Benny
Mwaipaja, Dar es Salaam
BALOZI
wa China hapa nchini, Wang Ke, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa
Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango na kuahidi kuwa nchi yake iko tayari
kushawishi taasisi za fedha ikiwemo Benki ya EXIM ya nchini humo kushiriki
ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa baada ya kufanyika kwa
upembuzi yakinifu wa mradi huo.
Alisema
kuwa kutokana na ukubwa wa mradi huo, unaokadiriwa utagharimu Dola za Marekani
bilioni 7.6 hadi kukamilika kwake, utahitaji kufanyiwa upembuzi yakinifu ili
kukidhi masharti ya kupata mkopo kupitia Benki ya Exim na taasisi nyingine
zitakazotaka kujenga mradi huo muhimu.
“Mradi
huu ni muhimu na wa kihistoria kwa nchi hizi mbili, China ingependa kuona mradi
huo unaboreshwa ili uweze kutoa huduma ya kusafirisha mizigo na abiria na
kwamba kuimarika kwake kutaokoa miundombinu ya barabara kwa kuwa shehena kubwa
ya mizigo itasafirishwa kupitia reli hiyo.
Aidha,
Balozi Ke alisema kuwa nchi yake inasubiri pia kukamilika kwa taratibu za ndani
kati yake na Tanzania ili mradi wa reli ya TAZARA uanze ili kuboresha usafiri na usafirishaji wa
mizigo na abiria kati ya Tanzania na Zambia pamoja na nchi za maziwa makuu.
Balozi
Ke alitumia fursa hiyo kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya
Tano kwa kukusanya kodi, kusimamia matumizi adili ya fedha za umma, kupunguza matumizi
yasiyo ya lazima na kupambana na rushwa.
Akizungumza
mara baada ya mazungumzo na mgeni wake, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip
Mpango alisema kuwa Serikali imeridhia uamuzi wa China wa kufanya upembuzi yakinifu
wa mradi huo wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa (SGR) ili China kupitia
taasisi zake iweze kujenga sehemu ya mradi huo.
“Tayari
mradi umeanza kujengwa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, kwahiyo kujitokeza kwa
China kutaka kufadhili ujenzi wa mradi huo kutasaidia kukamilisha mradi huo
muhimu kwa haraka na kwa wakati” Alisema Dkt. Mpango.
Alisema
pia kuwa China imeonesha nia ya kusaidia kuujenga na kuupanga mji wa Dodoma
kutokana na nchi hiyo kuwa na uzoefu wa kupanga miji ambapo nchi hiyo imeonesha
nia ya kujenga miundombinu ya elimu, barabara,
uwanja wa ndege wa kimataifa-Msalato, kujenga mfumo wa maji safi na maji taka
pamoja na majengo ya kisasa.
Kuhusu
biashara, Dkt. Mpango alisema wamekubaliana kuwa China itaisaidia Tanzania
kukuza kiwango cha biashara ambapo takwimu zilizoko zinaonesha kuwa urari wa
biashara kati ya nchi hizo unaonesha kuwa Tanzania imekuwa ikinunua bidhaa
nyingi kutoka nchini humo kuliko inavyo uza bidhaa na huduma zake.
“Mwaka
2016 Tanzania iliuza China bidhaa na huduma zenye thamani ya Dola za marekani
milioni 460 wakati China iliuza hapa nchini bidhaa zenye thamani ya Dola za
Marekani bilioni 1.2, kiwango ambacho ni kikubwa karibu mara 5 ya kile
tulichowauzia” Alisema Dkt. Mpango.
Ili
kuvutia Sekta ya utalii, Tanzania imeiomba China kuanzisha safari ya ndege wa
moja kwa moja kutoka China hadi Tanzania ili kuvutia watalii wengi kutoka
nchini humo na kwamba utaratibu utafanyika ili Mamlaka ya usafiri wa anga iweze
iratibu na kusaini makubaliano ya ushirikiano na hivyo kufanikisha jambo hilo.
“China
imeandaa maonesho makubwa ya uwekezaji na biashara ya bidhaa na huduma
mbalimbali mwezi Novemba, 2018, hivyo wafanyabiashara wa Tanzania pamoja
na Bodi ya Utalii nchini wahakikishe wanashiriki
kikamilifu kwenye maonesho hayo ili kutumia nafasi hiyo kujitangaza” Alisistiza
Dkt. Mpango.
Aidha,
Dkt. Mpango alieleza kuwa Balozi Wang Ke, amesema kuwa Nchi yake itashiriki
katika ujenzi wa miradi ya bandari ili kukuza masuala ya usafiri kwa kuboresha
bandari za Tanga, Bagamoyo, Kigoma, Bagamoyo, Dar es Salaam, Mtwara na katika
Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika.
Waziri
huyo wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango alitoa wito kwa wawekezaji kutoka
China na nchi nyingine kuja kuwekeza nchini katika kipindi hiki ambacho
Tanzania inaipeleka nchi katika uchumi wa viwanda.
Miradi
mikubwa ambayo China imewekeza na kufadhili hadi sasa hapa nchini ni Reli ya
TAZARA, Kiwanda cha Urafiki, ujenzi wa barabara, majengo, ujenzi wa bomba la
gesi kutoka Mtwara hadi dar es Salaam, Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa
Mwalimu Nyerere Jijini Dare Salaam, Ujenzi wa Mabweni ya wanafunzi wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam na miradi mingine kadha wa kadha.

إرسال تعليق