Chama cha Mapinduzi kinapenda kutoa taarifa kuhusu masuala kadhaa.
Mwenendo wa Kampeni
Kwa
kifupi, Mgombea Urais, Ndugu John Pombe Magufuli na Mgombea-Mwenza
Ndugu Samia Suluhu Hassan, wanaendelea vizuri na kampeni. Kila mmoja
anafanya mikutano na wananchi kati ya 8 hadi 11 kwa siku na kukutana na
maelfu kwa maelfu ya wananchi. Tunawashukuru wananchi wanaokuja kwenye
mikutano yetu. Tunawashukuru pia makada wa CCM wanaojitolea kwa hali na
mali kukipigania Chama cha Mapinduzi na kumtafutia kura Ndugu Magufuli.
Tunaridhika
sana na mwenendo wa kampeni yetu. Katika nusu hii ya pili ya kampeni
tutaongeza kasi na msukumo wa kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa mbinu
na mikakati mipya.
Midahalo ya Wagombea
Tumeshangazwa
na kauli ya Ndugu Kajubi Mukajanga, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari
Tanzania kwamba CCM haijathibitisha kushiriki mdahalo. CCM ilipokea
mwaliko wa MCT na kuijibu kwa barua ya tarehe 13 Septemba 2015 yenye
kumbukumbu CMM/OND/M/190/132 iliyosainiwa na Ndugu Stephen Msami,
Msaidizi wa Katibu Mkuu. Barua hiyo ilipelekwa na kupokelewa kwa
dispatch ambayo nakala yake tunayo. Baada ya hapo, Katibu Mkuu wa CCM,
Ndugu Abdulrahman Kinana, alifanya kikao na wawakilishi wa MCT katika
Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba ili kutaka kujua zaidi na kutoa maoni ya CCM
kuhusu utaratibu mzima wa mdahalo. Katika kikao hicho, ambapo MCT
iliwakilishwa na Afisa wake, Ndugu Allan Lawa, pamoja na Ndugu Tido
Mhando, CCM ilithibitisha tena kushiriki mdahalo. Tatu, tarehe 16
Septemba 2015, CCM ilitoa kauli rasmi, iliyosainiwa, ikithibitisha
kushiriki mdahalo. Kauli ya Ndugu Mukajanga inalenga kuwasaidia kisiasa
wale ambao hawajathibitisha au hawana nia ya kuthibitisha kushiriki. Kwa
msingi huu, tunaamini ni vyema mdahalo huu ukaandaliwa na ushirika wa
taasisi mbalimbali zilizokuwa na nia ya kuandaa midahalo, (kama vile CEO
Roundtable, UDASA, Twaweza) ili kuiondolea uwezo taasisi moja, au
kikundi cha watu wachache, kuhodhi na kuwa na ukiritimba kwenye jambo
hili kubwa na muhimu.
CCM inapenda kusisitiza yafuatayo:
1. Ndugu Magufuli amekubali kushiriki mdahalo wa wagombea Urais
2. Mdahalo uwashirikishe wagombea wenyewe na sio wawakilishi wao.
3. Wagombea wote, hasa wa vyama vikuu, wawepo na washiriki.
Tunapozungumzia
mabadiliko katika nchi maana yake ni utayari wa kufanya mambo mapya
yenye tija ambayo hayajawahi kufanyika, ikiwemo mdahalo wa wagombea
Urais. Wanaohubiri mabadiliko huku wakiogopa kushiriki mdahalo
wanahubiri mabadiliko hewa.
Utafiti wa TWAWEZA
CCM
haikushangazwa na matokeo ya utafiti wa taasisi huru ya Twaweza
yaliyotangazwa jana ambayo yanatoa ushindi wa asilimia 65 kwa Ndugu John
Pombe Magufuli dhidi ya asilimia 25 za Mgombea wa UKAWA.
Hatukushangazwa na matokeo ya utafiti huu kwasababu tano:
1.
