Meza kuu katika warsha ya wadau wa ajira kwa vijana iliyofadhiliwa
na Mpango wa Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada
(IDRC) na kuratibiwa na ESRF. Kutoka kushoto ni Afisa kutoka Wizara ya
Kazi na Ajira kitengo cha Ajira, Joseph Nganga, Mkurugenzi wa Kazi
katika Wizara ya Kazi na Ajira, Ally M. Ahmed, Mkuu wa utafiti na
machapisho Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Profesa
Fortunata Makene, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel na Mratibu Kazi wa
Shirika la Kimataifa la Kazi (ILO) Dk. Annmarie Kiaga.(Picha zote na
Zainul Mzige wa Modewjiblog)
Na Mwandishi wetu
PAMOJA
na kuwepo na maendeleo ya kuridhisha katika suala la ajira kwa vijana,
serikali imekiri kwamba ukosefu wa ajira bado ni tatizo kubwa duniani na
kwa taifa kwa ujumla.
Kutokana na hali hiyo suala la ajira kwa vijana limebaki kuwa ajenda kuu nchini.
Kauli
hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Kazi katika Wizara ya kazi Ally M.
Ahmed wakati akifungua warsha ya siku moja ya wadau wa ajira kwa vijana
iliyofanyika hoteli ya Double Tree by Hilton.
Alifanya ufunguzi huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Eric Shitindi.
Alisema
Tanzania inaendelea kukabiliana na tatizo la ajira kutokana na wigo
mdogo wa fursa za ajira, tatizo la utaalamu na ukosefu wa uzoefu .
Alisema
hata hivyo vijana wanaoamua kujiajiri wenyewe wamekuwa wakikabiliana na
tatizo kubwa la mtaji, maeneo ya kufanyia kazi na utaalamu katika
ujasiriamali utakaowawezesha kuendesha miradi wanayoibuni.
Alisema
kutokana na uwapo wa sera, mipango na miradi ya maendeleo kuhusu ajira
kwa vijana inayoendeshwa kitaifa na kimataifa kumekuwepo na dalili njema
za kupungua kwa ukosefu wa ajira.
Alisema
utafiti wa mwaka 2014 (ILFS) umeonesha kwamba ukosefu wa ajira
umepungua kutoka asilimia 11.7 kwa mwaka 2006 hadi kufikia asilimia 10.3
ka mwaka 2014 huku kwa vijana (wenye umri wa miaka 15 hadi 35)
ukipungua kutoka asilimia 13.2 kwa mwaka 2006 hadi asilimia 11.7 kwa
mwaka 2014.
Mkuu
wa Utafiti na mchapishi wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii
(ESRF), Profesa Fortunata Makene akitoa hotuba ya utangulizi katika
warsha ya vijana na ajira iliyofanyika hoteli ya Double Tree by Hilton.
Katika hotuba yake ya ufunguzi alitoa wito wa washiriki kuangalia kwa
undani tatizo la ajira kwa vijana na kutoa mwelekeo utakaosaidia watunga
sera kuwa na sera madhubuti kuhusu ajira kwa vijana.
Alisema
mafanikio yaliyopatikana hayaondoi ukweli kuwa kuna tatizo kubwa la
ajira miongoni mwa vijana na kutokana na mazingira ya sasa ni vyema
wadau wa ajira kuangalia kwa undani tatizo la ajira la sasa ili kutoa
ushauri wa kukabiliana nalo kwa kipindi kifupi na kirefu.
Shitindi
alisema kwamba serikali inafurahishwa na juhudi zinazofanywa na wadau
mbalimbali kutafuta majibu ya tatizo la ajira, majibu ambayo alisema
yakifanywa vyema yatasaidia sana wataalamu wa serikali kutengeneza sera
na kanuni zitakazo kidhi haja.
Alisema
ipo haja kwa wachambuzi (watafiti) kuelekeza nguvu zao katika kutafiti
soko la ajira ili kusaidia watengeneza sera kuona mahitaji ya soko
katika miaka kadhaa ijayo.
Alisema
wakati uchumi wa Tanzania unakua kwa asilimia 7 kwa mwaka kwa miaka
kumi iliyopita ajira zimekuwa haziendi sambamba na ukuaji wa uchumi na
hivyo kuleta maswali mengi ya sintofahamu.
Alisema
serikali kwa sasa inataka kuhakikisha kwamba inaboresha upatikanaji wa
ajira lakini hilo linawezekana kama taasisi zake zinazotengeneza sera na
kuweka mipango zinatambua tatizo na kuona namna ya kuliangalia.
Alisema
watafiti wana wajibu mkubwa wa kusaidia serikali kuwezesha vijana kuwa
na kazi zenye staha kama sera ya ajira ya taifa inavyotaka.
Mkurugenzi
wa kazi wizara ya kazi na ajira, Ally Msaki Ahmed, akisoma hotuba kwa
niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Ajira, Eric Shitindi katika
warsha ya kitaifa ya ajira kwa vijana iliyofanyika hoteli ya Duble Tree
by Hilton. Katika hotuba yake aliwataka washiriki kujadili kwa makini
matatizo ya vijana na kutoa suluhu itakayosaidia watendaji kutunga sera
na kutoa mwelekeo mpya wa kukabiliana na tatizo hilo.
