Pages

November 19, 2015

Yaani Bungeni palikuwa hapatoshi! Kassim Majaliwa Waziri mkuu Tanzania!


Dr. Magufuli hapa ni kazi tu Baba! - AFP
19/11/2015 15:38
Hatimaye, Rais Dk. John Magufuli ametegua kitendawili cha Waziri Mkuu wa awamu ya tano baada ya kuleta jina la Kassim Majaliwa ambaye ni mbunge wa Ruangwa na wabunge kulithibitisha kwa kura 258 sawa na asilimia 73.5. Katika hali isiyo ya kawaida Rais amedhihirisha usiri utakaotawala katika serikali yake ya awamu ya hii kutokana na kufanya jina hilo kuwa siri kubwa kwa watanzania, wabunge na hata waandishi wa habari. Licha ya vyombo mbalimbali vya habari kubashiri nani atakuwa waziri mkuu na kutaja majina mengi wanasiasa wenye majina, lakini hakuna aliyekuwa na uhakika wa asilimia mia kwa mia.
Hali hiyo imekuwa tofauti na awamu nyingine ziliopita kwani hata ujuo wa bahasha ulikuwa ni tofauti kabisa na safari hii. Takribani sasa nzima wabunge, waandishi wa habari waliokuwa bungeni, wananchi ndani na nje waliokuwa akiangalia kwenye TV walijikuta wakipata shauku kubwa ya kusubiri kutajwa kwa jina hilo kutokana za utaratibu kuchukua muda mrefu. Rais, alidhihirisha usiri huo baada ya kulazimika kumtuma mlinzi wake ili aweze kuleta jina hilo moja kwa moja na kulikabidhi kwa spika.
Wakati wakiendelea kusuburi Spika wa Bunge Job Ndugai alitumia muda huo kuwaeleza wabunge taratibu zitakazofuata baada ya yeye kufungua bahasha yenye jina la Waziri mkuu. Mnamo sasa 3.31, mlinzi wa Rais alionekana akiwa anaingia katika geti la bunge huku akiwa amebeba bahasha ambayo ilikuwa imebeba ujumbe wenye jina la Waziri mkuu uliotoka kwa Rais. Wakati huo Spika alikuwa tayari amemtuma katibu mkuu wa bunge kutoka nje ya ukumbi ili aweze kurejea na bahasha hiyo. Hilo likiendelea ndani ya ukumbi wa Bunge kulikuwa kumetawala ukimya wa ajabu ambapo kila mtu alikuwa na hamu ya kujua jambo hilo haraka, na kama watu wangepimwa presha basi kila mtu presha yake ingekuwa juu. Majira ya saa 4 Katibu mkuu wa Bunge, arirejea ndani ya ukumbi wa Bunge na kumpa taarifa Spika kuwa bahasha hiyo tayari imeshawasili katika viwanja vya Bunge na Rais amemuagiza mlinzi wake wa Ikulu aweze kuileta na kumkabidhi Spika.
“Nimepokea taarifa kutoka kwa Katibu mkuu wa Bunge kuwa mambo yameshaiva na Rais amemuagiza mlinzi wake ailete kwangu na kwa kuwa mlinzi huyo ni askari ataileta moja kwa moja akiongozwa na askari ambao ni walinzi wa Bunge,” alisema Spika Ndugai. Baada ya hapo aliruhusu mlinzi huyo, aingie ambapo aliingia, huku mbele yake kukiwa na askari wa Bunge na nyuma yake pia kulikuwa na askari wa Bunge na yeye akiwa katikati yao. Wakati mlinzi huyo, aliyeleta ujumbe wa Rais akiingia ndani ya ukumbi wabunge walikuwa wakipiga makofi, na alipofika alimkaribia Spika na kumpigia saluti ndipo akamkabidhi bahasha hiyo. Spika Ndugai, alipopokea bahasha hiyo aliinyanya juu kuonyesha kwamba imekuja kwa siri huku ikiwa imegonjwa muhiri wa siri ambao ni muhuri wa moto. Akisaidiwa kufungua bahasha hiyo na Katibu mkuu Thomas Kashililah, Ndugai alisema, nimefungua bahasha ya kwanza ndani yake kuna bahasha nyingine nafungua tena bahasha ya pili na bahasha ya tatu ndiyo iliyobeba karatasi yenye jina la Waziri Mkuu.
