Pages

September 26, 2017

KAMATI YS MIUNDOMBINU YAKAGUA MINARA YA SIMU

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigallla King (aliyesimama) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kizengi (hawapo pichani) kilichopo kata ya Kizengi wilaya ya Uyui mkoani Tabora baada ya kukagua ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini wakati wa ziara ya Kamati hiyo. 
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Eng. Peter Ulanga(aliyesimama mbele) akifafanua jambo mbele ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini kwenye kijiji cha Mayamaya kilichopo Kata ya Zanka wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.
Meneja wa Kampuni ya Simu ya TTCL Mkoa wa Tabora Bwana James Mlaguzi (wa kwanza kulia) akitoa taarifa kwa wajumbe wa Kamati hiyo wakati wa ziara yao ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano viijini kwenye kijiji cha Kizengi kilichopo kata ya Kizengi wilaya ya Uyui mkoani Tabora.
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Mussa Ntimizi akisalimiana na wananchi wa kijiji cha Kizengi kilichopo kata ya Kizengi wilaya ya Uyui mkoani Tabora wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini.

…………………
Kamati ya Miundombinu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania inaendelea na ziara ya kukagua ujenzi wa minara ya simu, ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini na kwenye maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata na kutumia huduma za mawasiliano kwenye maeneo mbali mbali nchini. Kamti hiyo imeendelea na ziara yake kwenye mikoa ya Dodoma na Tabora ili kujiridhisha na utendaji kazi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) wa kufikisha mawasiliano kwa wananchi.

Katika ziara hiyo, Mtendaji Mkuu wa UCSAF Eng. Peter Ulanga amesema kuwa Mfuko umetoa ruzuku kwa Kampuni ya simu ya TIGO kujenga mnara ili kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi. Mfuko umetumia zaidi ya dola za marekani elfu arobaini na moja na mia tano (41,500) ambapo ni sawa na zaidi ya shilingi milioni 85 kuipatia kampuni ya TIGO kujenga mnara ambao sasa unahudumia zaidi wa wakazi 4,000 wa kijiji cha Mayamaya na vijiji vingine vya kata ya Zanka wilaya ya Bahi mkoani Dodoma ambapo walikuwa hawana huduma za mawasiliano na sasa wananufaika na uwepo wa huu mnara na wanapata huduma za mawasiliano. Mnara huu ulikamilika mwezi Machi mwaka jana na kuanza kutoa huduma ya mawasiiano kwa wananchi.
Naye mwakilishi wa kampuni ya simu ya TIGO mkoa wa Dodoma mhandisi Hassan Said Gimbo wa kampuni hiyo amewaeleza wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu waliofanya ziara ya kukagua ujenzi wa minara, ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano kuwa kampuni yao imekamilisha ujenzi wa mnara na sasa unatoa mawasiliano kwa wananchi. Pia ameongeza kuwa kampuni ya TIGO inafuatilia mara kwa mara kwenye eneo hilo na kuhakikisha kuwa mawasiliano yanapatikana. “Tunajitahidi kwa kiasi kikubwa kukarabati na kuhakikisha kuwa pale mawasiliano yanapopotea au kuwa hafifu tunafanya haraka kuyarudisha”, amesema mhandisi Gimbo.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu akizungumza kwa niaba ya Kamati hiyo Mhe. Mussa Ntimizi ameipongeza Serikali kwa kutoa ruzuku kwa kampuni za simu za mkononi kupitia UCSAF ili kufikisha huduma za mawasiliano vijijini. Mhe. Ntimizi ameongeza kuwa kwa sisi wawakilishi wa wananchi tunaotoka vijijini tunaelewa mahitaji na kiu ya wananchi ya kupata mawasiliano kwenye makazi yao na umuhimu wa huduma nyingine za mawasiliano. “Ukiangalia eneo kama hili halivutii kibiashara hivyo sio rahisi kwa kampuni za simu kama hii ya TIGO kuja kuweka mnara wa simu hapa” amesema Mhe. Ntimizi.

Tumepata taarifa kuwa zaidi ya vijiji vitano vyenye wakazi zaidi ya watu 4,000 wanapata mawasiliano kupitia mnara huu wa TIGO. “Kwa wananchi zaidi ya 4,000 kukosa mawasiliano sio kitu kidogo na Mfuko huu unafanya kazi kubwa ya kufikisha mawasiliano vijijini na Serikali inatumia gharama kubwa kujenga minara ya simu za mkononi na kutoa huduma za mawasiliano vijjijini, hivyo wahakikishe kuwa huduma za mawasiliano zinapatikana muda wote”, amesema Mhe. Ntimizi.

Pia, ametoa rai kwa kampuni za simu nchini kuboresha na kukarabati miundombinu ya mawasiliano na minara yao ili wananchi waendelee kupata mawasiliano muda wote kwa kuwa serikali inatoa fedha nyingi kwa maana ya ruzuku na kuwapatia kampuni za simu ili ziweze kufikisha huduma za mawasiliano kwa wanachi muda wote.
Amesema kuwa huduma hizi zina gharama kubwa sana na wananchi hawajui gharama kubwa ambayo Serikali imeingia kutengeneza mnara huu ambazo ni kodi zao na hawaoni thamani ya Serikali kuwaletea huduma hii. Wananchi muendelee kulinda miundombinu ya mawasiliano na kusiwepo na wizi wa mafuta ya dizeli, mitambo na vitu vingine kwa kuwa Serikali inatumia gharama kubwa kufikisha huduma za mawasiliano vijijini ambapo ujenzi wa mnara mmoja unagharimu zaidi ya shilingi milioni 200, hivyo kila mwananchi awe mlinzi wa mwenzake ili kulinda miundombinu hii ya mawasiliano.

Tunaipongeza Serikali kwa kujenga mnara kwenye kijiji chetu kwa kuwa tunapata mawasiliano na pale yanapokuwa hayapatikani yanakatika wataalamu wa kampuni ya TIGO wanafika na kurekebisha hali hii, “hakuna mawasiliano ya kampuni nyingine yoyote zaidi ya hii ya TIGO kwenye eneo hili”, amesema mkazi wa kijiji cha Mayamaya, Bwana Emmanuel Konyanza kilichopo kata ya Zanka wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.
Katika ziara hiyo ya Kamati kwenye kijiji cha Kizengi kata ya Kizengi iliyopo wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Meneja wa TTCL mkoa wa Tabora Bwana James Mlaguzi ameihaidi Kamati hiyo kuwa wataongeza upana wa masafa ya TTCL ili yaweze kufika kwenye vijiji vya mbali zaidi kwenye kata ya Kizengi ndani ya kipindi cha miezi miwili kuanzia sasa. Naye Diwani wa Kata hiyo Bwana Magindika Lugaira Masaga akizungumza kwa niaba ya wananchi mbele ya wajumbe wa Kamati hiyo amesema kuwa hapo mwanzo wananchi walikuwa na shida kubwa ya mawasiliano. 

Bwana Masaga anawashukuru wajumbe wa Kamati hiyo kufanya ziara na wanategemea kuwa huduma za mawasiliano zitaongezeka na kuwa bora zaidi kwa kuwa mawasiliano ya minara ya kampuni nyingine sio mazuri sana bali wanategemea mnara wa Halotel pekee ambao una masafa marefu na kufikia wananchi walio wengi zaidi. hivyo mnara wa TTCL ukikamilika utasaidia kuwafikia wananchi wengi zaidi wa kata hii yenye vijiji saba na wakazi 23,534.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...