Wanafunzi wa shule za Msingi mkoani hapa wametakiwa kuwa
makini na kutokuwa na tamaa ya kuomba “lift” au kupewa chipsi au kushawishiwa
kwa namna yoyote ile na watu ambao hawafahamiana nao pindi wanapokwenda shule
au wanaporudi majumbani kwao.
Hayo yalielezwa na Mkuu wa kitengo cha Dawati la Jinsia na
Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu wakati alipokuwa akitoa
elimu ya Ukatili na Unyanyasaji wa kijinsia katika vipengele vya ubakaji, ulawiti
na vipigo kwa wanafunzi 63 wa Elimu Maalum kitengo cha viziwi katika shule ya
Msingi Meru iliyopo halmashauri ya jiji la Arusha.
Alisema baadhi ya wanafunzi wanajikuta wanafanyiwa vitendo
vya ukatili wa kijinsia kama ubakaji na ulawiti baada ya ushawishi mdogo mdogo kwa
kupewa lift, kununuliwa vyakula mbalimbali kama vile chipsi na kadhalika.
“Baadhi ya vitu ambavyo vinasababisha ushawishi na hatimaye
wanafunzi wanafanyiwa ukatili wa kubakwa au kulawitiwa bila hata wao wenyewe
kudhani kama hali hiyo inaweza kutokea ni pamoja na lift za magari au pikipiki,
kununuliwa vyakula mbalimbali kama vile chipsi.”. Alisema Mkuu huyo wa Dawati
Happyness Temu.
“Sio watu wote wana nia mbaya katika utoaji wa “lift” ila
kuna wachache si wema na hawawezi kujulikana yupi mwema na yupi mbaya hivyo wazazi
wanatakiwa wawafuatilie kwa ukaribu na kuwaeleza uhalisia wa mabadiliko ya
maisha watoto wao ili kuwaepusha na watu wenye nia mbaya dhidi yao”. Aliongeza Mkaguzi huyo wa Polisi Happyness Temu.
Wakiongea kwa lugha ya ishara na kutafsiriwa na walimu wa
shule hiyo Veila Wilson na John Maukiri, baadhi ya wanafunzi walionyesha
kufurahia elimu hiyo na kupata ufahamu juu ya hatua wanazoweza kuchukua katika
kujiepusha na vitendo vya ukatili na unyanyasaji na pia walifahamu hatua za
kuchukua mara watakapofanyiwa ukatili wa aina yoyote.
Baadhi ya wanafunzi hao walikiri kufanyiwa hasa ukatili wa
vipigo majumbani mwao huku mkuu huyo wa Dawati kuahidi kuwasilikiza
walalamikaji na kufuatilia kwa ukaribu kwa nia ya kukomesha tabia hiyo.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ambayo inamchanganyiko wa
wanafunzi wa elimu ya kawaida na elimu maalum Bw.Musa Luambano, alilishukuru Jeshi
la Polisi kupitia kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto kwa kutoa elimu hiyo
kwa wanafunzi hao ambayo itawasaidia kujua hatua za kuchukua pindi
wanapofanyiwa ukatili lakini pia wao watakuwa mabalozi kwa wengine katika
kuwaelimisha.
| Mkuu wa kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu akiwa katika picha ya pamoja na Walimu na Wanafunzi wa shule ya Msingi Meru kitengo cha elimu maalum. |

إرسال تعليق