupata rasilimali za kidijitali za kujifunzia kwa watoto wa Afrika, kwa kushirikiana na serikali husika.
Bw. Taldar aliongeza: "Wanafunzi wanapata elimu ya kiwango cha juu kutoka kwenye mtaala ulioandaliwa na UNICEF kwa kushirikiana na Wizara mbalimbali za Elimu, inayopatikana kupitia mtandao wa Airtel. Pia tunawajengea uwezo walimu ili waweze kutumia njia za kidijitali kwa ufanisi kutoa elimu. Lengo letu ni kuendelea kuimarisha upatikanaji wa mtandao wenye tija mashuleni kwa kutoa intaneti ya bure, majukwaa yasiyotozwa gharama za data, na kuwanoa walimu kote barani."
Akitoa shukrani zake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Wasichana ya Mtakatifu Monika (St. Monica), Sr. Matilda Soloko alisema: "Sisi ni miongoni mwa mwa shule za kwanza kabisa kuunganishwa katika awamu ya kwanza na wanafunzi wetu wameweza kusoma kwa kutumia njia za kidijitali kujifunzia na uelewa wao katika masomo umeimarika sana. Tunwashukuru sana Airtel na UNICEF."
Mwakilishi wa UNICEF nchini Zambia, Dkt. Saja Farooq Abdullah alisema: "Ushirikiano wet una Airtel Africa ni kuziba pengo la ujumuishi wa kidijitali. Tunataka kuhakikisha kwamba kila mtoto anaweza kujifunza sehemu yoyote alipo. Kwetu, jambo la kujivunia sana kuona wanafunzi hawa wasichana wanavyoweza kujifunza kwa wakati na kasi yao wenyewe, jinsi wanavyoweza kupitia upya masomo, na jinsi wanavyofanya kazi zao za nyumbani (homework) kwa urahisi."
Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari katika Wizara ya Elimu nchini Zambia, Yvonne Mwemba Chuulu, aliwapongeza UNICEF na Airtel kwa ushirikiano huo akisema: "Sisi kama Wizara ya Elimu hatuwezi kufanya haya peke yetu, na tunashukuru kwa ushirikiano tulio nao na wenzetu wa Airtel Africa na UNICEF. Watoto wetu wana uwezo wa kujifunza kwa mfumo mseto, ambapo tuna mwalimu ambaye pia anatumia vifaa vya kidijitali. Pia tumesikia kutoka kwa wanafunzi kwamba wana uwezo wa kuingia kwenye mifumo ya kidijitali wakiwa nyumbani, jambo ambalo ni zuri kwa sababu wanafunzi wetu wanaendelea kujifunza wakiwa katika mazingira ya majumbani mwao."
Mpango huu wa Kuunganisha Shule unatoa uwanja mpana kwa wanafunzi kujifunza kwa njia za kidijitali katika nchi 13: Chad, Kongo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Gabon, Kenya, Madagascar, Malawi, Niger, Nigeria, Rwanda, Tanzania, Uganda, na Zambia. Kwa kuzipatia shule hizi huduma ya intaneti na kuwapatia walimu mafunzo ya matumizi ya zana za kidijitali, mpango huu unawapa watoto, hasa katika maeneo ya pembezoni mwa miji na ya vijijini, zana na ujuzi wa kidijitali wanaouhitaji ili kufanikiwa.
Taasisi ya Airtel Africa Foundation inaendelea kuboresha maendeleo jumuishi kupitia nguzo nne za kimkakati: Ujumuishi wa Kifedha, Elimu, Uendelevu wa Mazingira, na Ujumuishi wa Kidijitali. Ripoti ya Mwaka ya Airtel Africa Foundation ya 2025/26 inapatikana katika www.airtelafricafoundation.org.


Post a Comment