Pages

June 30, 2017

WANANCHI MKOA WA ARUSHA WALALAMIKIA KUTAPELIWA NA SACCOS

Arusha.Wananchi zaidi ya  50 mkoani hapa wamedai kutapeliwa na taasisi ya fedha iitwayo Tanzania Pastors Saccos Limited yenye makao yake makuu jijini Dar  es Salaam zaidi ya Sh 120 milioni walizozitoa zikiwa  amana kabla ya kuanza kunufaika na mikopo kama walivyoahidiwa na taasisi hiyo.


Katika barua yao kwa Mkuu wa mkoa wa Arusha,Mrisho Gambo waliyomwandikia Juni 6 ,mwaka huu wakiomba awasaidie kuwabana watuhumiwa warejeshe fedha zao baada ya jitihada zao kukwama katika kuwafatilia waliokua viongozi wa  taasisi hiyo na vyombo vya dola.


Akizungumza kwa niaba ya wenzake,Mchungaji Peter Kitilla alisema taasisi hiyo ilianza shughuli zake jijini Arusha Kata ya Unga Limited na Mianzini baadaye kufungua matawi eneo la Tengeru na Kikatiti wilaya ya Arumeru huku ikiwa inawachangisha  wanachama wapya fedha za kiingilio,akiba na kununua hisa.


“Lengo la Saccos hii ambayo wengi tulisadiki kuwa inatokana na watumishi wa Mungu kutokana na jina lao na malengo yake ambayo hakika yalikua ni kuweka akiba,kutoa mikopo ya aina mbalimbali kwa muda muafaka na kuweka utaratibu wa kurejesha fedha hizo,”alisema Mchungaji Kitilla


Alisema mwakilishi wa taasisi hiyo aliyekuja kufungua matawi Arusha,Paulo Daniel baada ya kukusanya kiasi hicho cha fedha kutoka kwa wanachama aliowapata alitokomea kusikojulikana Desemba mwaka jana na harakati za kumtafuta zilifanikiwa kumpata Januari  mwaka huu  jijini Mwanza  na aliletwa Arusha chini ya ulinzi wa polisi.


Mchungaji Kitilla alisema katika kipindi hicho hadi sasa hawajui kinachoendelea licha ya jitihada zao za mara kwa mara kufatilia ofisi ya Mkuu wa Makosa ya Jinai(RCO) mkoa  kwani hakuna dalili ya kurejeshewa mamilioni yao.


Naye Lucas Kitomary alisema baada ya ofisi ya RCO kuwatafuta viongozi wa taasisi hiyo makao makuu jijini Dar es Salaam walifika Arusha na kuahidi hadi mwezi Februari watakua wamewarejeshea fedha zao lakini hadi wanamwandikia Mkuu wa Mkoa barua walikua wamekata tamaa.


“Mheshimiwa Mkuu wa mkoa hadi tunaandika barua hii kwa machungu mengi Saccos hii ilianza kutapeli wanachama kwa kukusanya akiba za watu kwa ahadi ya kutoa mikopo kwa muda mfupi,lakini hawakutoa mikopo kama walivyoahidi kwa mfano tu mmoja wa wanachama aliyeanza kuchangia tangu mwezi Agosti mwaka jana,”alisema Kitomary


Alisema baada ya tukio hilo ofisi za taasisi hiyo zilifungwa wakati hatima ya wao kurejeshewa fedha zao zikionekana kugonga ukuta huku wanachama wakiwa hawapewi maelezo ya kutosha namna watakavyorejeshewa hizo fedha kwani wameathirika sana kutokana na wengine kushindwa kumudu maisha baada ya fedha walizokua wametoa kama akiba kwaajili ya kupata mikopo kuyeyuka.


Naye Mtendaji Mkuu wa Tanzania Pastors Saccos Limited,Nathaniel Mwaluko alisema taasisi yake inafanya kazi kwa weledi na makosa yaliyofanywa na mwakilishi wao,Paulo Daniel ni binafsi na anashikiliwa kwa mahojiano ili aweze kuukabili mkondo wa sheria.


“Sisi tulimtuma kuhamasisha watu na kuwaeleza namna taasisi yetu inavyofanya kazi na manufaa yake lakini akakusanya fedha bila kupata mwongozo wa ofisi jinsi unavyotakiwa baada ya wanachama kuwa wakali alitoroka na tulifanikiwa kumkamata na yupo mikononi mwa polisi,”alisema Mwaluko

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...