Pages

July 19, 2017

Balozi Seif Ali Iddi azindua Tamasha la 22 la Utamaduni wa Mzanzibari


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesisitiza umuhimu wa Jamii Nchini kuendelea kukuza maadili na kujiepusha na vitendo vya unyanyasi wa kijinsia dhidi ya Watoto na Wanawake ili irejeshea heshima yake Zanzibar. 
 
Alisema Visiwa vya Zanzibar havikuwa ni kituo muhimu cha Biashara katika mkarne zilizopita bali pia vilikuwa ni kitovu cha Elimu, heshima, ustaarabu na ukuzaji wa silka, mila na desturi za Utamaduni wa asili. 
 
Akilifungua Tamasha la 22 la Utamaduni wa Mzanzibari hapo katika Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduzi Michenzani Mjini Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwaomba wana Jamii kushirikiana na Wizara inayosimamia Utamaduni katika kuuenzi Utamaduni wa Taifa hasa kuhamasisha jamii kuepuka tabia zisizofaa zinazowadhalilisha Watoto, Wanawake na Watu wenye mahitaji Maalum. Balozi Seif alisema suala la kukuza utamaduni si jambo geni na ni vyema wazazi wa karne hii wakaiga mifano ya Wazazi wa zamani waliotumia mbinu mbali mbali zikiwemo sherehe za jando na unyago mfumo uliomtayarisha Kijana wa Kike na wa Kiume namna ya kukabiliana na maisha yake ya baadae. 
 
Alisema mfumo huo wa malezi uliozingatia heshima iliyopevuka Wazee hao pia walijumuisha matumizi ya hadithi, nyimba na hata misemo ya kiswahili katika kujenga tabia za Vijana zinazokubalika katika Jamii na Taifa kwa ujumla bila ya kutokea mgongano katika imani za Dini na Makabila. 
 
Balozi Seif alikumbusha kwamba Jamii iliyopita iliishi kwa Utamaduni wa kusaidiana malezi bila ya kulaumiana wala kudombana jambo ambalo liliashiria kuwepo kwa maadili mema katika jamii yaliyodhibiti matatizo ya udhalilishaji wa kijinsia ambao kwa sana unaonekana kama jambo la kawaida. 
 
Alisisitiza Wajibu wa Wazazi katika kushirikiana na Serikali na Taasisi zinazohamasisha haki za Watoto na Wanawake kuwafichua waovu wanaoendeleza vitendo vya kikatili vya ubakaji badala ya kuwatetea waovu hao waliokusudia kuliangamiza Taifa la baadae. 
 
Balozi Seif alieleza kwamba ni uhimu kwa Wananchi, Wazazi, Walimu wa Skuli hata wale wa Vyuo vya Quran kusimamia ipasavyo malezi ya Vijana kwa pamoja kwa vile wana nafasi kubwa ya kusaidiana na malezi hayo na utoaji wa miongozo kwa vijana wao. 
 
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na hata ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania zimeandaa Mikakati kadhaa katika kuhakikisha kwamba wale wote watakaohusika na vitendo vya udhalilishaji wa Watoto, Wanawaka na Watu wenye Mahitaji Maalum wanachukuliwa hatua za kinidhamu na Kisheria. 
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea faraja yake kutokana hatua kubwa zinazochukuliwa na Taasisi Maalum zilizomo ndani ya Wziara ya Kazi, Uwezeshaji, Vijana, Wazee, Wanawake na Watoto wakishirikiana na Taasisi za Kiraia zinasimamia kadhia hizo ambazo zinapigwa vita Kitaifa na Kimataifa. 
 
Aliipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kwa maandalizi mazuri ya mwaka huu yaliyojumisha shughuli mbali mbali zilizojumuisha Vikundi tofauti vya Wajasiri Amali wa Kazi za Mikono. 
Balozi Seif alisema kwmba hiyo inadhihirisha wazi kuwa ndani ya Utamaduni wa Taifa zimo hazina zitakazosaidia kuongeza Kipato cha Wananchi kupitia kazi zao za ujasiri amali. 
 
