Pages

July 15, 2015

TANZANIA YAELEZEA MATUMAINI YAKE KWA MKUTANO WA UFADHILI WA MAENDELEO

Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Saada  Mkuya Salum akizungumza  katika siku ya pili ya mkutano wa tatu wa kimataifa kuhusu ufadhili wa  maendeleo ( FFD3) unaoendelea jijini Addis Ababa- Ethiopia
Na   Mwandishi Maalum, 
New York
Mkutano wa tatu wa kimataifa  kuhusu ufadhili wa maendeleo, ( FFD3) jana (jumanne) umeingia siku yake   pili ambapo  Waziri wa  Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Saada   Mkuya Salum alielezea matumaini ya   Tanzania  juu ya matokeo ya mkutano huo katika kusukuma mbele ajenda ya maendeleo endelevu.
 Waziri   wa Fedha ambaye anamwakilishi  Mhe. Rais Jayaka Mrisho Kikwete katika mkutano huo,  amesema kuwa,  Tanzania  inaamini  kwamba ufadhili wa  maendeleo ni moja ya ajenda muhimu kwa Bara la Afrika .  Kwa sababu hiyo Tanzania,   inategemea  kuona ufadhili huo  unakuwa na  matokeo makubwa   katika kuondoa umaskini katika   nchi nyingi za Afrika.
“  Kama kweli  tunataka kuwa na utekelezaji wa uhakika wa  malengo ya maendeleo endelevu baada ya 2015, Matumaini ya  nchi yangu ni kuona   kuwa mkutano huu unatoka na  matarajio mathubuti yatakayo hakikisha mtiririko  usio shaka wa  rasilimali kuchagiza maendeleo”. Amesema Mhe.Waziri
          Ametoa  wito wakuwapo kwa    mikakati ya   pamoja  baina ya   pande zote, kule zitokako au  asili ya  raslimali  hizo na  nchi zinazopokea misaada hiyo  lengo  likiwa  kudhibiti  mrititiko wa fedha chafu, uwezeshwaji wa kukomboa raslimali na kuzirejesha  raslimali  hizo kwa nchi husika.
“ Afrika inapoteza  karibu  dola  bilioni 50 kwa mwaka kutokana na  mtiririko wa fedha chafu kutoka nchi zinazoendelea,  hali inayosababisha  kusababisha uhaba mkubwa wa   hazina ya fedha za kigeni,  kupungua kwa makusanyo ya kodi,  kufutwa  vyanzo vya uwekezaji uwekezaji na hatimaye kuongezeka kwa umaskini”. Amesema  Waziri  wa Fedha.
Kiongozi huyo wa ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo,  ameelezea umuhimu wa    Mkakati wa Addis Ababa kujielekeza  na kuwa mfumo  madhubuti utakaoimarisha ushirikiano katika masuala  ya kodi.
 Vile vile Waziri wa fedha,  amesisitiza kwamba takwimu zitakazotumiwa na Taasisi ambazo zitapewa  jukumu la  kufuatilia na kufanya marejeo  kuhusu ufadhili  wa maendeleo , takwimu hizo ni  lazime zitoke  katika   taasisi za takwimu ambazo zinatambuliwa na serikali ya nchi husika.
Akabinisha kwamba  matumizi ya  takwimu  rasmi kutoka  taasisi zinazotambuliwa na serikali , kutaepusha  kutumiwa  kwa takwimu  ambazo si rasmi na hivyo kusababisha sitofahamu  na migongano  kati ya  Nchi wanachama na   Umoja wa Mataifa.
Waziri Saada Mkuya Salumu  akatoa wito   wa   kuongezwa raslimali fedha  hususani kwa nchi  zinazoendelea   ili ziwe  na uwezo wa kuboresha mifumo  yake ya  ukusanyaji wa takwimu, kuzichambua na kuzifanyia tathmini.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...