Siku UKAWA walipomteua Ndugu Edward Lowassa kuwa mgombea wao ndio siku
CCM ilipohakikishiwa ushindi katika uchaguzi wa mwaka huu. CCM
hatukumteua kwasababu tuliamini hakuna namna ambapo Watanzania wengi
watamchagua.
2.
Katika uchaguzi wa mwaka huu CCM tunafanya utafiti wetu wa ndani wa
kisanyansi kila wiki kujua mwenendo na mwelekeo wa kampeni na maeneo
yanayohitaji nguvu mahsusi. Tangu tuanze utafiti wetu mwishoni mwa mwezi
Agosti, karibu kila wiki asilimia za ushindi wa CCM hazijawahi kushuka
chini ya asilimia 60 na zimekuwa zinapanda.
3.
Kazi kubwa anayofanya mgombea wetu, Ndugu John Pombe Magufuli, na
mgombea-mwenza, Ndugu Samia Suluhu Hassan, kuzunguka nchi nzima kwa
barabara na kuongea moja kwa moja na wapiga kura inazaa matunda.
Wanawafikia wapiga kura wengi, hasa wa vijijini, na wapiga kura hao
wanawaelewa.
4.
Kampeni kubwa zinazofanywa na wagombea Ubunge na Udiwani wa CCM na
makada na viongozi wa Chama katika ngazi zote nchi nzima kila siku
kumuombea kura Magufuli nazo zinazaa matunda.
5.
Tunaamini pia migogoro ndani ya UKAWA katika kipindi hiki cha uchaguzi
iliyopelekea mitafaruku katika kuachiana majimbo na, baadaye, kutokana
na uteuzi wa Mgombea Urais wa UKAWA, kupelekea kujiuzulu kwa viongozi wa
muda mrefu na maarufu wa UKAWA, Profesa Ibrahim Lipumba na Dr. Wilbrod
Slaa, na migongano ndani ya NCCR-Mageuzi, yote haya yamepunguza imani ya
wananchi kuhusu uwezo wa vyama hivi kushika dola.
Lakini
vilevile matokeo ya utafiti huu ni ishara kwamba Watanzania wamempokea
na kumuelewa Ndugu Magufuli na wako tayari kumkabidhi nchi.
Sisi kama CCM kuna baadhi ya mambo tumeyachukua katika utafiti huu na tutayafanyia kazi ili kujihakikishia ushindi.
Tumeshangazwa
na taharuki, hasa kutoka miongoni mwa wasomi na wanaharakati, kuhusu
matokeo ya utafiti huu. CCM ilitegemea kwamba jamii ya wasomi na
wanaharakati ingefurahia utamaduni wa tafiti za kisiasa unaoanza
kujitokeza hapa nchini ili siku zijazo tujikite katika kurekebishana
kwenye kanuni za utafiti na ithibati na uhakiki wa ubora. Tunasikitika
kwamba yanawekwa mazingira ya kutisha na kukatisha tamaa (atmosphere of
intimidation) kwa watu wanaotaka kufanya tafiti za kisiasa nchini.
Utafiti
ni sayansi. Matokeo ya utafiti hupingwa kwa matokeo ya utafiti
mwingine, sio kwa kuponda tu au kwa matusi na vitisho. Ni vyema
tukajifunza kupokea habari mbaya bila taharuki.
Itakumbukwa
kwamba, mwezi Agosti 2010, taasisi ya utafiti ya kimataifa ya Synovate
ilitoa utafiti ikionyesha kwamba CCM itashinda Uchaguzi Mkuu wa 2010 kwa
asilimia 61. Baadhi ya wana-CCM hawakufurahishwa na matokeo ya utafiiti
huo kwasababu waliamini kwamba ushindi wetu ulikuwa ni mkubwa zaidi.
Wapinzani waliwalaani, kuwatukana na hata kutaka kuwashtaki Synovate.
Kwenye matokeo halisi ya kura, CCM ilipata asilimia zilezile 61
zilizotabiriwa na Synovate.
Ni vyema kuweka akiba ya maneno kwenye masuala haya.
Imetolewa na:
January Makamba
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM
23.09.2015
|
No comments:
Post a Comment