MWANANCHI
“Anakatwa, hakatwi” ndilo swali lililokuwa linaulizwa nchi nzima jana, lakini hatimaye Kamati Kuu ya CCM iliyokutana hadi usiku wa manane iliibuka na jibu kwamba Edward Lowassa amekatwa, huku kukiwa na wingu zito baada ya wajumbe watatu kupingana na uamuzi huo.
Muda mfupi baada ya kikao hicho, pamoja na kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,Nape Nnauye alikataa kutaja majina yaliyopitishwa, akaunti ya Twitter ya CCM, iliwataja waliopitishwa kuwa ni Bernard Membe, Dk John Magufuli, Dk Asha Rose Migiro, January Makamba na Amina Salum Ali na kuwatupa wengine 33 akiwamo Lowassa.
“Kikao cha Kamati Kuu kimeisha salama. Kesho (leo) Halmashauri Kuu itakutana kuanzia saa 4:00 asubuhi,” alisema Nape baada ya kikao hicho.
Alipotakiwa kutaja majina ya makada watano waliopitishwa, Nape alisema: “Nimeambiwa mchakato bado unaendelea na kesho (leo) Halmashauri Kuu itakutana kuendelea na kazi. Kwa hiyo nawakaribisha kesho kuanzia saa 4:00 asubuhi mje mchukue picha, habari, karibu sana.” Mkutano Mkuu utafanyika saa nane mchana leo.”
Dakika chache baada ya kikao hicho kumalizika, wajumbe watatu wa Kamati Kuu, wakiongozwa na mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi waliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa wanapinga uamuzi huo ambao hawakuutaja, wakidai kuwa si majina yote yaliyowasilishwa mbele ya kamati hiyo.
Dk Nchimbi, akiongozana na mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisana mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sofia Simba waliwaeleza waandishi wa habari mara tu baada ya mkutano wa Kamati Kuu kuwa kikao hicho hakikufuata kanuni kwa kuwa majina machache yaliwasilishwa na hayakuhusisha mgombea anayekubalika.
Ingawa hawakumtaja mgombea huyo waliyesema anatajwa na wengi, wajumbe hao wanafahamika kuwa wanamuunga mkono Lowassa.
Baada ya kikao hicho taarifa za wagombea hao zilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii na mijadala ya wazi ilianza kuhusu uamuzi wa kumtosa Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Mmoja wa makada watano waliopitishwa kwenye mchujo huo aliithibitishia Mwananchi kuwa jina lake limepita, lakini akasema hataki akaririwe na badala yake akamshauri mwandishi aangalie akaunti ya twitter ya CCM baada ya nusu saa.
Habari za jina la Lowassa kukatwa zilizagaa tangu jana asubuhi, ilipoelezwa kuwa CCM ilifanya majadiliano na wadau mbalimbali kuangalia jinsi ya kudhibiti watu wanaounga mkono baada ya kupata taarifa kuwa ameenguliwa.
Awali wakati Kamati Kuu ya CCM ikikutana jana usiku kupitisha majina ya makada watano walioomba kuwania urais, jina la Edward Lowassa ndilo lililotawala mijadala mingi kwenye mitandao ya kijamii, likiambatana na swali moja; amekatwa, hajakatwa?
MWANANCHI
Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete alilazimika kutafuta ushauri kutoka kwa watu mbalimbali kwa ajili ya kuwezesha kazi ya mchujo wa wagombea urais kuisha salama, chama hicho kilisema jana.
Kikao cha Kamati Kuu, ambacho ratiba ya awali ilionyesha kingefanyika Julai 9, hakikuweza kufanyika kama ilivyopangwa na badala yake kilifanyika jana jioni mpaka usiku, hali iliyosababisha vikao vingine kuchelewa kuanza pia.
Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema mwenyekiti huyo alikuwa akitafuta ushauri kwa watu mbalimbali na ndio maana vikao hivyo vya juu havikuweza kufanyika katika muda uliopangwa.
Nape alisema sababu nyingine ya kuchelewa kwa vikao hivyo ni shughuli za chama na Serikali alizokuwa akizifanya Rais Kikwete, ambaye juzi alizindua ukumbi mpya wa chama hicho na baadaye mchana alihutubia Bunge kwa ajili ya kulivunja.
“Mwenyekiti alikuwa na vikao mbalimbali vya consultation (mashauriano) na wadau ili kuhakikisha vikao vinakwenda salama,” Nape.
Hata hivyo, Nape hakuelezea vikao vya mashauriano kati ya Rais Kikwete na Serikali vilihusisha makundi gani.
Lakini Rais Kikwete kwa mujibu wa Katiba ni Amiri Jeshi Mkuu na pia ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Taifa inayohusisha majeshi yote na wadau wengine.
Hata hivyo, kumekuwa na minong’ono mingi kwamba baadhi ya kambi za wagombea wenye nguvu na ushawishi zilikuwa zikiendelea na vikao usiku kucha kwa ajili ya kuweka mikakati ya jinsi ya kufanikisha azma za wagombea wao.
