Pages

July 12, 2015

POMBE ACHAGULIWA RASMI DODOMA KUPEPERUSHA BENDERA YA CCM NGAZI YA URAIS KATIKA UCHAGUZI OKTOBA 25 MWAKA HUU.




Waziri wa Ujenzi, Dk Magufuli ambaye ameteuliwa na CCM kuwania nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu ujao. Picha ya Maktaba.

Dodoma. Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi leo umemtangaza Dk John Magufuli kuwa mgombea wa urais kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu. 

Dk Magufuli amepata asilimia 87 ya kura zote za wajumbe, huku wengine walioingia tatu bora; Balozi Amina Salum Ali akipata asilimia 10.5 na Dk Asha Rose Migiro akipata asilimia 2.4. 


Mkutano Mkuu ulipiga kura jana usiku chini ya usimamizi wa Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais Jakaya Kikwete. 


Dk Magufuli alifanikiwa kufika katika hatua ya tatu bora akiwa na watangaza nia wengine; Dk Asha Rose Migiro na Balozi Amina Salum Ali. 


Watatu hao walifanikiwa kuingia hatua hiyo ya mwisho ya kupigiwa kura na mkutano mkuu baada ya kuwabwaga makada wengine wawili, Bernard Membe, ambaye alikuwa akipewa nafasi kubwa kutokana na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuenguliwa na Kamati Kuu juzi, na January Makamba katika kura zilizopigwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu. 


Awali kabla ya kupigiwa kura na Mkutano Mkuu jana, Kikwete aliwataka wajumbe kumuunga mkono mgombea atakayepitishwa kupeperusha bendera ya chama hicho na kuachana na makundi. 


“Wagombea wapo watatu na wote wana sifa za kuwa Rais. Halmashauri Kuu imewapitisha kwa kujiridhisha na tabia na mienendo yao na atakayepitishwa ataiongoza nchi yetu vizuri. Anatakiwa apatikane Rais zaidi yangu ili tusonge mbele. Tunataka rais atakayefanya mambo zaidi yangu,” alisema JK. 


“Tumevuka hatua ya makundi na sasa tunatafuta mgombea wa chama na si mgombea wa kundi au mgombea binafsi. Wagombea urais waliojitokeza walikuwa 38 na makundi lazima yalikuwa mengi. Tukipata mgombea mmoja makundi yanatakiwa kuyeyuka.” 


Hisia za wajumbe kwa Dk Magufuli zilionekana wazi wakati makada hao walipopewa dakika 15 za kujieleza mbele ya Mkutano Mkuu, huku mwenyekiti akiweka sharti la kuzuia kushangilia hata kama wakiguswa. Lakini sharti hilo lilionekana kuwasumbua wajumbe hao na mara kwa mara wakajikuta wakilipuka na kushangilia. 


John Pombe Magufuli 
Akijinadi kwenye mkutano huo, Dk Magufuli, ambaye alizungumza kwa dakika tisa kuanzia saa 5:55 hadi saa 6:04 usiku, aliwashukuru wajumbe wa mkutano huo, wakiwamo wageni waalikwa na muda huo wajumbe wakaanza kumshangilia. 


“Naombeni kura kwa sababu ninaamini kuwa nitafanya kazi na nyinyi na mtanituma na nitakuwa mwakilishi wenu na nitailinda CCM katika kushinda kikamilifu na kushika dola ili kuiongoza nchi hii. Nitadumisha Muungano wetu,” alisema Magufuli.


“CCM imenilea na ninawaahidi wajumbe sitawaangusha. Nimefanya kazi na Rais Kikwete na nadhani sikukuangusha. Umenituma katika kipindi chote cha miaka 10 na nilidhani leo utataka nielezee barabara ulizonituma wewe.” 


Magufuli alisema anatamani kueleza jinsi alivyojenga madaraja, barabara, lakini hawezi kwa kuwa mkutano huo ni wa kuomba kura na akafafanua kuwa kazi ya uongozi ni ya kupokezana vijiti. 


“Viongozi waliopita wamefanya kazi nzuri na mimi nafarijika kuona nimejifunza vya kutosha katika kipindi hicho na sitawaangusha na nina uhakika hapa ninapozungumza wapinzani huko walipo wapo matumbo joto maana maendeleo hayana chama ila lazima yaletwe na chama kinachojua kujisimamia,” alisema. 


Magufuli aliwageukia viongozi wakuu wa CCM waliokuwa wamekaa meza kuu na kuwaomba kura sambamba na wajumbe wengine wa mkutano huo, baada ya hapo aliwapa mikono viongozi hao na kuimba kidogo kupitia kipaza sauti. 


Amina Salum Ali 
Balozi Amina, ambaye alizungumza kwa dakika 11 kuanziaa saa 5:35 mpaka saa 5:46 usiku, alieleza uzoefu wake wa miaka 38 ya utumishi ndani ya CCM na miaka 42 ya utendaji serikalini. 


Alisema amelelewa na viongozi wakuu wa chama hicho akiwamo Rais Kikwete na kufafanua kuwa hana kundi ndani ya CCM hivyo atawaunganisha na kuwa kitu kimoja. 


“Naomba mnichague ili tutoke Dodoma tukiwa na ushindi. Taifa letu lipo katika uchumi wa kati na tunatakiwa kwenda katika uchumi wa juu hivyo ni lazima tuendeleze mazuri yaliyofikiwa na Serikali ya Awamu ya Nne,” alisema. 


Kuhusu Muungano alisema ataudumisha kwa kila hali na kusisitiza kuwa Muungano hauwezi kudumishwa kama chama hakitakuwa na viongozi imara. 


Kilipofika kipindi cha maswali, hakuna mjumbe hata mmoja wa mkutano huo aliyejitokeza kumuuliza swali kama ilivyokuwa kwa wagombea wote watatu ambao hawakuulizwa maswali. 


Asha-Rose Migiro 
Dk Migiro, ambaye kipaumbele chake ni kukuza uchumi utakaowafikia Watanzania wengi, alizungumza kuanzia kwa dakika tano tu kuanzia saa 5:48 mpaka saa 5.53 usiku.


Alisema kwa kutumia uzoefu wake wa uongozi na elimu atadumisha na kusimamia Muungano na mchakato wa kupata Katiba Mpya na kwamba ataongoza nchi kwa kufuata ilani ya CCM. 


“Nipeni ridhaa yenu ili niweze kuipeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu huu. Nipeni kura usiku huu ili niweze kusonga mbele,” alisema Migiro. 


Membe amfuata Lowassa 


Awali jana usiku, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) ilipitisha majina matatu ya makada wanaowania urais kwa tiketi ya chama hicho, ikiwa imeandika historia mpya kwa kupitisha kwa mara ya kwanza wanawake wawili, huku kigogo mwingine, Bernard Membe akitemwa. 


Dk John Magufuli, Dk Asha Rose Migiro na Balozi Amina Salum Ali ndio waliopita kwenye mchujo huo wa Halmashauri Kuu na majina yao kupelekwa kwenye Mkutano Mkuu ambao ulianza saa 3 usiku. 


Kada mwingine aliyekuwa amepita kwenye tano bora juzi, January Makamba, hakufurukuta mbele ya Halmashauri Kuu na aliungana na Membe kuaga licha ya awali kupewa nafasi kubwa ya kushinda baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuenguliwa na Kamati Kuu ya chama hicho Ijumaa usiku. 


Hii ni mara ya kwanza kwa wanawake kufika hatua ya tatu bora katika mchakato.mwananchi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...