Askofu Mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Blaston Gaville (kushoto).
Askofu Blaston Gaville wakati akiwekwa wakfu kuongoza Dayosisi ya Iringa ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
KUKAMILIKA
kwa mchakato wa uaandaaji wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kutasaidia kuweka misingi imara na kuondoa changamoto zilizopo
katika Katiba ya sasa, hivyo kukomesha ufisadi na kuinua uchumi wa
Tanzania.
Aidha,
kukamilika huko kwa Katiba Mpya kutaakisi jitihada kubwa zinazofanywa
na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli.
Hayo
yalisemwa hivi karibuni na Askofu Mteule wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Blaston Gaville, ambaye
alimtaka Rais Magufuli kuumalizia mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya,
kwani alisema mbali ya kuakisi kasi yake anayoifanya ya kukuza uchumi
pia kutasaidia kuhimiza uwajibikaji.
“Wakristo
na Watanzania kwa ujumla tuna imani kubwa na Serikali ya Awamu ya Tano
na ni matarajio yetu kwamba mchakato wa kuandika Katiba utamalizwa kama
lengo lilivyokuwa,” alisema.
Askofu Gaville amesimikwa ili kuchukua nafasi ya Askofu Dkt. Owdenburg Mdegella ambaye amestaafu.Alisema
wanatiwa moyo na jitihada zinazoendelea kufanywa na Dkt. Magufuli
katika kufufua uchumi na kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika kwa
manufaa ya Watanzania wote.
Alisema
Tanzania ina wanyonge wengi kuliko wenye nguvu, hivyo wanatiwa moyo na
jitihada zinazofanywa na Rais Magufuli na serikali yake hasa
anapowatetea wanyonge.Aidha,
pamoja na kupongeza jitihada hizo, Askofu Gaville, aliishukuru Serikali
ya Awamu ya Tano kwa kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa kodi akisema
hakuna nchi inayoweza kupata maendeleo bila mapato hayo.
“Tunaiomba
serikali iangalie upya suala la kodi kwa mashirika ya dini kwani baadhi
ya kodi tunazolipa, ikiwemo ya kuendeleza vyuo vya ufundi na ya Mfuko
wa Fidia kwa Wafanyakazi, zimekuwa mzigo mkubwa kwaetu.
“Kazi
ya Kanisa ni kutoa huduma, siyo kutengeneza faida, kodi hizo zimeleta
changamoto kubwa kwa uendeshaji wa taasisi, tunaomba serikali iziangalie
upya,” alisema.
Kuhusu
elimu, Askofu Gaville alisema Kanisa linasaidia watoto maskini ili
wapate haki yao ya elimu na akaiomba serikali isiwaingize katika kundi
la watoto wanaotoka katika familia zenye uwezo kwa sababu wanasoma shule
binafsi.
“Wanapojiunga
na vyuo vikuu, tunaomba Bodi ya Mikopo isiwanyime mikopo stahiki kwa
kisingizio cha shule wanazotoka, ufanyike upembuzi ili kutoa msaada kwa
walengwa wote,” alisema.
Aidha,
alisema Dayosisi ya Iringa inatoa mwaliko kwa vyama vyote vya kisiasa
na jamii nzima ya Watanzania kuendeleza na kukuza tunu ya ushirikiano na
moyo wa kizalendo ili kuwa na maendeleo yenye tija, badala ya kujenga
uhasama kwa sababu za kiitikadi.
Katika
salamu zake kwa waumini wa dayosisi hiyo, Askofu Mkuu wa KKKT Tanzania,
Dkt. Fredrick Shoo, alizipongeza kamati mbili za madini zilizoundwa na
Rais Magufuli akisema zimewaumbua baadhi ya Watanzania waliodhani ni
sifa kusaini mikataba ya madini inayonyonya haki ya Watanzania.
“Kama
hao watu waliosaini hiyo mikataba walidhani wanaisadia nchi huku wakijua
mikataba hiyo inalenga kuiibia nchi, wajue hayo ni mambo ya aibu na ni
upumbavu mkubwa kufanya mambo kama hayo kwa ajili ya matumbo yao
binafsi,” alisema.
Mkuu
wa Wilaya ya Mufindi, Jamuhuri William, akitoa salamu za serikali kwa
niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, alisema serikali
itaendelea kushirikiana na taasisi zote za dini ili kufikia malengo yake
ya maendeleo.
William
alizungumzia fursa mbalimbali za maendeleo zilizopo mkoani Iringa na
akawaomba Watanzania na wawekezaji kuzitumia ipasavyo kuunga mkono
jitihada za Rais za kuifanya nchi kuwa ya viwanda.
Katika
hatua nyingine, Askofu Mstaafu wa Dayosisi hiyo, Dkt. Owdenburg
Mdegela, aliipongeza serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa hatua
mbalimbali inazochukua kujirekebisha.
Akiungana
na mamia ya wakazi wa Mkoa wa Iringa katika maandamano ya amani siku
moja kabla ya kumsimika Askofu Gaville, Dkt. Mdegela alisema moja ya
makosa makubwa yaliyofanywa na serikali lilikuwa ni kuua Azimio la
Arusha la mwaka 1967.
Maandamano
hayo yalifanyika mjini Iringa kwa nia ya kupongeza juhudi zinazofanywa
na Rais Dkt. Magufuli katika kushughulikia changamoto zinazolikabili
Taifa, ambapo yalipokelewa katika viwanja vya Mwembetogwa na Mkuu wa
Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, huku yakihudhuriwa na viongozi mbalimbali
wa dini, siasa na serikali, watumishi, wanafunzi, wafanyabiashara na
wadau wengine wa maendeleo kutoka wilaya zote za mkoa huo.
“Hatukupaswa
kuua Azimio la Arusha pamoja na kwamba kuna mambo yalipaswa
kubadilishwa. Kimsingi azimio lile lilikuwa na mambo mengi ya msingi
ambayo ni ya faida kwa Taifa, hayo ni pamoja na maadili kwa viongozi na
msingi wa kujitegemea,” alisema.
Alibainisha
wazi kwamba, serikali ya CCM ilichoka, lakini kupitia kwa Rais Magufuli
imeanza kujirekebisha ikiwa ni pamoja na kutembea katika misingi ya
Azimio la Arusha, hatua inayopaswa kupongezwa hadharani.
“Anayempinga
Rais anayekamata wezi, watumishi hewa na anayepambana kulinda
rasilimali za nchi kwa manufaa ya Watanzania wote na kuhimiza
uwajibikaji lazima atakuwa alipata matokeo mabaya ya mtihani wa darasa
la saba na kidato cha nne.
“Tunapaswa
kuiona falsafa ya kiongozi wetu pamoja na kwamba wapo watu wanambeza
kwa maneno mengi ya kuudhi lakini wanaombeza Magufuli wakumbuke kwamba
hata Mungu alibezwa na theluthi moja ya malaika zake,” alisema.
Amina
Masenza, katika utangulizi wake, alisema Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015
inasema katika miaka mitano ijayo, CCM itazielekeza serikali zake
kutumia nguvu zake zote kuondoa umaskini, kutatua tatizo la ajira hasa
kwa vijana, katika vita dhidi ya rushwa na ubadhilifu wa mali za umma na
kudumisha amani, ulinzi na usalama.
No comments:
Post a Comment