Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,
akifuatilia mambo mbalimbali yaliyokuwa yakijadiliwa wakati wa ufunguzi
wa mkutano wa 27 kwa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi wanachama wa
Umoja wa Afrika AU ulioanza jana katika ukumbi wa KCC mjini Kigali
Rwanda. Makamu wa Rais amemuwakilisha Rais John Magufuli kwenye mkutano
huo.Picha na OMR.
KIGALI, RWANDA.
Tanzania
imeuhakikishia Umoja wa Afrika (AU) kwamba itaendelea kufanya kazi kwa
karibu na nchi wanachama wa AU katika kujadili changamoto za kiusalama
zinazolikabili Bara la Afrika kwa njia ya mazungumzo na upatanishi kama
inavyoelekeza Katiba ya umoja huo.
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan
ametoa kauli hiyo wakati akichangia mada kuhusu Hali ya amani na usalama
katika Bara la Afrika katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa
Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika hapa Kigali, Rwanda.Mheshimiwa Samia
alisema Tanzania inasikitishwa na inalaani vikali matukio ya uvunjifu wa
amani yanayoendelea kujitokeza katika baadhi ya nchi za Kiafrika kiasi
cha kutishia usalama wa raia.
Alielezea
mauaji ya Hafsa Mossi, aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki na
waziri wa zamani wa Burundi na mapigano ya hivi karibuni Sudan ya
Kusini ambapo mamia ya raia wasiokuwa na hatia waliuwawa na wengine
maelfu wameachwa bila makazi kwamba ni muendelezo wa uvunjifu wa amani
katika nchi hizo.
Aliwataka
wadau husika katika nchi za Burundi na Sudan ya Kusini kushiriki
kikamilifu katika mazungumzo yanayoendelea kwa kuwa hiyo ndiyo njia
muafaka ya kuleta amani, usalama na utulivu wa kudumu katika nchi
zao.Aidha, Makamu wa Rais ambaye alimwakilisha Rais John Magufuli katika
mkutano huo aliiomba Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuisadia Sudan ya
Kusini katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu katika mgogoro ulioikumba nchi
hiyo.
Akichangia
kuhusu mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Makamu wa Rais
alisema Tanzania kwa ujumla inaunga mkono msimamo wa Afrika wa kuwa na
viti viwili katika baraza hilo na kura ya turufu bila ya masharti
yoyote.Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo viongozi walisisitiza suala la
kuimarisha umoja baina ya nchi wanachama na kusema hiyo ndiyo nguzo
muhimu katika kukuza uchumi na ustawi wa wananchi wa Bara la Afrika.
Katika
mkutano huo kulikuwa na uzinduzi wa pasi ya kusafiria ya Afrika ambayo
ilitolewa kwa Mwenyekiti wa AU, Rais Idris Deby wa Chad na nchi mwenyeji
wa mkutano, Rais Paul Kagame wa Rwanda.Mkutano huo ambao ulizungumzia
pia gharama za kuendesha umoja huo na masuala ya haki za wanawake
ulihudhuriwa na Wakuu wa Nchi zaidi ya 35, Marais wastaafu, wake wa
Marais pamoja na viongozi wa serikali.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais

Post a Comment