TAARIFA ya hali ya wakimbizi duniani
kufikia mwaka 2015 inaonesha kwamba watu milioni 65.3 wanaishi kikimbizi
ikilinganishwa na watu milioni 59.5 kwa mwaka 2014.
Ongezeko hilo la watu milioni 5.8 katika
kipindi cha miezi kumi na mbili kimelezwa kuwa ni la kiwango cha juu
tangu kuanzishwakwa Umoja wa Mataifa.
Katika taarifa yake kuadhimisha siku ya
wakimbizi duniani (Global Trends) Shirika la Kuhudumia wakimbizi (UNHCR)
limesema dunia kwa sasa inakabiliwa na kundi kubwa la watu
waliolazimika kuyakimbia makazi yao kwa sababu mbalimbali ikiwamo
migogoro ya kivita, ubaguzi na uvunjaji wa haki za binadamu.
“Takwimu zilizopo leo hii, aina ya
migogoro iliyopo na ugumu wake kumesababisha kuwapo na wimbi kubwa la
wakimbizi tangu kuanzishwa tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa; watu
milioni 60 wameondolewa katika makazi yao duniani hapa. Kila siku janga
la wakimbizi linatangazwa katika vyombo vya habari ; watoto, wanawake na
wanaume wakipoteza maisha yao katika jaribio la kukimbia vurugu
zilizopo katika eneo lao" anasema Filippo Grandi, Mkuu wa UNHCR.
Kati ya wakimbizi milioni 65.3,
wakimbizi milioni 3.2 wako katika nchi zenye viwanda wakisubiri
kutambuliwa hadhi zao kama wakimbizi, milioni 21.3 wametawanyika duniani
kote na milioni 40.8 wamelazimika kukimbia maeneo yao lakini wapo
katika nchi zao.
Mwakilishi wa UNHCR Tanzania, Bi Chansa
Kapaya akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani
yaliyofanyika katika kambi ya wakimbizi, wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.
Imeelezwa kuwa kwa kuzingatia idadi ya
watu waliopo duniani takribani bilioni 7.349 ina maana kwamba mtu mmoja
kati ya watu 113 ama anatafuta hifadhi, amekimbia makazi yake lakini
yupo katika nchi hiyo hiyo au ni mkimbizi.
Kimsingi duniani kwa sasa kuna watu
wengi waliolazimishwa kuhama makazi ya kuliko idadi ya watu waliopo
Uingereza, Ufaransa au Italia.
Miaka 10 iliyopita, mwishoni mwa mwaka
2005, UNHCR ilirekodi wastani wa watu sita kukosa makazi kila dakika
duniani lakini sasa ni wa 24 kila dakika.
Watu milioni 1.8 walilazimika kukimbia nchi zao kwa mwaka 2015 ukilinganisha na watu milioni 2.9 mwaka 2014.
Uturuki iliorodhesha idadi kubwa ya
wakimbizi wapya wakiwamo 946,800 kutoka Syria. Urusi walikuwa na
wakimbizi 149,600 kutoka Ukraine. Na vurugu zilipoibuka Burundi mwezi
Aprili, karibu watu 123,400 walikimbilia Tanzania.
Kwa idadi hiyo Tanzania inakuwa nchi ya tatu kwa kuhifadhi wakimbizi wengi duniani.
Wakati wakimbizi wapya wa Burundi
wanaingia Tanzania,UNHCR ilikuwa katika operesheni ya kuwawezesha
wakimbizi waliopo kuendelea na maisha yao ya kawaida. Aidha katika
kipindi hiki Tanzania ilitoa uraia kwa wakimbizi wa Burundi walioingia
nchini mwaka 1972 ambao walikuwa wakiishi Tabora na Katavi na Marekani
iliwapokea wakimbizi 30,000 wa Kongo waliokuwa wakiishi Nyarugusu,
Kigoma.
Tangu kuanza kwa wimbi jipya la
wakimbizi kutoka Burundi zaidi ya watu 141,000 wamekimbilia Tanzania
kutafuta hifadhi na kuifanya Tanzania kuwa nchi inayohifadhi wakimbizi
wengi kutoka Burundi.
Asilimia 77.9 ya wakimbizi hao wapya ni
wanawake na watoto, Watoto wengi waliofika Tanzania ni wale waliozaliwa
katika ardhi ya Tanzania (63,961) wamehifadhiwa katika kambi ya
Nyarugusu, moja ya kambi kubwa duniani ikiwa na wakimbizi
131,733.Mazingira ya maisha yao yakiwa magumu. Moja ya vitu ambavyo
vinafanywa na UNHCR ni kuwatawanya wakimbizi hao ili kuleta nafuu katika
kambi hiyo.
Wakimbizi wengine wapo katika kambi za
Nduta na Mtendeli zilizofunguliwa Oktoba 2015 na Januari 2016 kwa lengo
la kupunguza msongamano katika kambi ya Nyarugusu na wakati huo huo
kutoa nafasi kwa wakimbizi wapya.
Hata hivyo Nduta haraka sana ilifikia
kiwango chake cha juu kinachopaswa kuwepo hapo Ilipofika Aprili mwaka
huu; Kambi hiyo ina wakimbizi 55,000. Wakimbizi wapya kwa sasa
wanapokelewa kambi ya Mtendeli ambapo wakazi wake waliongezeka kufikia
21,796.
Lipo eneo jingine linafikiriwa kufanywa
kambi ya wakimbizi eneo la Karago, lakini eneo hili lina matatizo ya
maji na haifikiriwi kwamba inaweza kubeba wakimbizi 50,000 wanaotarajiwa
kuingia Tanzania kutoka Burundi.
“Wahisani wa kimataifa wameweza kuitikia
wito wa kukabiliana na wimbi la wakimbizi wa Burundi na hivyo
kuipunguzia mzigo serikali ya Tanzania,UNHCR na Mashirika mengine ya
Umoja wa pamoja na taasisi zisizo za kiserikali. hata hivyo bado
kunatakiwa raslimali nyingi zaidi ili kukabilina na wimbi hilo,” anasema
Mwakilishi wa UNHCR Tanzania, Bi Chansa Kapaya.
UNHCR Tanzania imepata asilimia 40 ya
mahitaji yake kusaidia wakimbizi wa Burundi mwaka kukiwa na pengo la
dola za Marekani milioni 44.8 hadi kufikia Juni 19,2016.Kwa mantiki hiyo
fedha kwa ajili ya kusaidia wakimbizi wa Burundi wanaotarajiwa kufikia
330,000 mwishoni mwa mwaka huu zipo kidogo sana.

إرسال تعليق