Mkuu wa wilaya ya Arusha azindua rasmi elimu ya Bima ya Afya kwa wote

Filbert Rweyemamu,Arusha

Mkuu wa wilaya ya Arusha,Joseph Mkude amezindua kampeni ya uhamasishaji wananchi kujiunga na mpango wa serikali wa Bima ya Afya kwa Wote unaolenga kuwapa fursa ya matibabu wananchi bila vikwazo ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizundua mpango huo jana,Desemba 29,2025 kwenye viwanja vya ofisi ya Mkuu wa wilaya amesema kilio cha muda mrefu cha wananchi ambao hawapo kwenye sekta rasmi ya Bima kimepatiwa ufumbuzi na serikali kuweka mpango utakaojumuisha wananchi wote bila kujali hali za vipato vyao.

Amesema mageuzi hayo katika sekta ya afya yanakuja ili kuwawezesha wananchi kuweza kugharamia matibabu yao kwanjia nafuu na kuwataka Watendaji wa Mitaa na Madiwani kuhamasisha wananchi kujiunga kwa wingi kwenye mfuko huo.

“Wananchi mnakumbuka ahadi za Rais wetu,Dk.Samia Suluhu Hassan wakati anaomba ridhaa kuendelea kuongoza nchi yetu,moja ya vipaumbele ni suala la afya na aliahidi kuhakikisha tunakuwa na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ambao elimu kwa umma inatolewa ili wananchi waanze kunufaika kikamilifu,”amesema Mkude

Ameongeza  kwa nyakati tofauti serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya wamefanya juhudi za kuboresha huduma za afya zikiwemo kambi za matibabu mikoa mbalimbali,ujenzi wa Zahanati , Vituo vya Afya,hospitali za wilaya na Rufaa ambazo zimesaidia kupunguza mzigo mkubwa wa huduma za afya.

Hata hivyo,Mkude amesema gharama za matibabu kwa wananchi walio wengi zimekua changamoto na baadhi ya wananchi wamekua wakimpigia simu ili awasaidie gharama wanazotakiwa kulipa baada ya matibabu hospitalini.

“Wananchi wamekua wakitupigia simu viongozi wakiomba tuwasaidie fedha wanazodaiwa hospitalini baada ya matibabu,wakati mwingine nimekua nikizungumza na madakari kiungwana nao wamekua wakichukulia kubinadamu na kuheshimu ofisi zetu,hivyo mpango huu wa Bima ya Afya kwa Wote ni mkombozi  kutokana unafuu wake,”amesema Mkude

Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha,Julius Sekeyani amemwahidi Mkuu wa wilaya kuwahamaisha madiwani kutoa elimu ya mpango huo kwa wananchi wao ili uwe ukombozi wa huduma za matibabu kutokana na gharama za matibabu kuendelea kuongezeka hasa magonjwa yanayotibiwa kwa muda mrefu.

“Huu ni ukombozi kwa wananchi wetu ambao wengi hawapo kwenye utaratibu wa kawaida wa Bima ya Afya,tunatarajia wataupokea kwa furaha na kuchangia kiasi tulichoambiwa cha Sh.150,000 ambazo zitawapa matibabu kulingana na utaratibu uliowekwa na serikali,nina amini wananchi wenye afya njema wanaweza kujenga uchumi wa nchi yetu kikamilifu,”amesema  Sekeyani

Afisa Uanachama wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) mkoa wa Arusha,Miraji Kisile amesema utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ni utekelezaji wa sheria unaowataka wananchi kwenye makundi yao kuchangia mfuko huo kupitia utaratibu maalumu.

“Huu ni mpango wa kisheria ambao unawataka wananchi wote kushiriki ili kupata unafuu wa matibabu,pia sekta binafsi itatakiwa kufuata sheria ya kuwa kwenye mifuko ya afya ili watumishi wake wanufaike na huduma ya matibabu kupitia mpango wa Bima ya Afya kwa Wote,”amesema Kisile

Afisa Uanachama wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF),Miraji Kisile akizungumza wakati wa uzinduzi huo
Mkuu wa wilaya ya Arusha,Joseph Modest Mkude

Mkuu wa wilaya ya Arusha,Joseph Mkude(katikati) akiwa pamoja na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Arusha,Wilfred Soileli(kushoto) na Naibu Meya wa halmashari ya jiji la Arusha,Julius Sekeyani.

 


Post a Comment

أحدث أقدم