Serikali
imeeleza kuwa Uchukuaji wa baadhi ya vyanzo vya mapato katika
halmashauri ulifanyika kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti iliyoridhiwa na
Bunge ya mwaka 2015 kifungu namba 58 ikiwa na lengo la kuongeza ufanisi
wa ukusanyaji na matumizi ya mapato hayo.
Hayo
yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge
wa Viti Maalum Mhe. Suzana Mgonukulima, aliyependekeza itungwe sheria
ya kuibana serikali ikiwa haitarejesha fedha zilizotokana na vyanzo vya
mapato vilivyopo kwenye Miji, Halmashauri, Manispaa na Majiji
zitakazokusanywa na kuwekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
Akijibu
swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 44 cha
Sheria ya Bajeti, mgao wa fedha kutoka katika Mfuko Mkuu wa Serikali
utazingatia bajeti iliyoidhinishwa, upatikanaji na mtiririko wa fedha,
utekelezaji mpango wa ununuzi na mpango wa kuajiri hivyo hakuna Fungu
litakaloruhusiwa kufanya matumizi ya aina yoyote mpaka kuwe na fedha za
kulipa matumizi husika.
“Usimamizi
wa Mapato hayo kwa mujibu ya Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2015 Kifungu
namba 58 unazingatia mapato kuingizwa kwenye Sheria ya Kuidhinisha
Matumizi ya Fedha za Serikali, aliyepewa mamlaka ya kukusanya mapato ya
Serikali atawajibika katika ukusanyaji wenye ufanisi, utunzaji wa
hesabu, utoaji wa taarifa na kuzuia ufujaji wa mapato”, alisema Dkt.
Kijaji.
Alisema
Usimamizi wa mapato na matumizi umebainishwa vizuri na hivyo hakuna
haja ya kutunga sheria nyingine ya kuibana Serikali ikiwa haitapeleka
fedha kwenye, Miji, Halmashauri, Manispaa na Majiji.
Aidha
akijibu swali la nyongezai la Mhe. Mgonukulima kuhusu kutokuwa na usawa
katika utoaji wa fedha za maendeleo katika Wilaya, Dkt. Kijaji alisema
kuwa tarehe 5 Mei, 2018 Serikali ilizindua Mkakati wa kuziwezesha
Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza miradi yenye kuchochea
upatikanaji wa Mapato ili ziweze kujitegemea hivyo ni vema Halmashauri
zikabuni miradi ya maendeleo itakayoongeza mapato.
Akieleza
kuhusu utaratibu wa malipo ya Kodi ya Majengo kutoka katika Halmashauri
nchini Naibu Waziri Dkt. Kijaji, alisema kuwa Majengo yasiyofanyiwa
tathimini yanatakiwa kutozwa kiwango sawa cha Sh. 10,000 na majengo ya
juu (ghorofa) yanatakiwa kutozwa kiwango sawa cha Sh. 50,000.
Alisema
majengo yaliyofanyiwa tahimini ndiyo yanayoweza kulipiwa kodi zaidi ya
kiasi hicho, hivyo wakurugenzi wa Halmashauri wanapaswa kuzingatia
utaratibu huo uliowekwa katika ukusanyaji wa kodi hiyo, alieleza Dkt.
Kijaji.
Imetolewa na;
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
No comments:
Post a Comment