Ndugai alisema, barua hiyo imeandikwa na Rais Magufuli kwa mkono wake mwenyewe na si kuchapwa kwa komputa. Alilisoma jina hilo, ambapo wabunge walisimama huku wabunge wa CCM wakionekana kumafuta Majaliwa ili wampongeze, ambaye hakuwemo ndani ya ukumbi huo wakati jina lake likitajwa. Spika baada ya kukamilisha kazi hiyo aliahirisha bunge kwa muda wa saa moja ili kumpa nafasi Katibu wa Bunge kwenda kuandaa wasifu wa Waziri mkuu.
Wakati huo huo, Katibu muhutasi wa Waziri mkuu, Kasim Majaliwa, Angle Nyoni amemuelezea kuwa ni kiongozi makini na mchapakazi aliye na uwezo wa kufanya kazi usiku na mchana. Akizungumza na UHURU katika mahojiano maalum Ofisini kwake TAMISEMI mjini hapa, katibu muhutasi huyo alisema kuwa anafuraha isiyo na kipimo baada ya bosi wake kuteuliwa kuwa waziri mkuu wa awamu ya tano. Alieleza, kuwa yupo katika ofisi hiyo ya TAMISEMI toka mwaka 2010, hivyo anafahamu vyema utendaji kazi wake.Pia alisema, amekuwa naye kwa muda wa miaka mitano toka mwkaa 2010 kwa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI-Elimu). Alisema, Waziri Mkuu Majaliwa ni msikivu, makini, mtaratibu, mvumilivu na mtu wa kutaka ushauri kutoka kwa watu wengine bila kujali cheo cha mtu akiwemo yeye.
Katibu muhutasi huyo alifafanua, kuwa kwa nafasi ya cheo hicho alichopewa Majaliwa anastahili na bila shaka atakitendea haki. “Anafaa cheo hiki kwa asilimia 100, mana hana dharau kwa kila mtu, hana makundi, nilikuwa nikimtania kwamba bosi unaweza ukajikuta wewe ndio jina lako linaletwa na unakuwa waziri mkuu, yeye alikuwa naniambia haiwezekani kutokea kitu kama hicho,” alisema Angle. Alisema, baada ya kusikia Spika wa Bunge akitaja jina la Kassim Majaliwa alipomaliza kufungua bahasha zilizoletwa na Rais alifurahi sana na kurukaruka huku akimtukuza Mungu na kumshukuru kwa kuwapatia watanzania kiongozi hodari na mchapa kazi!
Hata hivyo alisema, alipokuwa akisikia sifa za mtu anayetakiwa kuwa Waziri mkuu zikitajwa tajwa katika akili yake aliona kabisa kuwa Bosi wake anafaa kushika nafasi hiyo kwani sifa zote anazo. “Hapa nilipo simu yangu imekuwa‘busy’ kwa muda tangu jina hilo lilipotajwa nikipokea simu za pongeza kutoka kwa watu mbalimbali, hakika ninafuraha ya ajabu na ninamuombea kwa mungu ampe afya njema wakati wote ili aweze kutekeleza majukumu hayo makubwa aliyopewa,”alisema.
Alisema, chaguo la Rais Magufuli kwa kwa Majaliwa limetimia na hajakosea kumteua kwani hatomuangusha na anampongeza sana kwa uteuzi huo. Sambamba na hilo alizungumzia usiri uliokuwepo wakati wote watanzania wakisubiri nani atakuwa Waziri mkuu alisema usiri wa Rais ulikuwa wa ajabu na haijapata kutokea vipindi vingine. Alisema, watu walikuwa wakijaribu kubashiri na kutaja majina ya watu mbalimbali ya wanaoweza kushika wadhifa huo, licha ya kuwa magazeti mengine yalimtaka Majaliwa lakini yalikuwa hayana uhakika mia kwa mia. Alishauri, usiri huo uendelea katika serikali ili mambo yanayokuwa yakipangwa yasiweze kujulikana kabla ya kufikia muda wa kujulikana. “Kasi ya Mheshimiwa Rais kwa kweli Mheshimiwa Majaliwa naweza, tena anaweza bila kulala,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...