Pages

December 18, 2017

TMRC YATOA MSAADA KWA WATOTO YATIMA KIWALANI

Kampuni ya Tanzania Mortgage Refinance Company Limited (TMRC), imetoa zawadi ya Sikukuu ya Krismas zenye thamani ya Shilingi Milioni Mbili (Shilingi 2,000,000) kwa Kituo cha Watoto yatima cha Kiwalani (Kiwalani Orphanage Centre) kilichopo jijini Dar es Salaam.
Zawadi hizo zimekabidhiwa leo na Afisa Mtendaji Mkuu wa TMRC, Bw. Oscar P. Mgaya kwa Mkurugenzi wa Kituo hicho, Mchungaji   Elias Mwakalukwa -, katika ghafla iliyofanyika kwenye Kituo hicho kilichopo jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa zawadi zilizotolewa kwa kituo hicho cha watoto yatima ni pamoja na mchele, mafuta ya kupikia, unga wa sembe, maharage, sabuni za kufulia na kuogea, sukari ,  chumvi,  dawa za meno, majani, kalamu na madaftari
“Kwa upendo wetu wa dhati kabisa tumeona umuhimu wa kushiriki pamoja na watoto yatima, ambao wapo katika mazingira magumu, katika kusherehekea Sikukuu ya Krimas mwaka 2017,” alisema Bw. Mgaya.
Bw. Mgaya, alisema kuwa taasisi yake imeamua kujumuika na watoto hawa yatima katika kuelekea kusherehekea Sikukuu ya Krismasi kwa kutoa zawadi mbalimbali za vyakula kama njia ya kuwafanya wajisikie furaha.
Hata hivyo, Mtendaji Mkuu huyo, amezitaka taasisi nyingine na watu binafsi kujitoa kwa dhati kuwasaidia watoto  walioko maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo hicho, Mchungaji   Elias Mwakalukwa, ameishukuru TMRC, kwa msaada huo na ameziomba taasisi nyingine kuiga mfano wao.
“Tunaishukuru sana TMRC, ninyi mmeonyesha mfano na hakika mmeonyesha upendo wa dhati kwa watoto hawa. Niziombe taasisi nyingine kuchukua mfano huu uliofanywa na taasisi yenu,” Mchungaji   Elias Mwakalukwa alisema.
Aliongeza kuwa uhitaji wa misaada kwa kituo chake ni mkubwa, lakini taasisi yao inapata faraja kupata wadau wanao ona umuhimu wa kusaidia watoto hao yatima.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...