Na Jumia Travel Tanzania
Inaonekana
mwaka 2017 umeanza vizuri katika sekta ya utalii nchini Tanzania
kutokana na watu kadhaa mashuhuri kuzuru vivutio vyake. Sehemu ambazo
zimeonekana kuwavutia watu wengi zaidi ni hifadhi ya mbuga ya Serengeti
na bonde la Ngorongoro.
Alianza
mwigizaji maarufu wa filamu kutokea Hollywood nchini Marekani, Will
Smith na mkewe Jada Pinkett-Smith. Mwanzoni mwa mwezi Machi walitua
nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na
kujivinjari katika mbuga ya Serengeti. Wakiwa huko familia ya Smith
walikutana na msanii mwingine kutokea huko huko Marekani, lakini huyu
yeye ni mwanamitindo na mrembo, Chanel Iman.
Haikupita muda mrefu
sana tangu watu hao mashuhuri kuwepo nchini, kwani siku chache
zilizopita aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Taifa la Israel, Bw. Ehud Barak
naye alitembelea mbuga ya Serengeti pamoja na Ngorongoro.
 Hii
ni ishara nzuri kwa sekta ya utalii nchini ambapo kupitia watu hawa
maarufu wengine nao wanapata taarifa na kuhamasika kutembelea pia.
Lakini
lazima tujiulize ni kwa nini Ngorongoro huwavutia watu zaidi na
kuwafanya kufunga safari kuja Tanzania na sio sehemu zingine? Jumia
Travel imekukusanyia vitu ambavyo vinapatikana katika eneo hilo la
urithi wa dunia ambalo hakuna mtu atakayesimuliwa na kutotaka
kulitembelea:
Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro. Kama ulikuwa
haufahamu bonde la Ngorongoro ni shimo kubwa lililotokana na mlipuko wa
volkeno ambalo halijai maji wala kubomoka duniani. Eneo hili ambalo
limetangazwa kuwa ni urithi wa dunia na Shirika la Umoja wa Mataifa la
Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO); lina urefu wa kilometa 20, kina
cha mita 600 na ukubwa wa kilometa za mraba 300.
 Vifuatavyo ni vivutio vinavyopatikana katika hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro:
Binadamu
na Wanyama kuishi pamoja. Kwa zaidi ya miaka 200 iliyopita watu wa
kabila la Wamasai walifika eneo hili na kuishi hapo. Maisha yao ya jadi
yamewafanya waweze kuishi pamoja na mifugo yao kwa amani na utulivu
kabisa bila ya kuwabugudhi wanyamapori. Mpaka hivi sasa kuna wafugaji wa
Kimasai takribani 42,000 wakiishi katika hifadhi pamoja na mifugo yao
kama vile ng’ombe, punda, mbuzi na kondoo. Kipindi cha mvua hutoka eneo
hili na kuelekea maeneo ya tambarare ambapo kiangazi kikifika hujisogeza
maeneo ya karibu ya mlima na misitu iliyopo. Wamasai huruhusiwa
kuingiza mifugo yao kwa ajili ya kuilisha na kuinywesha lakini si
kufanya shughuli za kilimo; lakini maeneo mengine ya hifadhi
wanaruhusiwa kurandaranda.
Bonde la Volkeno na Wanyamapori. Bonde
la Ngorongoro lilitokana na mlipuko wa volkeno takribani miaka milioni 3
iliyopita ambapo ni kubwa, lisilobomoka wala kutojaa maji. Lilitangazwa
na UNESCO kuwa ni urithi wa dunia mwaka 1979 na ni eneo pekee ambalo
binadamu, mifugo na wanyama wanaishi kwa pamoja kwa amani na utulivu
kabisa. Unaweza kukuta kuna wakati ng’ombe wa Wamasai wanachunga pamoja
na pundamilia katika mbuga za Ngorongoro. 
