Pages

June 5, 2018

KAMPUNI YA EASY TRAVEL AND TOURS LTD YAKUSANYA TAKA ZA PLASTIKI KUTUNZA MAZINGIRA

Wapagazi wa kampuni ya Easy Travel and Tours Ltd wanaobeba mizigo ya watalii kwenye Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro(Kinapa)wakikusanya mifuko na chupa za plastiki kwaajili ya kusafisha mazingira eneo la Kwamrombo jijini Arusha

Mkurugenzi wa Jiji la Arusha,Athumani Kihamia(kulia)akishiriki na wapagazi wa kampuni ya Easy Travel and Tours Ltd.

Wapagazi wa kampuni ya Easy Travel and Tours Ltd wakimwaga taka za mifuko na chupa za plastiki baada ya kusafisha mazingira .Picha na Filbert Rweyemamu
Filbert Rweyemamu,Arusha
Wapagazi zaidi ya 100 wa kampuni ya utalii ya Easy Travel & Tourism Ltd ya jijini hapa wamefanya usafi wa mazingira kwa kukusanya mifuko na chupa za plastiki ikiwa ni sehemu za maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yanayofanyika Juni 5 kila mwaka.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Jiji la Arusha,Athumani Kihamia alisema eneo la Kwamrombo Kata ya Muriet ambalo kampuni hiyo ilijitolea kufanya usafi lina idadi kubwa ya watu na kuwa na mkusanyiko wa taka ngumu hasa mifuko na chupa za plastiki.

"Eneo hili lina idadi kubwa ya watu na uzalishaji wa taka ni mkubwa ninaishukuru kampuni hii kwa kushirikiana na halmashauri yetu kuona umuhimu wa kuweka mazingira yetu yakiwa safi,"alisema Kihamia

Mkurugenzi wa kampuni hiyo,Musaddiq Gullamhussein alisema tatizo la taka ngumu hasa  mifuko na chupa za plastiki limekua likiongezeka na wataalamu wa mazingira wanadai ifikapo mwaka 2050 idadi ya chupa za plastiki baharini zitakua nyingi kuliko samaki.

Alisema kuwashirikisha wafanyakazi wake ambao muda mwingi wanakua Mlima Kilimanjaro kuwaongoza watalii ni sehemu ya kuwapa elimu ili wawe mabalozi ya kutunza mazingira ya mlima huo ambao ni sehemu chanzo kikuu cha mapato nchini.

Aliongeza kuwa baada ya kukusanya taka hizo watazipeleka kwenye moja ya viwanda kwaajili ya kuzichakata na kupata bidhaa zitakazotumika kuvutia watalii kwenye maeneo mbalimbali watakayotembelea.

Meneja Msimamizi wa kampuni ya Easy Travel,James Makoye  alisema kuweka mazingira safi ni njia ya sahihi ya kujiepusha na magonjwa yanayoambukizwa na kulinda mazalia ya samaki kwaajili ya kupata lishe bora na kuhakikisha usalama wa vizazi vijavyo.

Alisema wataendelea kukusanya chupa na mifuko ya plastiki ili kuwa na hatma salama na kujenga mwamko wa jamii inayopenda kutunza mazingira yanayowazunguka na vyanzo vya maji.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...