Mratibu wa Mradi kutoka Tamisemi Sanford Kway akielezea wajibu wa Wizara
katika kusimamia Mradi huu wa Mabadiliko ya hali ya hewa na tabia ya nchi
katika halmashauri 15 Tanzania.
|
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo akitoa
maelekezo katika kikao cha kutambulisha Mradi wa Mabadiliko ya hali ya hewa na Tabia
ya Nchi.
|
Nteghenjwa
Hoseah, Arusha
Wakuu wa Wilaya
za Arusha kusimamia Mradi wa Mabadiliko ya Hali ya hewa Na Tabia ya Nchi
Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mhe Mrisho Gambo
amewaagiza Wakuu wa Wilaya tatu za Mkoa wa Arusha zinazotekeleza mradi wa mabadiliko ya hali ya
hewa na tabia ya nchi kuwa Wenyeviti wa kamati za mradi huo ili
kuharakisha utekelezaji wake katika
maeneo hayo.
Akizungumza katika kikao cha kutambulisha
mradi huo wa awamu ya Pili utakaofanya kazi katika wilaya za Ngorongoro, Monduli
na Longido za Mkoa wa Arusha kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2016
hadi 2021 alisema kuna haja ya kuimarisha usimamizi wa mradi huu ili kuwajengea uwezo wanajamii katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya
hali ya hewa na tabia nchi ili mradi huu uweze kuleta Tija iliyokusudiwa.
Alisema awali kamati hizo zilikuwa
zikisimamiwa na Maafisa Mipango katika halmashauri hizo ila kutokana na
majukumu yao ameonyesha wasiwasi iwapo wanaweza kuusimamia ipasavyo hivyo
aliwataka Wakuu wa wilaya kuwa vinara wa
kuusimamia na kuratibu kwa karibu ili
kuleta mapinduzi katika maeneo ya wafugaji na kuhakikisha wanatengeneza mfumo imara
na
utekelezaji wa mradi huo unafanikiwa kuanzia ngazi ya kijiji.
“Nahitaji kuona halmashauri ambazo
zinatekeleza mradi huu ifikapo mwezi Novemba ziwe zimeshaanza kutekeleza
majukumu yake bila vikwazo vyovyote na nipate taarifa zake mara kwa mara ili
fedha zilizotolewa na wafadhili zilete matokeo chanya,”alisema Gambo
Akizungumza wakati wa
Kikao hicho Mwakilishi Mshauri wa Taasisi ya Kimataifa ya Mazingira na
Maendeleo (IIED) Alais Morindat alisema kuwa mabadiliko ya hali ya hewa imekua ni
tishio kubwa kwa wananchi haswa wa maeneo haya ya wafugaji na ndio maana
tulianza na Halmashauri hizi kutokana na athari zilizojitokeza katika jamii za wafugaji
ambapo mifugo mingi katika maeneo yao ilipoteza uhai.
Aliongeza
kuwa mradi huu unatofauti na miradi mingine tuliyoizoea kwa sababu Jamii
inakuwa na nafasi ya kuamua jinsi Fedha za Mradi zitakavyotumika huku malengo
ya mradi yakiwa ni kuijengea uwezo Ofisi ya Raisi –TAMISEMI
katika maeneo makubwa mawili ambayo ni uimarishaji wa taasisi katika
uratibu wa mradi na uwezo wa kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kuziwezesha
mamlaka za serikali za mitaa hapa nchini ziweze kutoa elimu kwa jamii
kutambua na kutekeleza Miradi ya kukabiliana na athari ya mabadiliko ya
hali ya hewa na tabianchi
Serikali kwa
kushirikiana na wadau wa maendeleo hususan Shirika la Kimataifa la Mazingira na
Maendeleo (IIED), Haki Kazi Catalyst (HKC), Jumuiko la Maliasili Tanzania(TNRF)
chini ya ufadhili wa Serikali ya Uingereza (UK-aid) na Mfuko wa Umoja wa
Mataifa wa Maendeleo (UNCDF LoCAL) itatekeleza mradi huu katika Halmashauri 15
huku zaidi ya Bilioni 6 zinatarajia kutumika katika mradi huu.
No comments:
Post a Comment