Masalia
ya Kale ya Binadamu wa Mwanzo. Ngorongoro ndimo linapopatikana bonde la
Olduvai ambalo kwa mujibu wa wanahistoria yanapatikana masalia ya
binadamu wa mwanzo kuishi duniani. Hapa ndipo wanaikolojia maarufu Dkt.
Louis na mkewe Mary Leakey walipata masalia ya kale likiwemo fuvu la mtu
wa kale zaidi, Zinjanthropus, ambaye alipata kuishi miaka milioni 1.75
iliyopita. Utafiti wao uliweza kuvumbua mabadiliko ya taratibu ya ukubwa
wa ubongo na zana zao za mawe walizokuwa wanazitumia.
Vivutio
vingine. Mbali na vivutio vilivotajwa hapo juu pia kuna vitu vingine
chungu nzima vya kuvutia watu wanavyoweza kuvifurahia kuviona.
Ziwa
Ndutu na Masek; maziwa haya hujaa kutokana na maji yanayotiririka
kutokea milimani, na maji yake hayafai kwa matumizi ya binadamu kutokana
na chumvi nyingi iliyonayo.
Oldonyo
Lengai; hili ni jina la lugha ya Kimasai likiwa na maana ya ‘Mlima wa
Mungu,’ unapatikana nje kidogo ya hifadhi ya Ngorongoro. Ni mlima pekee
wenye volkeno hai ambapo ilishawahi kulipuka mwaka 2006 na siku za hivi
karibuni mwezi Julai mwaka 2007.
Mchanga Unaohama; safu ya
mchanga mweusi umetakana na majivu ya mlima wa volkeno wa Oldonyo
Lengai, umekuwa ukisukumwa taratibu kuelekea upande wa Magharibi wa
hifadhi kwa kiwango cha mita 17 kwa mwaka. Una kimo cha mita 9 na mzingo
wenye urefu wa mita 100, unapatikana Kaskazini mwa bonde la Olduvai.
Bonde
la Olkarien; eneo hili nalo ni muhimu katika hifadhi kwani hutoa
hifadhi kwa ndege tai aina ya Ruppell Griffon. Msimu mzuri wa kutembelea
eneo hili ni miezi ya Machi mpaka Aprili ambapo tai huzaliana. Wanyama
huja eneo hili pale panapokuwa na malisho ya kutosha.

Kutazama
ndege aina ya Flamingo na wengineo wa kila aina. Ndege aina ya Flamingo
wanaonekana sana katika maziwa yanayopatikana ndani ya hifadhi. Mbali
na ndege hao pia kuna aina mbalimbali za ndege ambao wanaweza kuonekana
katika misimu tofauti ya majira ya mwaka hususani miezi ya mvua.
Safari
ya Kuizunguka Hifadhi. Utakuwa hujaifaidi Ngorongoro kama
haujavizungukia vivutio mbalimbali vinavyopatikana ndani yake. Kwa
kuwatumia waongozaji wa mbuga, hakikisha kwamba unatembelea sehemu kama
vile bonde la Olmoti kuelekea nyanda za Embakai, shuka chini kuelekea
Bonde la Ufa, pandisha Kaskazini kwenye nyanda za hifadhi ya misitu na
kisha eneo la tambarare la Mashariki kuzunga miamba ya Nassera, milima
ya Goli na bonde la Olkarien.
 Kwa
hakika hii ni Edeni ya sasa kama watu wengi wanavyopenda kuiita
kutokana na maajabu iliyonayo pamoja na historia ya binadamu wa mwanzo
kuishi mule. Sasa kama watu wanasafiri kutoka kila pembe ya dunia kuja
kulitembelea eneo hili kwa nini na wewe mtanzania usitenge muda na
kupanga kufanya hivyo? Haihitaji kuwa milionea kutembelea eneo hili,
kunafikika kwa urahisi na hata malazi ni nafuu pia kwani Jumia Travel
wamekurahisishia hilo.
|
إرسال تعليق