Mgombea Urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa akimnadi mgombea
Ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Daniel Rumenyela wakati wa mkutano wa
kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Mwanga Community Center, mkoani
Kigoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Kigoma. Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema,
Edward Lowassa amewaahidi wakazi wa mkoa wa Kigoma kuwa atajenga bandari
ya kisasa ikiwa watamchagua kuwa rais wa awamu ya tano katika uchaguzi
mkuu ujao.
Lowassa ambaye alitua mjini hapa kwa chopa
akitokea Nguruka na Kalinze alikofanya mikutano ya kampeni, alisema
mbali ya bandari pia atajenga reli ya kati ya kisasa (standard gauge).
Lowassa
aliipiga kijembe Serikali akidai imekumbuka shuka kumekucha, baada ya
hivi karibuni Waziri wa Uchukuzi, Samwel Sitta kusema kuwa Serikali ipo
katika hatua za mwisho kuanza ujenzi wa reli hiyo.
Katika
mkutano huo wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Mwanga Community
Centre, Lowassa alisema: “Ninataka mnipe kura nikafanye mabadiliko ya
kweli kwa kila Mtanzania. Nitahakikisha unafanyika uvuvi wa kisasa
katika Ziwa Tanganyika na Bandari ya Kigoma lazima ijengwe iwe ya
kisasa.”
Lowassa anayegombea urais kwa tiketi ya
Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa alitumia dakika 11 kuzungumza na
wananchi hao, akisema akiwa rais atahakikisha Watanzania wanajenga
nyumba bora na kuwa na makazi ya kisasa. “Tutatunga sera kuhakikisha
tunaondoa nyumba za nyasi nchi nzima. Lazima tufanane na mataifa
mengine, hatuwezi kubaki nyuma kila siku,” alisema.
Awali
ilizuka hali ya sintofahamu katika uwanja huo kutokana na wananchi
waliokuwa wamekaa nyuma ya uwanja huo kuonekana kupingana na kilichokuwa
kikizungumzwa na viongozi wa Chadema kwa kunyoosha mikono juu, lakini
mara baada ya Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe kupanda jukwaani na
kuzungumza, hali ya kupinga ilibadilika wakaanza kuwashangilia.
Mbowe
alisema kuwa lengo la Ukawa ni kuipeleka CCM likizo kutokana na
kushindwa kuwaletea maendeleo wananchi. “Hatuwezi kujenga umoja kwa
kutumia vyama 20, tutajenga taifa kwa kuuganisha nguvu na kushirikiana.
Vyama vya mageuzi kazi yake kubwa ni kupambana na chama kilichopo
madarakani.”
Mkoa wa Kigoma ni kati ya mikoa ambayo ni
ngome ya vyama vya upinzani, ushindani umeongezeka zaidi baada ya
aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema, Zitto Kabwe
kujitosa kugombea ubunge jimbo la Kigoma Mjini kwa tiketi ya
ACT-Wazalendo kupambana na kada wa zamani wa Chadema, Dk Amani Kaburou
anayegombea kupitia CCM.
Lowassa alisema akichaguliwa atafuta michango na ada ya shule, kubadili mfumo mzima wa elimu ili uwe na manufaa kwa wananchi na kuwawezesha vijana kujiajiri.
Lowassa alisema akichaguliwa atafuta michango na ada ya shule, kubadili mfumo mzima wa elimu ili uwe na manufaa kwa wananchi na kuwawezesha vijana kujiajiri.
Aidha,
alisema ataanzisha kilimo cha umwagiliaji, kuwawezesha vijana kupata
ajira, kufufua kilimo cha michikichi kwa kuanzisha viwanda vya kuzalisha
mafuta ya mawese kutokana na zao hilo.
“Umeme ni kero
kubwa sana, lakini nawaahidi kuwa nitalishughulikia kuhakikisha kuwa
umeme unakuwa si kero tena. Kama niliweza kutoa maji kutoka Ziwa
Victoria kwenda katika mikoa mbalimbali sitashindwa kutoa maji katika
Ziwa Tanganyika kuwafikia wananchi wa Kigoma,” alisema Lowassa.
Mbunge
wa Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi aliyemaliza muda wake,
David Kafulila alisema Kigoma ni ngome ya upinzani na itadhihirika
katika uchaguzi mkuu, huku akisisitiza kuwa mwaka huu ni wa mabadiliko
na kwamba wanashindana na CCM isiyokubalika kokote.
“CCM
imepoteza uhalali kitaifa na kimataifa na hata misaada kutoka nje
haipati tena. Marekani imezuia misada ya Dola 700 milioni. Lowassa ana
sababu na sifa zote za kuwa rais wa nchi hii. Ukimtizama na kumsikiliza
unaona anatosha kuunganisha Waislamu na Wakristo, Watanzania na raia wa
nchi nyingine,” alisema Kafulila.
Alisema Lowassa ana rekodi ambayo haina shaka na tangu ajiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008 Serikali ya Awamu ya Nne imeyumba.

إرسال تعليق