Wakati Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Nairobi, familia yake imefanya kikao cha siri na uongozi ya Bunge kujadili matibabu ya mbunge huyo.
Kikao
hicho kimefanyika leo Jumatatu jijini Dar es Salaam na imeelezwa
kimehudhuriwa na Spika Job Ndugai, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, Katibu
wa Bunge, Thomas Kashilila, Mbunge wa Vunjo, James Mbatia, Mbunge wa
Hanang’, Dk Mary Nagu na ndugu watatu wa Lissu, wanaume wawili na
mwanamke mmoja.
Baada ya kupata taarifa za uwepo wa kikao hicho Mwananchi
iliweka kambi nje ya Ofisi Ndogo za Bunge tangu saa 3:55 asubuhi na
kushuhudia shughuli za kawaida zikiendelea huku kukiwa na watu wachache
wanaoingia na kutoka ndani ya ofisi hizo.
Ilipofika saa
7:40 mchana, alitoka Mbatia akielekea kwenye gari lake baada ya
kumaliza kikao hicho. Mwandishi alimfuata kujua kilichojiri ndani ya
kikao hicho, Mbatia alikiri kuwepo kwa kikao hicho lakini hakutaka
kuzungumza lolote na kuelekeza aulizwe Spika Ndugai.
“Ni
kweli tulikuwa kwenye kikao na familia ya Lissu, lakini siwezi kusema
tumezungumzia nini. Kwa taarifa zaidi nendeni kwa Spika au Katibu wa
Bunge, walikuwepo pia ndugu zake watatu, wafuateni wanaweza kuwaeleza,”
alisema Mbatia.
Msemaji wa familia ya Lissu, Alute
Mughwai alipotafutwa alisema kikao hicho kimefanyika kati ya familia na
uongozi wa Bunge kuhusu mambo yanayomhusu Lissu, hata hivyo alisema
hakijakamilika kwa sababu ya kukosekana kwa upande wa Chadema.
Mughwai
alisema kikao hicho kimeahirishwa mpaka wakati mwingine pande zote
zitakapotimia ili kulijadili suala hilo kwa ukamilifu wake. Alisema
Chadema kupitia kwa mwenyekiti wake Freeman Mbowe walipewa mwaliko
lakini hawakuweza kufika.
“Siwezi kukwambia
tumezungumzia nini, moja ya masharti tuliyopeana ni kutokusema hadharani
mambo tuliyoyajadili lakini yanamuhusu Lissu. Wote ‘interest’ yetu ni
kuona Lissu anapona na kuendelea na majukumu yake kama kawaida,” alisema
Mughwai.
Hata hivyo, jitihada za kumtafuta Spika wa
Bunge pamoja na Katibu wa Bunge zilishindikana baada ya simu zao kuita
bila kupokelewa.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano,
Uenenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alipoulizwa kuhusu kikao
hicho amesema taarifa kuhusu kikao hicho zilipelekwa Ofisi ya Kiongozi
wa Kambi ya Upinzani Bungeni na siyo kwenye chama.
chanzo :Mwananchi
chanzo :Mwananchi

Post a Comment