Waziri
wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango, amewataka Watumishi wa
Wizara hiyo kuongeza ukusanyaji wa mapato na kusimamia nidhamu ya
matumizi ya Fedha za Umma ili kuijengea Serikali uwezo wa kuwahudumia
wananchi na kuifanya nchi iwe na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Dkt.
Mpango ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Baraza
la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliowakutanisha wajumbe zaidi ya 190
kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Amesema
kuwa Wizara ya Fedha na Mipango inajukumu la kuhakikisha inatekeleza
usemi wa “Wizara ya Fedha na Mipango ndiyo Moyo wa Serikali” kwa
kutumia Baraza la Wafanyakazi katika kushauriana na kuchangia mawazo
yatakayosaidia katika kutekeleza majukumu ya Wizara kama yalivyopangwa
na kusukuma kasi ya maendeleo ya uchumi wa Taifa.
“Watumishi
wote wa Wizara mnaowajibu wa kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kutumia
utaalamu mlionao na kutekeleza majukumu kwa kuzingatia nidhamu,
maadili, sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa Umma ili kuongeza
tija” alieleza Dkt. Mpango.
Akizungumzia
suala la maadili Dkt. Mpango amesema kila mtumishi wa Wizara hiyo
anapaswa kutunza siri na nyaraka za Serikali kwa kuzingatia kuwa taarifa
zinazopatikana kutokana na majukumu haziachwi ovyo na hatimaye
kuangukia mikononi mwa watu wasiohusika.
“Watumishi
wote mnapaswa kutotumia nyaraka au taarifa za ofisi za umma kwa masuala
ya kisiasa kwani huo ni uvunjaji wa taratibu za utumishi wa Umma”,
alisisitiza Waziri Mpango.
Amesema
kila mtumishi anao wajibu wa kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana
kila mmoja katika nafasi yake ili hatimaye Wizara ya Fedha iweze kufikia
malengo iliyojiwekea kwa mwaka ujao wa fedha 2018/2019 na kuchangia
ipasavyo katika utekezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.
Dkt.
Mpango, amewaagiza watendaji wa Wizara hiyo kuhakikisha kuwa vikao vya
Baraza la Wafanyakazi vinafanyika kama vilivyopangwa kwa kuwa ni
sehemu nzuri ya wafanyakazi kueleza changamoto zao na kutoa mawazo namna
ya kuboresha utendaji kazi wa Wizara.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Doto James, amemhakikishia
Waziri Mpango kuwa watatekeleza maelekezo yote aliyoyatoa kwa ukamilifu
ili kuongeza tija.
Akitoa
maoni yake, Mhakiki mali za Serikali kutoka Mkoa wa Dar es Salaam Bw.
Ismail Ugaga ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Baraza hilo amesema kuwa
umefika wakati ambao Serikali inapaswa kuchukua hatua kali kwa wale wote
wanaotoa siri za Serikali ili kukomesha tatizo hilo miongoni mwa
watumishi wa umma.
Lengo
kuu la Baraza la Wafanyakazi sehemu za kazi ni kuongeza tija, ufanisi
na ushirikishwaji wa wafanyakazi katika uongozi wa pamoja mahali pa kazi
kama linavyoagiza Agizo la Rais Na. 1 la mwaka 1970 likisomwa pamoja na
miongozo mingine inayoyekeleza agizo hilo.
Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (katikati)
akiimba wimbo wa Mshikamano Daima pamoja na meza kuu kabla ya kufungua
rasmi Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Mipango
Jijini Dodoma.
Sehemu
ya wajumbe zaidi ya 190 wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara
ya Fedha na Mipango wakiimba wimbo wa Mshikamano Daima wakati wa Mkutano
wa Baraza hilo Jijini Dodoma.
Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) katikati walio
kaa, wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Wizara hiyo
walioshiriki Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na
Mipango Jijini Dodoma.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kulia) akifafanua
jambo wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na
Mipango Jijini Dodoma, kushoto ni Katibu wa Baraza hilo Bw. Cyprian
Kuyava.
Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano Serikali wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw.
Benny Mwaipaja (kushoto) na Mhasibu Mkuu wa Fungu 21 wa Wizara hiyo Bw.
Sayi Nsungi, wakifuatilia majadiliano wakati wa Mkutano wa Baraza la
Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
Wajumbe Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiendelea na Mkutano Jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango)
No comments:
Post a Comment