WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Cuba
nchini Tanzania, Balozi Lucas Domingo Polledo, ambapo amewakaribisha
wafanyabiashara wa Cuba kuja kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya
dawa.
Amesema
kwa sasa Serikali ya Tanzania inaagiza dawa kutoka nje ya nchi jambo
ambalo linasababisha kutumia fedha nyingi, hivyo uwepo wa kiwanda
utasaidia katika kupunguza gharama. Pia wawekezaji watakuwa na uhakika
wa soko la bidhaa zao.
Waziri
Mkuu aliyasema hayo jana jioni (Jumanne, Agosti 22, 2017) wakati
akizungumza na Balozi Polledo mjini Havana. Waziri Mkuu yuko nchini Cuba
kwa ajili ya ziara ya kikazi yenye lengo la kudumisha ushirikiano kati
ya nchi hizo mbili.
Alisema
Serikali imedhamiria kuendeleza sekta ya viwanda nchini kama mkakati wa
kukuza uchumi na kufikia uchumi wa kati, hivyo wafanyabiashara kutoka
nchini Cuba wanakaribishwa kuja kuwekeza nchini, hususani katika viwanda
vya dawa na sukari.
Waziri
Mkuu alisema licha ya Tanzania kuwa ni nchi ya amani na yenye utulivu
wa kisiasa, pia imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji jambo ambalo
litawawezesha watakaokuja kuwekeza nchini kupata tija.
Pia
alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Cuba kwa ushirikiano mzuri na
Serikali ya Tanzania kwa sababu Cuba ni mojawapo kati ya nchi zenye
ushirikano wa muda mrefu na Tanzania hususani katika masuala ya Kisiasa,
Kijamii, Kielimu na Kiuchumi.
“Tanzania
na Cuba zina historia ya kutosha. Tunatambua mahusiano mazuri yaliyopo
kati nchi zote mbili, ambayo yalikuwepo kuanzia Serikali ya Awamu ya
kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere.”
Kwa
upande wake, Balozi Polledo alisema Serikali ya Cuba itahakikisha
uhusiano wake na Serikali ya Tanzania unaendelea kuimarishwa. Pia
alipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha maendeleo
pamoja na kukuza uchumi.
Alisema
licha ya kuwahi kufanya kazi kama Balozi katika nchi mbalimbali za
Afrika, baada ya kufika Tanzania amefurahishwa na kasi ya ukuaji wa
uchumi pamoja na kuimarika kwa hali ya siasa na amani.”Hali hii ni
tofauti na mataifa mengine ya Afrika.”
Pia
Balozi Polledo alisema kwamba Serikali ya Cuba itaendelea kushirikiana
na Tanzania katika uboreshaji wa Sekta za Afya na Elimu, ambapo alisema
jumla ya madaktari 50 wa Cuba wakiwemo maprofesa 11 wako nchini
wakihudumia wananchi katika mikoa mbalimbali.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, AGOSTI 23, 2017.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa (kulia) akisalimiana na Balozi wa Cuba Nnchini
Tanzania Bwana Lucas Domingo Polledo walipo kutana kwa mazungumzo ya
kikazi jana August 22/2017 akiwa katika ziara ya kikazi Havana Cuba. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Post a Comment