Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliishukuru na
kuipongeza Taasisi ya Kiraia ya Zanzibar Relief and Development
Foundation { ZANRDEF} kwa uamuzi wake wa kusaidia huduma za msingi
ya Kijamii za Maji safi katika azma yake ya kuona maisha ya Wananchi
yanaendelea kustawika.
Alisema uamuzi huo wa ZANRDEF utasaidia kuwapunguzia machungu Wananchi
walio wengi kupata huduma hizo sambamba na kuiunga Mkono Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika mipango yake ya kuwasogezea karibu
mahitaji ya msingi Wananchi wake.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda alitoa
shukrani hizo wakati akizungumza na Viongozi wa Kamati ya Maendeleo ya
Jimbo la Mahonda mara baada ya kukikagua Kisima cha Maji safi na salama
kinachochimbwa katika Skuli ya Mahonda kwa msaada wa Taasisi ya
ZANRDEF.
Alisema zipo changamoto nyingi za upatikanaji wa huduma za Maji safi na
salama kwa Wananchi walio wengi Visiwani Zanzibar licha ya juhudi kubwa
inayoendelea kuchukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na washirika wa
Maendeleo kuitafutia ufumbuzi changamoto hiyo.
Balozi Seif aliutolea mfano Mkoa wa Kaskazini Unguja ukiwa ni miongni
mwa Mikoa inayokumbwa na changamoto hiyo hasa kwa baadhi ya Vijiji,
Majengo ya huduma za Kijamii kama Hospitali na Maskuli lakini kukosekana
kwa huduma hiyo kwa baadhi ya maeneo wakati mwengine husababishwa kwa
makusudi na baadhi ya Watu kwa sababu za itikadi za Kisiasa.
Aliwanasihi Wananchi kuendelea kuheshimu Miundombinu mbali mbali
inayowekwa na Serikali sambamba na baadhi ya Watu kuacha tabia ya
kuiharibu kwa makusudi Miuondombinu hiyo kwani inaweza kulisababishia
hasara kubwa Taifa.
Mapema Katibu wa Taasisi ya Kiraia ya Zanzibar Relief and Development
Foundation Bwana Ali Mohamed Haji alisema Taasisi hiyo inayoshirikiana
na Ubalozi wa Uturuki Nchini Tanzania imeazimia Kuchimba Visima 40
Zanzibar ili kusaidia kupatikana kwa huduma ya Maji safi na salama.
Bwana Ali alisema Visima Vitano vya mwanzo vinatarajiwa kuchimbwa ndani
ya Jimbo la Mahonda ambapo kile cha Skuli ya Mahonda kikiwa cha kwanza
katika idadi hiyo ya awamu ya kwanza.
Alisema Awamu ya Pili ya uchimbaji Visima hivyo inatarajiwa kuanza ndani
ya Mwezi wa Mei kwa Visima 35 vitakavyotumia Nishati ya Umeme wa Jua
ambavyo kati ya hivyo 15 vitachimbwa ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B”
inayoonekana kukumbwa zaidi na changamoto ya huduma ya Maji safi na
salama.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Ndugu Rajab Ali Rajab alisema
huduma za maji safi na salama ndani ya Wilaya hiyo zimekuwa na upungufu
unaoleta athari kwa Jamii hasa katika Vituo vya Afya na Maskuli.
Nd. Raj alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni
Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif kwamba Wilaya ya Kaskazini
“B” ina Vituo 14 vya Afya na Skuli 31 ambazo asilimia kubwa ya Majengo
yake yanakabilia na changamoto za huduma za maji safi na salama.
Alisema hali hiyo wakati mwengine inaleta na kusababisha hatari ya
kuchafuka kwa mazingira na kuwapa kazi nzito zaidi akina Mama Wajawazito
wanaofika katika Vituo vya Afya kwa ajili ya kujifungua.
Uchimbaji wa Kisima cha maji safi na salama ndani ya Skuli ya Mahonda
unatarajiwa kukamilika muda mfupi kutokana na ubora wa mashine
zinazotumiwa na Taasisi ya ZANRDEF ambapo utasaidia kuwaondoshea shida
Wanafunzi wake pamoja na Wananchi wa Vijiji vinavyoizunguuka Skuli hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifika Skuli
ya Mahonda kukagua uchimbaji Kisima cha Maji safi na salama
kitakachowaondoshea usumbufu Wanafunzi na Walimu wa Skuli hiyo.
Balozi Seif pamoja na Uongozi wa Wilaya ya Kaskazini B na Kamati ya
Maendeleo ya Jimbo la Mahonda wakishuhudia harakati za Uchimbwaji wa
Kisima cha Maji safi na Salama katika Skuli ya Mahonda Msingi na
Sekondari chini ya usimamizi wa Mhandisi wa Taasisi hiyo Bwana Doto
Saleh wa kwanza Kulia aliyevaa Kofia ya Manjano.
Balozi
Seif Kati Kati akipongeza na Kuishukuru Taasisi ya Kiraia kwa uamuzi
wake wa kusaidia huduma za Maji Safi na Salama Ndani ya Skuli ya Msingi
na Sekondari ya Mahonda. Kushoto
ya Balozi Seif ni Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini B Nd. Rajab Ali Rajab na
Kulia yake ni Katibu wa ZANRDEF Bwana Ali Mohamed Haji.
Harakti za uchimbwaji wa Kisima cha Maji safi na Salama katika Skuli ya
Mahonda zikiendelea licha ya mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha muda mrefu.
Mkuu
wa Wilaya ya Kaskazini “B” Nd. Rajab Ali Rajab akitoa shukrani kwa
Uongozi wa Jimbo la Mahonda na Taasisi ya Kiraia ya ZANRDEF kwa jitihada
za kusogeza huduma za Maji safi katika Skuli ya Mahonda Msingi na
Sekondari. Picha na – OMPR – ZNZ.
No comments:
Post a Comment