Pages

November 8, 2015

Hawa ndio 47 waliotoswa viti maalumu CCM, Ukawa





Mchakato wa uteuzi wa wabunge wake wa viti maalumu wa Bunge la kumi na moja, umeacha simanzi kubwa baada ya orodha iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuonyesha kuwa wabunge 47 wametoswa katika vyama vya CCM, Chadema na CUF huku 33 wakipitishwa tena kuingia ‘mjengoni’.

Katika Bunge la 10 lililomaliza muda wake, CCM ilikuwa na wabunge 67 wa viti maalumu, Chadema 25 na CUF 10, hata hivyo kwa mujibu wa NEC katika uchaguzi wa mwaka huu idadi ya viti maalumu kwa CCM imeshuka hadi 64, Chadema imepanda hadi 36 na CUF ikibaki na viti 10.
Katika orodha hiyo wabunge wapya bungeni kutoka vyama vyote vitatu watakuwa79, CCM ikiwa na 39, Chadema 28 na CUF 10, akiwamo Riziki Lulida ambaye awali alikuwa mbunge wa viti maalumu CCM.

Mchanganuo uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa wabunge 36 wa CCM waliokuwapo katika Bunge la 10 wametoswa, huku 25 waliokuwa katika bunge hilo wakirejea tena.
Mchanganuo unaonyesha kuwa wabunge wanne wa viti maalumu CCM, walijitosa kugombea ubunge majimboni na kuibuka na ushindi ambao ni Mary Chatanda (Korogwe Mjini), Dk Prudenciana Kikwembe (Kavuu), Magreth Sitta (Urambo Mashariki) na Stella Manyanya (Nyasa).
Ester Bulaya alikuwa mbunge wa viti maalumu CCM, lakini alikihama chama hicho na kujiunga na Chadema na kugombea ubunge jimbo la Bunda Mjini na kuibuka mshindi. Anna Abdallah alistaafu siasa.

Baadhi ya wabunge wenye majina makubwa CCM waliotoswa ni Zarina Madabiba ambaye ni mke wa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, aliyekuwa Naibu Waziri wa wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Pindi Chana, aliyekuwa mwenyekiti wa Bunge, Lediana Mng’ong’o, Zainabu Kawawa, Diana Chilolo, Sarah Msafiri, Dk Maua Daftari na Ritha Kabati.

Chadema
Kwa upande wa Chadema wabunge tisa wa zamani wametemwa ambao ni Christina Lissu, Raya Hamisi, Rebecca Mngodo, Christowaja Mtinda, Maulida Komu, Mwanamrisho Abama, Naomi Kaihula, Rachel Mashishanga na Lucy Owenya.

Wabunge wa zamani wa viti maalumu walioteuliwa tena ni Sabrina Sungura, Joyce Mukya, Mariam Msabaha, Susan Lyimo, Cecilia Paresso, Conchestar Rwamlaza, Rose Kamili na Grace Kiwelu.
Chama hicho kimepata sura mpya 28, akiwemo Katibu wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Grace Tendega na Jesca Kishoa ambaye ni mke wa aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila.

CUF
Kwa upande wa CUF wameteuliwa wabunge tisa wapya ambao ni Riziki Lulida, Mgeni Kadika, Raisa Mussa, Salma Mwassa, Riziki Mngwali, Hadija Ally, Halima Mohammed, Saumu Sakala, Miza Haji pamoja na Savelina Mwijage ambaye alikuwa mbunge wa viti maalumu 2005-2010.
Kati ya wabunge 10 wa zamani wa viti maalumu wa chama hicho, Naibu Katibu Mkuu-Bara, Magdalena Sakaya ndiye mbunge pekee aliyegombea ubunge wa jimbo na kushinda wengine tisa hawakuteuliwa.
-Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...