“ Wajasiri Amali wana umemo wao wanaouamini usemao Utamaduni wako ajira yako ”. Alifafanua Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
 
 Aliishauri Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kuendelea na desturi yake ya kushirikiana na Taasisi nyengine zenye kufanya Matamasha ya Utamaduni kwa lengo la kwenda sambamba na kasi ya kuulinda Utamaduni wa Asili. 
 
Alisema Matamasha hayo kama lile la Filamu la Kimataifa {ZIFF}, Tamasha la Mwaka Kogwa, Tamasha la Jahazi na Tamasha la Vyakula vya asili la Makunduchi yana mchango mkubwa katika kukuza Utamaduni wa Zanzibar na ni vyema yakadumishwa zaidi. 
 
Akitoa Taarifa ya Tamasha hilo Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni, Utalii na Michezo Nd. Omar Hassan Omar alisema lengo la Tamshala Utamaduni wa Mzanzibari ni kukuza na kuendeleza sanaa ya Utamaduni, kuwakusanya pamoja wazalishaji wa sanaa ili kulinda urithi wa Zanzibar.
 
Hata hivyo Ndugu alisema Utamaduni wa Zanzibar unapita katika wakati mgumu wa mmong’onyoko wa maadili kutokana na baadhi ya watu waovu kuendeleza Kisisi na uvundo wa ubakaji mambo ambayo lazima Jamii ijikaze katika kukabiliana nayo. 
 
Alisema vitendo hivyo mbali ya kulitia aibu Taifa lililokulia katika maadili ya heshima lakini pia linarudisha nyuma maendeleo ya wananchi kutokana na athari kubwa wanayoipata watu wanaoathirika na ubakwaji. 
 
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Hari, Utamaduni, Utalii na Michezo waliwahimiza na kuwaomba wananchi Mjini na Vijijini kutumia fursa ya kuangalia maonyesho mbali mbali ya kazi za wajasiria amali wa fani ya sanaa ndani ya Wiki nzima ya Tamasha litakaloendelea hadi Tarehe 25 mwezi huu. Akimkaribisha Mgeni Rasmi kulifungua Tamasha hilo Waziri wa Habari, Utamduni, Utalii na Michezo Mh. Rashid Ali Juma aliisisitiza Jamii kutilia nguvu Ujumbe wa Mwaka huu wa Tulinde Maadili yetu kupinga udhalilishaji ili kurejesha hadhi ya Utamaduni Zanzibar. 
 
Utamaduni ni moja ya tasnia inayokuwa kwa kasi Duniani ambayo imekuwa ikikuza Sekta ya Utalii inayotegemewa kuwa muhimili wa Taifa. Hivyo aliwapongeza Wajasiri amali kwa juhudi wanazochukuwa katika kuimarisha kazi za sanaa. 
 
Alisema ipo haja ya kutenga eneo maalum la kutunza na kuendelea na kufufua vitu vilivyoanza kupotea ambavyo ni nembo na ishara inayoitangaza Zanzibar Kiutamaduni na kuipatia sifa Zanzibar Kimataifa.
 
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliangalia maonyesho ya Vikundi vya wajasiri amali kutoka Wilaya mbali mbali za Unguja na kuridhika na kazi kubwa inayoendelea kufanya na wasanii hao katika kulinda na kuendeleza sanaa ya Zanzibar. 
 
Balozi Seif pia akapokea gwaride la vikundi vya sanaa vilivyojumuisha ngoma za asili kama ngoma ya ndege, Meni Bati, Boso,Mkurungu, usukaji wa vifaa vya sanaa, Dhikiri pamoja na Maulidi ya Homu. Ujumbe wa Mwaka huu wa Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari unaeleza – “ Tulinde Maadili yetu kupinga udhalilishaji ”.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...