WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amefunguka tena kuhusiana na utawala wa serikali ya awamu ya tano huku akisema hakuna mtu anayemtakia mabaya Rais John Magufuli katika kutimiza majukumu yake.
Aidha, Lowassa aliyechuana vikali na Rais Magufuli katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 wakati alipogombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) huku akiwakilisha pia muungano wa vyama washirika vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NCCR-Mageuzi, NLD na Chama cha Wananchi (CUF), alisema kila mtu anamtakia mema Rais Magufuli ili atekeleze vyema haki na demokrasia nchini.
Lowassa aliyasema hayo juzi usiku wakati akihojiwa Jijini Nairobi, Kenya na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kuhusiana na hali ya kisiasa nchini.
Kabla ya juzi, Lowassa alishazungumza mara kadhaa pia kuhusiana na mtazamo wake juu ya hatua mbalimbali za Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli.
“Hakuna mtu ambaye anamtakia mabaya Mheshimiwa Magufuli. Kila mtu anamtakia mema… atekeleze haki na demokrasia,” alisema.
Lowassa alisema ili kuweka vizuri hali ya kisiasa nchini, kinachotakiwa ni kufanya mazungumzo na kufikia mwafaka ambao utaleta haki na demokrasia.
“Siasa ni mazungumzo, siyo kutishia kwa mabomu, magari na mahakama. Bila mazungumzo hakuna siasa,” alisema Lowassa.
Akizungumzia utendaji wa Rais Magufuli, Lowassa alisema baadhi ya maeneo (Rais) anafanya vizuri na kwamba uchambuzi zaidi wa kazi anazozifanya kiongozi huyo unaweza kutolewa na wanataaluma wengine, akimaanisha wale wa fani za utawala na uchumi.
Alipoulizwa kuhusu yeye kuwahi kukutana na Rais Magufuli na kufanya mazungumzo naye, Lowassa alisema ni kweli wamewahi kufanya hivyo lakini mazungumzo yao yalikuwa kidogo tu na siyo ya kutosha.
Aidha, Lowassa ambaye hivi sasa ni mmoja wa wajumbe wa vikao vya juu vya Chadema, alirejea kauli za viongozi wa chama chake (Chadema) kwamba kuhusiana na kusitisha kwao maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Septemba Mosi mwaka huu juu ya kutetea haki ya kushiriki shughuli za kisiasa nchini baada ya kuombwa kufanya hivyo na viongozi mbalimbali wa dini.
“Tuliandaa maandamano baada ya kuona utendaji kazi wa Serikali ya awamu ya tano una mwelekeo wa kiimla, hivyo tukaandaa maandamano kupinga kinachofanyika, lengo kupata amani na utulivu,”alisema.
Alisema ni matumaini yake kuwa mazungumzo yakifanyika, mwafaka utapatikana kuhusiana na hali ya kisiasa nchini, na hasa ikizingitiwa kuwa jambo pekee katika amani na utulivu ni kukubali sheria za nchi zifuatwe.
Katika matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Magufuli alitangazwa mshindi baada ya kupata zaidi ya asilimia 58 ya kura zilizopigwa huku Lowassa akimfuatia katika nafasi ya pili baada ya kupata asilimia 39.97 ya kura halali zilizopigwa.
Lowassa alihamia Chadema akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kupeperusha bendera ya Ukawa baada ya kuenguliwa katika namna aliyoamini kuwa ilijaa mizengwe wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM ambao mwishowe, Magufuli ndiye aliyeibuka kidedea kutoka miongoni mwa makada 38 waliojitokeza kuwania nafasi hiyo.NIPASHE
No comments:
Post a Comment