Kiongozi
wa kitaifa wa mradi wa CFIT, Prof. Ralph Masenge akimkaribisha mgeni
rasmi Kaimu Kamishina wa Elimu, Benjamin Kulwa (hayupo pichani)
kufungua kongamano linalohusu upitiaji wa waraka wa mafunzo ya Tehama
kwa wakufunzi wa vyuo vya ualimu linalofanyika mjini Bagamoyo.
Kaimu
Kamishina wa Elimu, Benjamin Kulwa akisoma hotuba kwa niaba ya
Kamishina wa Elimu, Profesa Eustella Bhalusesa wakati akifungua rasmi
kongamano linalohusu upitiaji wa waraka wa mafunzo ya Tehama kwa
wakufunzi wa vyuo vya ualimu linalofanyika mjini Bagamoyo. Kulia
ni Ofisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa
la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) nchini, Al Amin Yusuph.
Na Mwandishi wetu, Bagamoyo
KAMISHINA wa Elimu, Profesa Eustella Bhalalusesa amesisitiza
haja ya kuhakikisha kwamba viwango vya umahiri vya Tehama kwa wakufunzi
wa vyuo vya ualimu nchini vinakua vya juu kukidhi haja ya matumizi ya
kufundishia na kujifunza nchini.
Alitoa
kauli hiyo mjini hapa wakati akifungua kongamano linalohusu upitiaji
wa waraka wa mafunzo ya Tehama kwa wakufunzi wa vyuo vya ualimu.
Katika
hotuba yake iliyosomwa na Kaimu Kamishina wa Elimu, Benjamin Kulwa
alisema kwamba changamoto ya Tehama inaonekana wazi katika matumizi yake
na hivyo wakufunzi lazima wawe mahiri.
"Duniani
kote, sekta ya uchumi, fani mbalimbali, taasisi na hata mifumo ya
maisha yanategemea sana matumizi ya Tehama kwa sasa. Kadhalika,
maendeleo makubwa katika Tehama yamebadili namna mambo yanavyofanyika,”
alisema.
Alisema
kwa kuhakikisha kwamba kuna maendeleo ya kutosha ni vyema walimu kuwa
na umahiri unaotakiwa kwani Tehama inachangamoto nyingi zinazotakiwa
kuangaliwa ili kuweza kuitumia ipasavyo kuleta mabadiliko katika jamiii.
Aliwataka
washiriki kuhakikisha kwamba wanapitia muswada huo kwa makini na
kujazia maeneo yote ambayo wataalamu wameshindwa kumaliza na kusaidia
kuweka mtaala huo vyema kwa mafunzo.
Kongamano
hilo ambalo ni sehemu ya mradi wa kuimarisha uelewa kwa wanafunzi na
wakufunzi vyuo vya walimu ili kuboresha matumizi ya Tehama katika
mafunzo hasa masomo ya sayansi limeshirikisha wataalamu mbalimbali na
kuendeshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni
(UNESCO) kwa kushirikiana na watu wa China.
Alisema kwamba serikali inatambua kuwa Tehama inaweza kutumika vyema katika kubadili na kuboresha mfumo wa elimu Tanzania.
Aidha
alisema Sera mpya ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 inatambua umuhimu
wa Tehama katika kuboresha viwango vya elimu nchini Tanzania.
Alisema
moja ya malengo ya sera ni kuonesha mahitaji halisi ya Tehama nchini
katika upande wa wataalamu na vifaa ili kufanikisha utoaji wa elimu hata
ya masafa katika ngazi zote.
Kongamano
hilo ni moja ya mradi wa China Funds in Trust Project (CFIT) wa UNESCO
na serikali ya China wenye lengo la kusaidia serikali ya Tanzania
kuimarisha umahiri wa wakufunzi na walimu kwa kuwawezesha kujua tehama
na kuitumia.
Mradi
huo umelenga kuongeza uwezo wa vyuo vya walimu na teknolojia ya kisasa
ya Tehama na vifaa vyake ili kusaidia kujifunza na kufunza.
Ingawa
kwa sasa vyuo vinavyofanyiwa kazi na mradi huo vipo viwili vipo vingine
vinane vinavyofunza walimu wa sayansi na hesabu vitaingizwa.
Pichani
juu na chini ni washiriki wa kongamano linalohusu upitiaji wa waraka wa
mafunzo ya Tehama kwa wakufunzi wa vyuo vya ualimu wakati kongamano
hilo likiendelea mjini Bagamoyo.
Kiongozi
wa kitaifa wa mradi wa CFIT, Prof. Ralph Masenge (kushoto) akijadili
jambo na mgeni rasmi Kaimu Kamishina wa Elimu, Benjamin Kulwa
(katikati). Kulia ni Ofisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa
Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) nchini, Al
Amin Yusuph.
Kiongozi
wa kitaifa wa mradi wa CFIT, Prof. Ralph Masenge (kulia), akifurahi
jambo na Ofisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la
Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) nchini, Al Amin Yusuph
(katikati) pamoja na Mratibu wa kitaifa wa mradi wa CFIT kutoka UNESCO,
Faith Shayo (kushoto) mara baada ya kufunguliwa rasmi kwa kongamano
linalohusu upitiaji wa waraka wa mafunzo ya Tehama kwa wakufunzi wa vyuo
vya ualimu.
Mgeni
rasmi Kaimu Kamishina wa Elimu, Benjamin Kulwa (walioketi wa pili
kushoto) katika picha ya pamoja na washiriki wa warsha hiyo
inayomalizika jana mjini Bagamoyo.
No comments:
Post a Comment