NA FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Katika kipindi hiki cha kasi ya maendeleo ya teknolojia na mabadiliko makubwa ya mifumo ya mawasiliano duniani, waandishi wa habari hususan wanawake wametakiwa kuongeza juhudi katika kujiendeleza kielimu na kujikita kwenye taaluma za ubobezi ili kuendana na ushindani wa sekta ya habari na kuchangia maendeleo ya jamii.
Wito huo umetolewa mkoani Morogoro wakati wa Mahafali ya 47 ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), ambapo baadhi ya wahitimu wa fani mbalimbali, akiwemo mwanahabari Kelvin Gwabala na Sophia Makame, walizungumza kuhusu umuhimu wa wanahabari kuendelea kujifunza na kuongeza ujuzi wa kitaaluma.
Akizungumza mara baada ya kuhitimu, Kelvin Gwabala amesema maendeleo ya teknolojia yamebadilisha mfumo wa utoaji habari, hivyo wanahabari wanapaswa kujifunza mbinu mpya za uandishi na matumizi ya teknolojia ili kubaki na ushindani katika tasnia hiyo.
Kwa upande wake, Sophia Makame amesisitiza umuhimu wa wanawake waliopo kwenye sekta ya habari kujiamini na kutumia fursa za elimu kujijengea uwezo wa kitaaluma, akieleza kuwa elimu ndiyo msingi wa mafanikio katika kazi za habari.
Profesa Raphael Chibunda ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), amesema chuo hicho kinaendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia pamoja na kuongeza programu mbalimbali zinazolenga kuwaandaa wahitimu wenye uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira la sasa.
Aidha, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Andrew Massawe, amesema SUA imeendelea kupata mafanikio katika sekta za elimu, utafiti na ubunifu, huku akibainisha kuwa chuo hicho kitaendelea kuwekeza katika kukuza taaluma zinazochochea maendeleo ya taifa.



.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
Post a Comment