Licha ya kambi hizo pia kumekuwa na makundi ya wapambe wa wagombea waliojazana katika maeneo mbalimbali ya mji wa Dodoma, kwa kila kundi kutambia kundi jingine kwamba lazima washinde kwa namna yoyote, hali iliyoonekana kuashiria uwezekano wa kutokea uvunjaji wa amani.
Polisi wamekuwa wakifanya doria kwenye maeneo yenye baa kwa ajili ya kuwalazimisha wamiliki kufunga sehemu hizo za biashara kwa mujibu wa muda uliowekwa kisheria.
Kwa mujibu wa ratiba ya awali iliyotangazwa na Nnauye, Kamati ya Maadili na Usalama ya Taifa ilikuwa ifanyike Julai 8 na kufuatiwa na Kikao cha Kamati Kuu (CC) Julai 9 na kisha kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa jana na kufuatiwa na mkutano mkuu leo na kesho.
Kutokana na sababu hizo, Nnauye alisema Kamati ya Maadili na Usalama na CC vingefanyika jana kabla ya NEC kukutana leo na kuendelea na Mkutano Mkuu.
MWANANCHI
HABARILEO
Uongozi wa Rais Jakaya Kikwete unaotarajiwa kuondoka madarakani mwishoni mwa mwaka huu, pamoja na changamoto mbalimbali, utakumbukwa kwa mafanikio yaliyojidhihirisha kitakwimu na katika maisha ya watu.
Takwimu alizotangaza juzi katika hotuba yake ya kuaga wabunge, zimeonesha kuwa mafanikio ya uongozi huo wa Awamu ya Nne, yameanzia katika kupunguza baadhi ya gharama za maisha na kuongeza kipato cha wananchi.
Mbali na hatua hizo, ubora wa maisha ya Watanzania katika wakati wa uongozi huo ulioongozwa na kauli mbiu ya ‘Maisha Bora kwa Kila Mtanzania’, umeonekana kuanzia katika ongezeko la umri wa kuishi kwa watanzania, kupungua kwa udumavu wa watoto na ubora wa makazi ya wananchi.
Moja ya mbinu ya kupunguza gharama za maisha duniani ni kuongeza kipato cha watu, ambapo Rais Kikwete katika hotuba yake ya juzi, alieleza namna alivyoongeza mshahara wa wafanyakazi na kupunguza kodi inayokatwa katika mishahara hiyo.
Rais Kikwete, wakati alipoingia madarakani mwaka 2005, alikuta mshahara wa kima cha chini ni Sh 65,000, huku kodi inayokatwa katika mshahara huo (PAYE), ikiwa asilimia 18.
Katika jitihada za kumpunguzia mwananchi gharama za maisha, Rais Kikwete alisema Serikali yake ilianza kuongeza mshahara wa kima cha chini ambapo sasa anaondoka ukiwa Sh 300,000 kwa mwezi, huku kodi hiyo ikiwa asilimia 11.
Mbali na hatua hiyo iliyogusa moja kwa moja kundi kubwa la wananchi wanaofanya kazi, jitihada za uongozi huo zilisababisha pato la Taifa kuongezeka kwa asilimia saba na kuwa miongoni mwa nchi 10 Afrika na nchi 20 duniani zenye uchumi unaokua kwa kasi.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, pato ghafi la Taifa (GDP), limeongezeka zaidi ya mara tatu kutoka Sh trilioni 14.1 mwaka 2005, hadi kufikia trilioni 79.4 mwaka 2014.
Kwa mafanikio hayo, kitakwimu pato la wastani la Mtanzania nalo limeongezeka kutoka Sh 441,030 mwaka 2005 hadi Sh 1,724,416 mwaka 2014.
Shughuli za kiuchumi zilizofanyika ndani ya nchi, ikiwemo katika uzalishaji wa mazao ghafi mpaka mazao ya viwandani na kuuzwa kama huduma na bidhaa nje ya nchi, wameongezeka kutoka mauzo ya dola za Marekani bilioni 1.6 mwaka 2005, mpaka Dola za Marekani bilioni 8.67, mwaka jana.
MTANZANIA
Hatimaye jina la katibu Mkuu wa Chadema Dk Wibroad Slaa limeteuliwa na UKAWA kuwa mgombea wake wa nafasi ya Urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka ndani ya kamati inayounda kamati kuu ya UKAWA imesema jina la Slaa limepitishwa na idadi kubwa ya wajumbe baada ya kutokea mvutano mkubwa miongoni mwa vyama vinavyounda umoja huo.
Baadhi ya wajumbe wa kamati maalumu inayoongozwa na viongozi wa kitaifa jana walithibitisha kuteuliwa kwa Slaa kwa kueleza kuwa tayari jina lake limeshapitishwa na linatarajiwa kutangazwa rasmi baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati hiyo.
Aidha walieleza kuwa watatangaza wagombea wenza.
Ibrahim Lipumba ambaye awali alitangaza kuitaka nafasi hiyo, atautumia mkutano huo baina ya viongozi wa Ukawa kuliondoa jina lake ili kumpisha Slaa kugombea ili kulinda maslahi mapana na mafanikio ya Umoja huo.
No comments:
Post a Comment