Mkuu wa Mkoa wa
Arusha Mhe. Mrisho Gambo akiwasalimiana na viongozi wa Wilaya katika
eneo la mapokezi wakati wa ziara yake Wilayani hapo.
Nteghenjwa Hosseah , Monduli.
Mkuu wa Mkoa wa
Arusha, Mrisho Gambo ameuagiza uongozi wa wilaya ya Monduli Mkoani
Arusha pamoja na baraza la madiwani la wilaya hiyo kuhakikisha
wanabadilisha umiliki wa shamba la Manyara ranch lenye ukubwa wa ekari
44,930 kutoka kwa taasisi ya Tanzania Land Conservation Trust{TLCT}
kwenda kwa wananchi wa vijiji viwili kama Rais wa awamu ya tatu Mhe.
Benjamini William Mkapa alivyoagiza.
Rc Gambo alitoa
agizo hilo katika mikutano ya hadhara iliyofanyika katika kata ya
Elesilalei na Makuyuni baada ya kutembelea miradi ya mamilioni ya fedha
iliyopo ndani ya shamba hilo inayofadhiliwa na African Wildlife
Foundation{AWF} na kuelezwa kero na changamoto zilizopo juu ya umiliki
wa shamba hilo kwa taasisi ya TLCT.
Mkuu wa Mkoa wa
Arusha akitoa maelekezo ya kubadilisha Hati ya Umiliki wa shamba kutoka
kwa TLCT kwenda kwa wananchi wa vijiji vya Elesilalei na Ortukai.
Alisema nyaraka
zinaonyesha wazi kuwa Shamba hilo lilitolewa kwa wananchi wa vijiji vya
Elesilalei na Ortukai na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu mwaka 1999
kwa ajili ya kilimo na ufugaji lakini hilo halikufanyika badala yake
taasisi ya TLCT ikajimilikisha shamba hilo kinyume na maagizo.
Mkuu huyo wa
Mkoa alisema kutokana na hali hiyo ninawaagiza viongozi wote wa wilaya
ya Monduli wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo pamoja na baraza la
madiwani kuhakikisha ndani ya muda mfupi wanabadilisha umilikiwa wa
shamba hilo kutoka taasisi hiyo kwenda katika vijiji hivyo.
Gambo alisema
serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuli iko
madarakani kwa ajili ya kuwahudumia wanyonge na watu wa hali ya chini na
kamwe haiwezi kuona baadhi ya watu fulani wananufaika na rasilimali ya
nchi kwa manufaa yao.
Meneja wa Ranch
hiyo Ndg. Fidelis Ole Kashe akiwasilisha taarifa ya Shamba hilo kwenye
Kikao maalum na Mkuu wa Mkoa wa Arusha pamoja na viongozi wa Wilaya.
Alisema TLCT
inamiliki shamba hilo kinyume na maagizo kwani shamba hilo lilipaswa
kumilikiwa na vijiji hivyo kwa faida yao lakini walijitokeza wataalamu
wakabadilisha maelekezo hayo na kujimilikisha kitu ambacho Serikali ya
Awamu ya Tano haiwezi kulivumilia kamwe.
‘’Nimeagiza
umiliki wa shamba hili unapaswa kubadilishwa haraka kwa kushirikisha
vikao na kufuata taratibu zote za kisheria ikiwemo kupitishwa na baraza
la madiwani ili wananchi waweze kunufaika na ardhi yao na sio watu
wachache wanaolipwa mamilioni ya fedha bila ya sababu za msingi’’alisema
Gambo.
Naye Mbunge wa
Jimbo la Monduli, Mhe. Julius Kalanga na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo
Mhe. Isack Joseph wote kwa pamoja waliunga mkono wazo la Mkuu wa Mkoa na
kusema kuwa watatoa ushirikiano wa dhati kuhakikisha umiliki wa shamba
hilo unabadilishwa na kwenda kwa vijiji hivyo.
Mkurugenzi wa TLCT Ndg. Boniface Ngimojiro akielezea muundo wa Taasisi hiyo yenye umiliki wa Shamba la Manyara Ranch.
Mkurugenzi wa
TLCT Bonfance Ngimojiro alipopewa nafasi ya kujieleza katika mikutano
hiyo miwili alisema kuwa taasisi hiyo inaongozwa na bodi ya wadhamini
yenye wajumbe nane wakiongozwa na Mbunge wa zamani wa Mondul, Mhe.
Edward Lowassa kama mwenyekiti wa Bodi hiyo.
Ngimonjiro
alikiri kupata amri ya kubadilishwa umiliki wa shamba hilo kutoka katika
taasisi hiyo kwenda kwa wananchi wa vijiji hivyo viwili lakini yeye
hawezi kujuwa ni kwa nini amri hiyo hadi jana haikutekelezwa.
Mkurugenzi huyo
alisema yeye ni mwajiriwa tu ambaye hajalipwa mishahara kwa miaka zaidi
ya minne sasa katika taasisi hiyo hivyo hawezi kujuwa kwa undani zaidi
kushindikana kutekelezwa kwa amri hiyo kwani wakitafutwa wahusika
wanaweza kuwa na majibu sahihi.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo akikagua Boma la Ngombe lililopo katika shamba la Manyara Ranch.
Naye Meneja wa
AWF, Fidelis Ole Kashe yeye alisema kuwa wamekuwa wakifanya kazi katika
mazingira magumu sana ndani ya shamba hilo pamoja na kufadhili miradi
mbalimbali ya maendeleo katika shamba hilo ikiwemo shule,zahanati
,ufugaji wa kisasa na machinjio.
Kashe alisema
utulivu ndio njia pekee itayofanya miradi iliyopo katika shamba hilo
kuendelea vinginevyo wafadhili hao wanaweza kusikitisha kila kitu.
Alisema AWF
imekuwa mstari wa mbele kufadhili miradi mbalimbali katika wilaya ya
Monduli na nchini kwa ujumla na inapenda kuona fedha inazotoa zinafanya
kazi iliyokusudiwa na sio vinginevyo.
Mbunge wa LongIDO Mhe. Julius Kalanga(kulia) akiwa na viongozi wa Chama cha Mapinduzi katika ziara ya Mkuu wa Mkoa.
Eneo la malisho kwa ajili ya Ngombe 780 waliopo katika shamba hilo na Kondoo 300.

إرسال تعليق