Aliyekuwa
Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Lowassa amesema kuwa licha ya kuwa
upinzani nchini Tanzania unakumbwa na changamoto nyingi, lakini
atagombea tena urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Lowassa amesema kuwa atagombea tena na kwa mapenzi ya Mungu anaamini kuwa atashinda na kuingia Ikulu kwa mikono safi.
Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, aliyasema hayo
jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa Nation Media Group (NMG)
jijini Nairobi, Kenya.
“Kwa mapenzi ya Mungu nitajaribu tena mwaka 2020 na nitapita kwa mikono safi,” alisema Lowassa.
Kwa mwaka 2015, Lowassa aligombea urais kwa tiketi ya CHADEMA akiungwa
mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na kwa
mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), alipata kura 6,072,848 sawa
na asilimia 39.97 ya kura zote halali.
Lowassa alishindwa na Rais Magufuli ambaye alikuwa akipeperusha bendera
ya Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyejizolea kura 8,882,935 sawa na
asilimia 58.46.
Katika uchaguzi huo uliopita Lowassa aliukosoa na kusema kuwa aliibiwa
kura zake. Aidha, alifafanua kuwa, licha ya kuwa uchaguzi huo haukuwa
huru na wa haki, bado anamtambua John Pombe Magufuli kama Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Hata kama Dk Magufuli alichaguliwa katika mfumo usioaminika wa
uchaguzi, bado tunamheshimu kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Utendaji wa Rais Magufuli utaamuliwa na watu utakapofika
mwisho wa muhula huu mwaka 2020. Bora niwe makini katika hili nisije
nikanukuliwa vibaya nikaingia kwenye matatizo nitakaporudi nyumbani,”
alisema Lowassa
Kuhusu kuzuiwa kwa mikutano na maandamano ya kisiasa, Lowassa alisema
kuwa watakwenda mahakamani kuishtaki serikali kufuatia zuio hilo kwani
ni kinyume na sheria. Alisema kuwa, watu zaidi ya milioni 6 walimpigia
kura, lakini kitu cha ajabu haruhusiwi hata kwenda kuwashukuru.
“Nilipata kura milioni sita na siwezi kufanya mikutano hata ya
kuwashukuru watu kwa kunipigia kura. Hiyo si tu kinyume cha demokrasia,
bali si haki.”
Lowassa alikwenda Kenya kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Usalama, Jenerali Joseph Nkaiser aliyefariki hivi karibuni.
Mbali na siasa za Tanzania, Lowassa aliwasihi wa Kenya kufanya uchaguzi
kwa amani na kuepuka vurugu kama za mwaka 2007 ambazo zilipelekea zaidi
ya watu 1000 kufariki dunia, huku maelfu wakijeruhiwa pamoja na mali na
miundombinu kuharibiwa vibaya.
No comments:
Post a Comment