MAJALIWA ATEMBELEA VIWANDA JIJINI ARUSHA, AWATAKA WAHANDISI WASHAURI KUTOTUMIA VIBAYA DHAMANA WALIZOPEWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wahandisi Washauri nchini kutotumia vibaya vyeo na dhamana walizonazo kwa kuwalazimisha wakandarasi kununua bidhaa sehemu wanazotaka wao na badala yake wawashauri kununua bidhaa bora.
Pia amewataka watendaji wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Wakurugenzi wa Halmashauri na Majiji nchini pamoja na Wahandisi Washauri kutumia mabomba yanayozalishwa na viwanda vya ndani kwa kuwa yanakidhi viwango vya ubora.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Desemba 3, 2016) wakati wa uzindizi wa kiwanda cha kutengeneza bidhaa za plastiki cha Lodhia, akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Arusha. 
“Serikali inalenga kumaliza tatizo la ajira hasa kwa vijana na Serikali pekee haiwezi kuwaajiri watu wote. Viwanda pekee ndivyo vyenye uwezo wa kuzalisha ajira nyingi. Jukumu letu ni kuviunga mkono,” amesema.
Amesema haoni sababu ya halmashauri na wakandarasi kununua mabomba kutoka nje ya Arusha au nje ya nchi wakati bidhaa hizo zinazalishwa na wawekezaji ndani ya mkoa huo na zinakidhi viwango vya ubora.
Hata hivto Waziri Mkuu amewataka watumishi wa kiwanda hicho kufanya kazi kwa weledi na uaminifu mkubwa ili kukiwezesha kuzalisha bidhaa nyingi zaidi na hatimaye kuongeza ajira.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Sailesh Pandit amesema  moja ya changamoto kubwa inayowakabili kiwandani hapo ni kushindwa kuuza bidhaa wanazozalisha katika miradi mikubwa ya maji iliyotekelezwa Mkoani Arusha.
Amesema “licha ya kuwa na viwango vya ubora vilivyothibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS)  na ISO tunashindwa kuuza kutokana na hujuma tunazofanyiwa na baadhi ya wahandisi wa Halmashauri na washauri elekezi wa miradi ya maji mkoani hapa,”.
Mkurugenzi huyo alisema "Mheshimiwa Waziri Mkuu mara kadhaa wakandarasi wamezuiwa kununua mabomba ya maji kutoka kwenye kampuni yetu na badala yake hulazimishwa kununua mabomba kutoka nje ya Mkoa wa Arusha na kuisababishia serikali gharama zisizo za lazima "
Amesema kampuni hiyo imetoa ajira rasmi kwa Watanzania 1,300 huku wengine zaidi ya 500 wakinufaika kutokana na ushiriki wao katika utoaji wa huduma kiwandani hapo. Kiwanda kinalipa wastani wa sh. bilioni 20 kwa mwaka kama kodi na tozo mbalimbali.
Baada ya kutoka kiwandani hapo Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kutengeneza bodi za magari cha Hanspaul ambapo amewataka Wakurugenzi wa halmashauro zote nchini wanaohitaji magari ya kuzolea taka kwenda kununua katika kiwanda hicho.
“Tumekua tunanunua magari ya kuzolea taka kwa gharama kubwa ambayo ni kati ya sh. milioni 300 hadi sh. milioni 400 kutoka nje ya nchi wakati magari hayo yanapatikana Tanzania tena mkoani Arusha kwa sh. milioni 200,” amesema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAMOSI, DESEMBA 3, 2016.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua kiwanda cha Lodhia Plastic Industries Limited kabala ya kukitembelea kiwanda hicho Desemba 3, 2016.   Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho  Gambo na kulia kwa Waziri Mkuu ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Nodhia Group, Haroon Lodhia.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Kiwanda cha Lodhia Plastic Industries Limited cha jijini Arusha, Haroon Lodhia (kushoto ) kuhusu utengenezaji wa mabomba ya plastic wakati alipotembelea kiwanda hicho,Desemba 3, 2016.
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kitazama matangi yanayotengenezwa katika kwanda cha Lodhia Plastic Industries wakati alipokitembelea kiwanda hicho Desemba 3, 2016 .
 Waziri Mkuu,Kasim Majaliwa akitazama gari linalotengenezewa bodi maalum kwa ajili ya shughuli za utalii wakati alipotembelea kiwanda cha kutengeneza mabodi ya magari cha HansPaul cha jijini Atusha Desemba 3, 2016.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha Fibreboards cha Arusha, Tosky Hans (wapili kulia) kuhusu bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho wakati alipokitembelea Desemba 3, 2016. Watatu kulia ni Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha unga cha MONABAN cha Arusha wakati alipokitembelea  Desemba 3, 2016
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mfuko wenye unga wakati alipotembelea kiwanda cha unga cha MONABAN jijini Arusha Desemba 3, 2016
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua shehena ya ungwa uliosindikwa wakati alipotembelea kwanda cha unga cha MOBAN cha jijiniArusha Desemba 3, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 

Post a Comment

Previous Post Next Post