May 25, 2015
KUTANA NA KANALI MSTAAFU WA JWTZ ANAYEPILWA TSH22,000 TU KAMA PENSHENI LAKINI AMEFUNDISHA WANAJESHI WAPYA 30,000 KUANZISHA JESHI LA TZ.
Kanali mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Ameen Kashimir, ameilalamikia serikali kwa kutotambua mchango wake licha ya kuinusuru serikali wakati wa maasi ya jeshi hilo ya mwaka 1964.
Kadhalika, alisema pamoja na mchango wake kwa taifa mpaka sasa analipwa Sh. 22,000 kwa mwezi kama mafao ya uzeeni.
Kashimir ambaye alikuwa afisa wa kwanza kupata Kamisheni Jeshi la Tanganyika Rifles, kabla ya uhuru na baada ya uhuru, alikuwa Mnadhimu Mkuu wa kwanza wa jeshi hilo ambaye alifanya mambo mbalimbali ikiwemo kuwafundisha wanajeshi 30,000 kwa ajili ya kuanzisha jeshi jipya.
Hayo aliyasema jana jijini Dar es Salaam wakati alipohojiwa na waandishi wa habari wakati wa uwasilishwaji wa video kuhusiana na historia ya maisha yake.
Alisema mchango wake katika jeshi umesahaulika licha ya kwamba umesaidia kujenga msingi wa jeshi kutoka askari 50 waliobakia baada ya waasi na kuanzisha jeshi jipya la wanajeshi 30,000.
Alisema jeshi hilo lilikuwa imara na lilionyesha uhodari wake katika vita dhidi ya Idi Amini wa Uganda.
Kashmir alisema, yote waliyoyafanya yamesahaulika. “Kwa mimi binafsi nilibaki na cheo cha Kanali wakati nilitakiwa kuwa Meja Jenerali sasa hapa labda kulikuwa na ubaguzi wa aina fulani au sijui ni nini lakini nadhani serikali inatakiwa kuangalia suala la maofisa wa zamani.”
“Kwa mfano Jenerali Mstaafu Mirisho Sarakikya mafao anayopata ni Sh. 50,000 kwa mwezi na mimi napatiwa Sh. 22,000 na kama nisingekuwa na akili timamu na nguvu ningekuwa maskini na kuomba omba,” anasema.
Aliomba serikali ifikirie upya waliojitolea na kusaidia kujenga jeshi linaloonekana sasa wakumbukwe katika michango yao.
Aidha, alisema vijana wanatakiwa kuiga mfano wao kwa kuwa walikuwa ni wazalendo na nchi yao.
Alisema kuonyeshwa kwa video hiyo kutasaidia vijana kuelewa kazi walizokuwa wakizifanya katika kujenga nchi.
Alilishauri jeshi kuwa la kisasa lenye silaha za aina mbali mbali zinazotumia teknolojia mpya.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa chuo kikuu, Profesa Issa Shivji, alisema mchango wa mtu binafsi unakumbusha suala la historia na kwamba ni jambo zuri kukumbukwa kwa Kanali Kashmir kwani baada ya kutokea waasi wa jeshi mwaka 1964 ni nchi pekee Afrika ilivunja jeshi lake na kuunda jeshi jipya.
Alisema hatua hiyo ni muhimu kwa upande wake kwa kuwa ilikwenda sambamba na kizazi kile kujenga utaifa.
Profesa Shivji alisema wanapoangalia michango ya watu wanatakiwa kujikumbushia historia zao kwani ilikuwa na dira kwa nchi hivyo ni muhimu wakakumbukwa.CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment