Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akizungumza kwenye mkutano na Rais wa Shirika la Datang Telecom International Technology Company Limited la Serikali ya China Bw.Yuan Yong na ujumbe wake ambapo alipokea taarifa ya mpango wa serikali ya China wa kuikopesha TTCL ili kuipa uwezo wa kiteknolojia na kupanua mtandao wa mawasiliano vijijini na mijini pamoja na kujenga kiwanda cha kutengeneza vifaa vya mawasiliano hapa Tanzania. (Picha na kwa hisani ya Ofisi ya Makamu wa Rais).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja
na Rais wa Shirika la Datang Telecom International Technology Company Limited
la Serikali ya China Bw.Yuan Yong na ujumbe wake mara baada ya kupokea taarifa
ya mpango wa serikali ya China wa kuikopesha TTCL ili kuipa uwezo wa
kiteknolojia na kupanua mtandao wa mawasiliano vijijini na mijini pamoja
na kujenga kiwanda cha kutengeneza vifaa vya mawasiliano hapa Tanzania. (Picha
na kwa hisani ya Ofisi ya Makamu wa Rais).
...................................................................................
Shirika
la Datang Telecom International Technology Company Limited la Serikali ya China
lina mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha kutengeneza vifaa vya mawasiliano
nchini kwa ushirikiano na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).
Rais wa Shirika
hilo Yuan Yong ametoa kauli hiyo leo tarehe 1 mwezi Machi 2017 baada ya kukutana na kufanya
mazungumzo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia
Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es Salaam.
Yuan Yong
amemweleza Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Serikali ya China pia ina
mpango wa kuikopesha Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kiasi cha shilingi bilioni
600 ili kuipa uwezo wa kiteknolojia na kupanua mtandao wa mawasiliano katika
maeneo mbalimbali nchini hasa vijijini.
Rais huyo
amesema lengo la mkakati huo ni kuifanya TTCL kuwa Kampuni bora inayotoa huduma
za mawasiliano kwa njia ya kisasa kuliko kampuni yeyote katika ukanda wa Afrika
Mashariki na kati.
Amesema
kuwa mahusiano mazuri kati ya Tanzania na China ndio yamepelekea shirika hilo
kuweka mikakati ya kuja kuwekeza nchini katika sekta ya mawasiliano ili
kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata huduma bora za mawasiliano mijini na
vijijini kwa njia ya kisasa bila usumbufu wowote.
Kwa
upande wake, Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameonyesha
kufurahishwa na mikakati hiyo na kusisitiza kuwa serikali ipo tayari kwa
uwekezaji huo mkubwa kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa pande hizo Mbili.
Makamu wa
Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema anaimani kubwa kuwa uwekezaji huo
ukikamilika utaiwezesha (TTCL) kufanya kazi kwa ubora wa hali ya juu kwa
kutumia teknolojia ya kisasa.
Makamu wa
Rais amesema serikali ya awamu ya Tano imedhamiria kuelekea katika uchumi wa
viwanda kwa kishindo hali ambayo itasaidia taifa kuongeza pato lake la taifa
pamoja na kutoa ajira kwa mamia ya wananchi kupitia viwanda ambazo vitajengwa
nchini.
Makamu wa
Rais Mhe Samia Suluhu Hassan pia amepongeza mpango wa Shirika hilo la
Mawasiliano la Serikali ya China wa kutoa mafunzo mbalimbali kwa wafanyakazi wa
TTCL ikiwemo ujenzi wa Kituo Kikubwa cha Utafiti wa Mawasiliano nchini hatua
ambayo itasaidia kuimarisha utendaji kazi kwa wafanyakazi wa TTCL ili waweze
kuendana na teknolojia ya kisasa ya mawasiliano Duniani kupitia tafiti
zitakazofanywa nchini.


إرسال تعليق