Watendaji
wa halmashauri za wilaya na manispaa wamekuwa ni kiwanda cha
kutengeneza hoja za mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa hesabu za Serikali kwa
kukosa umakini, uaminifu, uwajibikaji na kutokuzingata sheria, kanuni na
maadili ya utumishi wa umma.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema ameyasema hayo mapema leo katika baraza
maalumu la madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wakati wa
kujadili hoja 80 za Mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa
mwaka 2015/16 licha ya halmashauri hiyo kupata hati safi.
Dkt
Nchimbi amesema wamekuwa ndio wazalishaji wakubwa wa hoja tena hoja
zenyewe zikionyesha udhaifu wao wa kutotimiza wajibu wao huku akiwaeleza
kuwa hoja hizo zinaonyesha kuwa kuna udhaifu katika utendaji wao.
“Hoja
hazitengenezwi na madiwani, ni nyinyi watendaji kwa uvivu, mnashindwa
kufuata taratibu hadi mnazalisha hoja, mmekuwa ni kiwanda na kiwanda
chenyewe kibaya cha kuzalisha hoja, badilikeni”, amesisitiza Dkt
Nchimbi.
Aidha
amewataka madiwani kuwa wasimamizi wa miradi na shughuli za serikali
pamoja utendaji wa watumishi ili wasiendelee kuzalisha hoja kwakuwa
utendaji ukilega lega unawaathiri wananchi ambao ndio wamewaamini ili
wawakilishe.
Dkt
amewasisitiza kuwa watumishi wengine huja na kuondoka lakini madiwani
ndio wazawa hivyo maendeleo yao wanapaswa kuyasimamia kwa nguvu zote
wakishirikiana na watumishi pamoja na kuwashauri viongozi wa halmashauri
katika kuboresha utendaji.
Amewataka
madiwani pia kuwasimamia watumishi wasijiingize kwenye ushabiki wa
kisiasa na kupandikiza chuki kwa wananchi bali wao wajikite kwenye
kuhudumia wananchi na kuwaachia siasa madiwani na wanasiasa wengine.
Naye
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina M Lutambi ameishauri
halmashauri hiyo kuhakikisha wanafunga hoja hizo ili halmashauri hiyo
iendelee kupata hati safi.
Dkt
Lutambi amesema watumishi wasijisahau na kufanya kazi kwa mazoea bali
wachape kazi kwa bidii, kwa ubunifu na kwa kufuata taratibu ili kutoa
huduma nzuri kwa wananchi na kuepuka kuzalisha hoja.Ameongeza
kuwa taifa na halmashauri ya Ikungi inazo rasilimali za kutosha, jukumu
la watumishi ni kuhakikisha rasilimali hizo zinawanufaisha wananchi
wote bila upendeleo au kuzifuja.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Rustika Turuka
amesema yeye na watendaji wake wote watahakikisha wanazingatia ushauri
na maelekezo yaliyotolewa katika baraza hilo ili hoja zifutwe.
Turuka
ameongeza kuwa atahakikisha halmashauri ya Ikungi haipati hoja nyingi
na itaendelea kupata hati safi kama ambavyo imekuwa ikipata kwa kipindi
cha miaka mitatu mfululizo.
Amesema
kuwa atashirikiana na madiwani katika kuhakikisha halmashauri
inakusanya mapato yake vizuri na kuongeza vyanzo vingine vya mapato ili
waweze kutoa huduma kwa wananchi kwa ajili ya maendeleo ya Ikungi na
taifa kwa ujumla.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza katika baraza maalumu
la madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wakati wa kujadili hoja
za Mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali. Kulia kwake ni Mkuu
wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu na Kushoto kwake ni
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ally Mwanga.
Watumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi katika baraza maalumu la madiwani la kujadili hoja za Mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Rustika Turuka akizungumza katika
baraza maalumu la madiwani la kujadili hoja za Mkaguzi na Mthibiti Mkuu
wa Hesabu za Serikali.
Madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Ikungi katika baraza maalumu la madiwani la kujadili hoja za Mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Watumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi katika baraza maalumu la madiwani la kujadili hoja za Mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Ikungi katika baraza maalumu la madiwani la kujadili hoja za Mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.
No comments:
Post a Comment