Na Kulwa Mayombi, EANA
Arusha, 1 Novemba 2015
(EANA)--ZAIDI ya wajumbe 200 wa kada ya sheria kutoka nchi mbalimbali za Afrika
wanatarajia kuhudhuria mkutano wa siku tatu ya majadiliano kuhusu masuala ya
sheria barani Afrika unaoanza jumatano mjini Arusha.
Majadiliano hayo ambayo,
yanaratibiwa kwa ushrikiano baina ya Mahakama ya Afrika ya haki za binadamu wa
watu(AfCHPR) yenye makao yake makuu mjini Arusha na Umoja wa Afrika(AU)
,yatawaleta pamoja majaji wakuu wa nchi husika, Marais wa Mahakama za juu na
Mahakama za Katiba,wasomi na watendaji wengine wa Mahakama za Kitaifa.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa na Mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na watu,majadiliano hayo
ya masuala ya sheria barani Afrika ,ambayo hufanyika mara moja kila baada ya
miaka miwili, yana kauli mbiu isemayo 'kuunganisha sheria za kitaifa na zile
za kimataifa' ,ni ufuatiliaji wa majadiliano ya kwanza ya aina hiyo
yaliyofanyika mjini Arusha mwaka 2013.
"Majadiliano kuhusu
sheria barani Afrika yanatoa fursa muhimu ya kubadilishana maarifa kwa lengo la
kuanzisha na kukuza ushirikiano baina ya Mahakama ya Afrika ya haki za Binadamu
na watu kwa upande mmoja na Mahakama za Kikanda na zile za kitaifa kwa upande
wa pili" alisema Rais wa Mahakama ya Afrika ya haki za Binadamu na
watu,Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Augustino Ramadhani.
Jaji Ramadhani aliongeza kuwa
majadiliano hayo pia yatasaidia kukuza masuala ya utawala bora katika sheria na
kuhakikisha utoaji bora wa haki kwa wananchi wa nchi za bara la Afrika.
Washiriki katika majadiliano
hayo watajadili pamoja na mambo mengine maboresho ya sheria yanayoendelea hivi
sasa barani Afrika,hali ilivyo kuhusu sheria za haki za binadamu,utoaji
endelevu wa elimu ya sheria,usimamizi wa taasisi za sheria,usimamizi bora wa
mifumo ya Mahakama na kubadilishana uzoefu kutoka mabara mengine.
Majadiliano ya kwanza
yalizungumzia kwa ujumla mfumo wa haki za Binadamu barani Afrika na
uhusiano baina ya Mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na watu na Tume ya
Afrika ya haki za binadamu na watu.
No comments:
Post a Comment