Na Estom Sanga- TASAF
Makamu wa
Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd
amesema mchango unaotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF katika
shughuli za maendeleo hususani katika jitihada za kupunguza umaskini wa
wananchi ni za kupongezwa kwani unatekelezwa kwa kuzingatia sera za
serikali za kupambana na umaskini.
Balozi
Seif akizungumza na Ujumbe wa Maafisa Waandamizi wa Benki ya Dunia
waliokuwako kisiwani Zanzibar pamoja na mambo mengine kuona namna
Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na serikali
kupitia TASAFwanavyonufaika , amesisitiza kuwa maisha ya Walengwa
wanaonufaika na huduma za Mpango huo yameboreshwa na kuwawekea msingi
imara wa kujitegemea.
Amesema
TASAF ni kielelezo stahiki cha namna serikali inavyowajali wananchi
hususani wanaoishi katika umaskini uliokithiri kwa kuwawekea mazingira
ya kufanya kazi za uzalishaji mali ili kujiongezea kipato huku pia mkazo
ukiwekwa katika sekta za Elimu, Afya na Lishe kwa kaya za Walengwa.
Makamu
huyo wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pia amesema
mchango wa kaya za Walengwa katika ukuaji wa uchumi umeanza kuonekana
kutokana na shughuli wanazozifanya hasa katika nyanja za kilimo cha
Mpunga, bustani ,ususi na ufugaji wa kuku wa kienyeji na mbuzi kwa
kutumia ruzuku kutoka TASAF masuala ambayo amesema yanawaongezea kipato .
Akitoa
mfano,Balozi Seif amesema miradi mingi iliyoanzishwa na Wananchi katika
maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba kupitia Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} na kupata msukumo wa Benki ya Dunia
imeleta ukombozi kwa Wananchi walio wengi kisiwani humo.Mapema
Mkurugenzi Mtendaji TASAF} Ladislaus Mwamanga amesema kazi kubwa
inayofanywa na Wananchi wa Zanzibar kwenye miradi ya Maendeleo kupitia
programu zinazosimamiwa na Mfuko huo imeleta mafanikio makubwa.
Mwamanga
amesema Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mfuko huo
itaendelea kuongeza nguvu mara dufu katika kuona kundi kubwa la Wananchi
walio na kipato duni hasa Vijijini wanaongezewa nguvu za uwezeshaji ili
kuondokana na mazingira magumu yanayowakabili.
Akitoa
salamu kwa niaba ya Ujumbe wa Viongozi hao wa Benki ya Dunia Mkurugenzi
na Mkuu wa Mtandao wa Masuala ya Kijamii na Ajira wa Benki ya Dunia
Bwana Michal Rutkowski alisema Taasisi hiyo ya Kimataifa ya Fedha haina
sababu ya kusua sua katika kuongeza nguvu kwenye miradi ya TASAF
inayoendelea vizuri katika utekelezaji wake.
Bwana
Michal alisema Uongozi wa juu wa Benki ya Dunia {World Bank}
umefurahishwa na jitihada kubwa zinazochukuliwa na Wananchi walio wengi
Visiwani Zanzibar katika utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ya Jamii
inayosimamiwa na TASAF .
Akimkaribisha
mgeni rasmi katika tafrija hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed alisema ushirikiano wa
karibu uliopo kati ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Dunia umesaidia kupunguza
umaskini kwa baadhi ya Kaya Nchini Tanzania.
Waziri
Aboud alisema ushirikiano huo unaendelea kuwa kigezo tosha kinachotoa
majibu ya uwepo wa utulivu wa kimaisha kwa Baadhi ya Familia za Kaya
hizo jambo ambalo limeleta faraja zaidi kwa watoto wao katika kushiriki
vyema masomo yao.
Hii ni
mara ya pili kwa Mkurugenzi ambae pia ni Mkuu wa Mtandao wa Masuala ya
Kijamii na Ajira wa Benki ya Dunia Bwana Michal Rutkowski na Maafisa
wake kutembelea miradi ya maendeleo ya Kijamii inayosimamiwa na Mfuko wa
TASAF Nchini Tanzania.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd akizungumza na Maafisa wa
Benki ya Dunia,TASAF na serikali ya Mapinduzi Zanzibar juu ya mchango
muhimu wa TASAF katika kukabiliana na umaskini nchini.
Waziri wa
Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud
Mohamed akishukuru ushirikiano uliopo kati ya SMT,SMZ na Benki ya Dunia
uliosaidia kuzikomboa Kaya Maskini Nchini.
Mkurugenzi
Mtendaji wa TASAF ,Ladislaus Mwamanga akipongeza usimamizi mzuri wa
serikali katika kufanikisha shughuli za taasisi hiyo kwenye hafla
iliyohudhuriwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Maafisa wa Benki
ya Dunia.
Mkurugenzi
na Mkuu wa Mtandao wa Masuala ya Kijamii na Ajira wa Benki ya Dunia
Bwana Michal Rutkowski akizungumza kwenye hafla iliyohudhuriwa na Makamu
wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.
Balozi
Seif Ali Idd (walioketi katikati )akiwa katika picha ya pamoja na baadhi
ya watendaji wa TASAF na Benki ya Dunia baada ya kutoa hotuba kufuatia
ziara ya maafisa hao ksiwani Zanzibar kuona shughuli za Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini.
No comments:
Post a Comment