Takriban watu 143 wamethibitishwa kufariki dunia, huku wengine kadhaa wakiwa hawajulikani walipo, baada ya boti ya mbao iliyokuwa imebeba mafuta na mamia ya abiria kushika moto na kupinduka katika Mto Kongo, kaskazini-magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Ajali hiyo imetokea siku ya Jumanne karibu na mji wa Mbandaka, mji mkuu wa Mkoa wa Equateur, katika makutano ya Mto Ruki na Mto Kongo, ambao unajulikana kuwa miongoni mwa mito yenye kina kirefu zaidi duniani.
Kwa mujibu wa Mkuu wa ujumbe wa wabunge wa kitaifa kutoka eneo hilo, Josephine-Pacifique Lokumu, boti hiyo ilikuwa imebeba mamia ya watu wakati moto ulipozuka.
“Miili 131 ya kwanza ilipatikana siku ya Jumatano, huku mingine 12 ikiopolewa siku ya Alhamisi na Ijumaa. Miili hiyo ilikuwa imeteketea,” amesema Lokumu.
Lokumu ameongeza kuwa chanzo cha moto huo kilikuwa kitendo cha abiria mmoja mwanamke kuamua kupika ndani ya boti hiyo, jambo lililosababisha mlipuko na moto mkubwa ulioenea haraka.
“Moto ndani ya boti hiyo ulisababishwa na kitendo cha mwanamke mmoja, ambaye alikuwa ni abiria, kuamua kupika ndani ya boti hiyo,” amesema Lokumu, akibainisha kuwa baadhi ya abiria waliokuwa ndani, wakiwemo wanawake na watoto, walilazimika kuruka majini na wengi wao walipoteza maisha kwa kushindwa kuogelea.
Mpaka sasa, bado haijafahamika ni watu wangapi walikuwa kwenye boti hiyo, lakini mashuhuda na vyanzo vya ndani vinasema ilikuwa imebeba idadi kubwa ya abiria, kinyume na uwezo wake.
Ijumaa ya wiki hii, baadhi ya familia kutoka eneo hilo wameripoti kukosekana kwa wapendwa wao waliokuwa safarini kwa kutumia boti hiyo, huku juhudi za kuwatafuta zikiendelea.


إرسال تعليق