Alisema
kwa kuangalia ukuaji wa kisekta, sekta ambayo sasa hivi inahitaji watu
ndio ambayo haina wataalamu wa kutosha na hivyo ukuaji wa sekta hizo
kama za mawasiliano hauendi sanjari na utaalamu uliopo katika soko.
Katibu
Mkuu huyo alitoa wito kwa watu binafsi na serikali kuhakikisha kwamba
wanakabiliana na vikwazo vya ajira kwa kutoa elimu na taaluma ili fursa
zionekane na kutumika ipasavyo.
Alisema
tija inaweza kuonekana katika ukubwa wa utaalamu, ubunifu na namna
mafunzo yanavyowawezesha wanafunzi kuwa na uhakika na kazi wanazotaka.
Alisema
ipo haja kwa wadau mbalimbali kushirikiana na serikali katika
kuhakikisha kwamba vijana wanaingizwa katika soko la ajira na tatizo la
ajira linapunguzwa.
Kiongozi
Mpango wa ukuaji na ajira wa taasisi hiyo, Shirika la Utafiti ya
Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada (IDRC), Dk. Arjan de Haan
akielezea sababu za taasisi hiyo kuunga mkono tafiti kwa ajili ya
kusaidia kupatikana ufumbuzi wa tatizo la ajira katika warsha ya ajira
na vijana iliyofanyika Double Tree by Hilton hotel.
Katika
moja ya maazimio yaliyotolewa na washiriki vijana, walitaka kuwepo na
mabadiliko makubwa katika utoaji elimu, ambapo walisema elimu itolewe
kwa Kiswahili lakini pia wanafunzi waandaliwe kuwa wabunifu na
kujiajiri.
Aidha wametaka kurejeshwa kwa shule za ufundi na shule maalumu kama ilivyokuwa zamani.
Walisema
vijana Wanatakiwa kushiriki katika utengenezaji wa sera na kanuni na si
kushirikishwa na kutaka matakwa yao yanastahili kuangaliwa na
kuzingatiwa ili mtu ajifunze kila anachoona anaweza kukifanya vyema.
Warsha
hiyo ya ajira kwa vijana imewezeshwa na IDRC na kuratibiwa na ESRF na
mada mbalimbali ziliwasilishwa ambazo zilichambua masuala ya elimu,
elimu ya ufundi, changamoto na fursa za vijana katika ajira.
Aidha kulikuwa na mada za majukumu ya serikali na sera katika kuboresha mchakato wa ajira kwa vijana.
Mchumi
na Mshauri huru Bi. Mahjabeen Haji akiwasilisha mada kuhusu hali ya
ajira kwa vijana nchini katika warsha ya vijana na ajira ilyofanyika
hoteli ya Double Tree by Hilton, katika mada yake alielezea mazingira ya
ajira ambapo elimu katika sekta zinazokua kwa kasi kama Tehama ni
kikwazo kikubwa katika kuwezesha ajira kwa vijana.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof.
Elisante Ole Gabriel (kulia) akijadiliana jambo na Mkuu wa Utafiti na
mchapishi wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Profesa
Fortunata Makene wakati warsha hiyo ikiendelea.
Mkurugenzi
wa Salama Foundation, Shadrack John Msuya akiwasilisha mapendekezo ya
vijana juu ya namna ambavyo vipaji, elimu na ubunifu vinavyoweza
kutengeneza ajira kwenye maeneo ya Sayansi, Teknolojia, Kilimo na
Ufugaji.Moja ya azimio ni kuwa na sera mpya ya vijana yenye mpango
mkakati na tafiti zinazotekelezeka katika warsha ya vijana na ajira.
Mshauri
mwelekezi katika uanzishwaji na uendelevu wa biashara na maendeleo ya
jamii, Gidufana Gafufen akiwasilisha mapendekezo yaliyowasilishwa katika
vikundi nini kifanyike ili vijana wapende kilimo katika warsha ya
vijana na ajira iliyofanyika katika hoteli ya Double Tree by Hilton.
Pichani juu na chini ni sehemu ya wadau pamoja na makundi ya vijana waliohudhuria warsha ya wadau wa ajira kwa vijana iliyofadhiliwa na Mpango wa Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada (IDRC) na kuratibiwa na ESRF.
Mmoja wa washiriki akitoa maoni kwenye warsha ya wadau wa ajira kwa vijana iliyofadhiliwa na Mpango wa Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada (IDRC) na kuratibiwa na ESRF.
Picha ya pamoja ya washiriki wa warsha ya wadau wa ajira kwa vijana iliyofadhiliwa na Mpango wa Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada (IDRC) na kuratibiwa na ESRF.
Pichani juu na chini ni wadau kutoka Taasisi mbalimbali walioshiriki warsha hiyo wakibadilishana mawazo.
Mratibu Kazi wa Shirika la Kimataifa la Kazi (ILO) Dk. Annmarie Kiaga (kulia) akiteta jambo na baadhi ya washiriki.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof.
Elisante Ole Gabriel (kushoto) akifurahi jambo na Mtafiti Mwandamizi
ESRF, Dk. Georgina Ole Saibul mara baada ya kumalizika kwa warsha hiyo.
No comments:
Post a Comment