

Imelda akiwa akiwa kazini
-Ashauri wanawake kuchangamkia masomo ya ufundi
“Tatizo
la ajira nchini limekuwa likiongezeka hapa nchini mwaka hadi mwaka ila
wanawake wengi ndio hawana kazi wameachwa nyuma katika sekta zote kiasi
kwamba kunahitajika ushawishi wa ziada wa kuwahimiza watoto wa kike
nchini kuachana na kasumba ya kuchagua kazi”Anasema Imelda Myovela
,mfanyakazi wa kiwanda cha TBL Arusha ambaye ni mwanamke pekee fundi wa
umeme.
Myovela
anaendelea kueleza kuwa iwapo watoto wa kike hawatapata ushawishi wa
kuwaeleza kuwa masomo yote wanayaweza wanapokuwa mashuleni na wana uwezo
wa kufanya kazi yoyote inayofanywa na wanaume kuna hatari ya wanawake
wa Tanzania kuendelea kubaki nyuma kwa kuachwa nje ya mfumo wa ajira.
Alisema
jambo la kusikitisha hata watoto wa kike wengi wanaosoma masomo ya
ufundi mara nyingi wanabadilisha kazi na wengine kuamua kukaa bila kazi
kwa kuogopa kufanya kazi walizosomea na hali hiyo ndio inasababisha kila
sehemu ya kazi hususani za kawaida kuwa na idadi kubwa ya wafanyakazi
wanaume.
Akielezea
historia ya elimu yake Imelda anasema baada ya kuhitimu masomo yake ya
sekondari mwanzoni mwa miaka ya themanini alijiunga na Chuo cha VETA
cha Dar es Salaam ambapo alisoma kozi ya ufundi wa umeme wa viwandani.
Baada
ya kuhitimu kozi hiyo na kufanya mafunzo ya vitendo,mwaka 1983
alifanikiwa kupata ajira katika kampuni ya TBL ya Dar es Salaam ambako
ameajiriwa kama fundi umeme hadi kufikia sasa.
“Kufanya
kazi katika kampuni hii kumeniwezesha kuwa na ujuzi mkubwa katika fani
hii ikizingatiwa kuwa kuna mafunzo mengi tunapata ambayo huwezi kuyapata
chuoni pia kampuni imefunga mitambo ya kisasa na inayotumia teknolojia
ya juu hivyo inahitaji uwe umebobea katika fani kwendana na mazingira ya
kazi”.Alisema.
Aliongeza
kwamba anajivunia kazi yake japo wenzake wote anaofanya nao kazi ni
wanaume na anafurahi kuona anaimudu na anaaminiwa na mwajiri wake kama
wanavyoaminiwa wafanyakazi wanaume.
Kuhusu
changamoto anazokabiliana nazo katika kazi yake alisema zipo changamoto
za kawaida kama zilizopo kwenye kazi nyingine . “Hakuna kazi isiyokuwa
na changamoto kwa kazi kama hii ya kwangu unapokuwa na watoto wadogo na
kufanya kazi za shift unakuwa na wasiwasi hata hivyo namshukuru mme
wangu ni muelewa amekuwa akinisaidia na kunitia moyo”.Alisema
Imelda
ambaye ni mama mwenye watoto watatu anasema kuwa anafurahi kufanya
kazi katika kampuni kubwa ya TBL kwa kuwa ina mifumo mizuri ya ajira
yenye maslahi mazuri ikiwemo taratibu za kuwapatia mafunzo ya mara kwa
mara wafanyakazi wake na anakiri kuwa ajira yake imemwezesha kupata
mafanikio kimaisha mojawapo ikiwa ni kuwasomesha watoto wake kwenye
shule nzuri .
“Kwenye
kampuni kama hizi tunafundishwa mambo mengi ambayo hata yanakunufaisha
ukiwa nyumbani kwako kama vile usafi wa mazingira pia kupanga bajeti
kwa kila kitu unachofanya”.Alisema
Kuhusu
mipago yake ya baadaye alisema kwa sasa hana mpango wa kubadilisha kazi
na itakapofikia wakati wa kustaafu ataendelea kufanya shuhuli zake
binafsi za kujiajiri.
Alimalizia
kwa kuwataka akina mama wajitokeze na kujiamini kufanya kazi zote bila
kuchagua kwa kuwa hakuna kazi kwa ajili ya wanaume peke yao au wanawake
peke yao na hakua kazi rahisi kila kazi ina changamoto zake. “Akina mama
tuamke na watoto wa kike changamkieni masomo ya ufundi ili muweze
kupata ajira nzuri zitakazowawezesha kuboresha maisha yenu”.Alisisitiza.

إرسال تعليق